WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema vijana wa Tanzania wapatao 497 wanaosoma katika
vyuo mbalimbali vilivyoko kwenye mji wa Wuhan nchini China wote wapo
salama.
Kwa sasa Mji
wa Wuhan umewekewa zuio hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka wala kuingia,
lengo likiwa ni kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo. Mlipuko wa
virusi vya corona ulianzia katika mji wa Wuhan.
Ametoa kauli
hiyo leo (Jumapili, Februari 16, 2020) kwenye Kumbukumbu ya Mazazi ya
Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida
Textile Mills (T) ltd, na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini
Dar-es-Salaam. Watu zaidi ya 1,500 wamefariki dunia kutokana na mlipuko
wa virusi hivyo.
Waziri Mkuu
amesema kutokana na zuio hilo wakazi wote wa mji huo wakiwemo vijana wa
Kitanzania wanapata huduma mbalimbali kupitia njia ya mtandao ukiwemo
ununuzi wa bidhaa mbalimbali.
“…Hakuna
usafiri hata wa umma unaofanya shughuli za kusafirisha watu katika mji
wa Wuhan kila mmoja anaetakiwa abakie katika makazi yake na kwamba
Serikali ya China na uongozi wa vyuo unawatunza wanafunzi wote wakiwemo
na Watanzania.”
Waziri Mkuu
amesema kwamba kwa sasa Wachina wameimarisha utoaji huduma kwa njia ya
mtandao hata kama mtu anataka kununua kitu ananunua kwa njia ya mtandao.
“Kama kijana ameishiwa basi atumiwe fedha kwa njia ya mtandao ili aweze
kujikimu wakati huu wa zuio.”
Waziri Mkuu
amesema jambo la muhimu kwa sasa ni usalama wao na kujali maelekezo
yaliyotolewa na Serikali ya China juu ya usalama wao pamoja na wananchi
wengine walioko katika eneo hilo.
Amesema
Serikali imeweka mitambo ya kupima watu katika maeneo yote ya mipaka na
kwamba inawataka wananchi washirikiane nayo katika kuhakikisha watu wote
wanaoingia nchini wanapita kwenye njia sahihi.
Pia, Waziri
Mkuu amerua kuwataka Watanzania waendelee kuwa watulivu na kuitegemea
Serikali katika kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala
mbalimbali zikiwemo na ya mlipuko wa virusi hivyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...