Na Woinde Shizza, Michuzi TV Arusha
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimekiagiza kiwanda cha Kuzalisha dawa za Mifugo, viatilifu na vifungashio cha Farm Access LTD, kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 20 ya sasa na kufikisha asilimia 100 ili kukidhi mahitaji ya mifugo nchini.
Kauli hiyo ameitoa mapema jana wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Ngaramtoni nje kidogo ya jiji la Arusha sanjari na kuweka jiwe la msingi katika jengo jipya la uzalishaji ambapo alisisitiza kwamba iwapo kiwanda hicho kitakidhi malengo ya asilimia 100 kitaisaidia serikali kupunguza gharama kubwa za uagizaji wa dawa za mifugo nje ya nchi.
"Kwa kuwa mmeeleza wenyewe kuwa soko la bidhaa zenu ni kubwa ni lazima muongeze uzalishaji kutoka asilimia 20 na kufikia asilimia 100 na muweze kusambaza hizi dawa maeneo mengi hapa chini jambo hilo litasaidia kupunguza matumizi ya fedha nyingi za serikali kuagiza bidhaa hizi nje ya nchi" Alisema Mpina.
Awali mkurugenzi wa biashara wa kiwanda hicho cha Farm Access, Danny Ngowi alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kuagiza na kusambaza dawa za mifugo kutoka nje ya nchi lakini kutokana na changamoto ya baadhi ya dawa kutokuwa na ubora wameamua kuanzisha kiwanda hicho na kutengeneza dawa hizo zikiwa na bora wa kiwango cha juu.
Alisema kiwanda hicho kimekuwa cha kwanza kutengeneza na kusambaza dawa za mifugo na viatilifu kwa ajili ya soko la ndani na hiyo ni mwitikio wa sera ya serikali ya uanzishaji wa viwanda.
Alisema wakati wanaanzisha kiwanda hicho walipata changamoto ya mtaji kutoka taasisi za fedha lakini baadaye mabenki mbalimbali yalijitokeza na kuonyesha nia ya kutoa fedha za mkopo ikiwemo benki ya maendeleo ya kilimo ,mifugo na uvuvi(TADB) ambayo imesaidia sana kuinua kiwanda hicho kwa kuwezesha mkopo mkubwa.
"Kiwanda hiki kikikamilika kitatoa ajira za moja kwa moja kwa watu zaidi ya miatatu na wale wasio na ajira za moja kwa moja wapatao 500 na kitachangia pato la serikali kwa kulipa kodi" Alisema Ngowi.
Naye kaimu mkurugenzi wa mikopo na Biashara wa benki ya TADB,Jeremia Mhale alisema kuwa kiwanda hicho ni kiwanda cha mkakati kwa kuwa kimeanzishwa kwa maksudi ya kuongeza uzalishaji wa dawa za mifugo ukizingatia kwamba hapa nchini kuna idadi kubwa ya mifugo ambayo haipati huduma ya dawa na kusababisha kukumbwa na magonjwa mbalimbali.
Aliongeza kuwa benki hiyo inathamini uwekezaji mkubwa hususani katika sekta ya kilimo na viwanda na hivyo imejikita kutoa mikopo ili kuinua sekta binafsi na kuunga mkono Sera ya serikali inayohimiza uanzishwaji wa viwanda.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiangalia moja ya jengo la kiwanda cha Kuzalisha dawa za Mifugo, viatilifu na vifungashio cha Farm Access LTD
(Picha na Woinde Shizza)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...