Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kigoma

RAIS wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DK.John Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Burundi Evarist Ndayishimiye wamekubaliana mambo kadhaa yenye lengo la kuleta maendeleo katika nchi zao.

Miongoni mwa mambo hayo ambayo wamekubaliana ni kuendeleza sekta ya biashara, barabara , reli, biashara ya madini ya Nicol pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi hizo.

Akizungumza baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo ambayo yamefanyika Ikulu ndogo ya Kigoma nchini, Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye amesema kuwa Tanzania kwao ni ndugu wa damu tangu enzi za waasisi wa mataifa hayo mawili wakati wa kupigania uhuru.

Akifafanua zaidi mazungumzo hayo, Rais Ndayishimiye amesema kuwa wamejadiliana kwa kina kuhusu masuala ya kisiasa , kiuchumi na kiutamaduni na wamekubaliana kuendeleza biashara ya madini na katika kufanikisha hilo wamekubaliana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili kuitisha mkutano mapema kujadili masuala hayo.

"Tumekubaliana kuimarisha miundombinu ya barabara, reli pamoja na bandari na katika eneo la reli tutaunganisha reli kutoka Uvinza , Msongat hadi Itenga yenye urefu wa kilometa 200 ili kuchochea ukuaji wa biashara,"amesema Rais Ndayishimiye.

Amefafanua katika mazungumzo yao wamebaini katika eneo la kibiashara bado nchi hizo hazitatumia vizuri fursa zilizopo kwa kila nchi, hivyo wamekubaliana kuendelea kudumisha biashara na kwa ngazi ya kikanda wamezungumzia hali ya usalama katika maeneo ya maziwa makuu ambapo wamekubaliana kudumisha umoja.

Wakati kwa upande wa kimataifa amesema wamekubaliana kukumbushana ajenda ya Afrika kuhusu maendeleo. 

Kuhusu wakimbizi, amesema hivi sasa wakimbizi wengi wanarudi Burundi kwani hali ya amani na usalama imeimarika na kutoa mwito wale ambao wako nje ya nchi hiyo nao warudi wakashiriki katika kuleta maendeleo.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema kuwa kilichozungumzwa na Rais Ndayishimiye ndicho ambacho wamekubaliana."Mengi Rais Ndayishimiye ameyealeza na ndio ambayo tumekubaliana, Rais amechagua Tanzania kuwa nchi yake ya kwanza mara tu ya kuchaguliwa, ameonesha heshima kubwa lakini pia inaonesha ni jinsi gani Tanzania na Burundi wamekuwa ndugu.

"Kuhusu wakimbizi, naendelea kutoa mwito kwa wananchi wa Burundi warudi kwao , kwani nchi yao imetulia, na ndio maana hata wamepata mkopo wa dola za milioni 23 kwa ajili ya kujenga bandari ya Burundi Bujumbura,"amesema.

Amesisitiza ni hatua nzuri kama nchi katika kuleta maendeleo huku akitoa mwito kwa jumuiya nyingine ambazo zilikuwa zinasita na kuwekea vikwazo nchi hiyo kuviondoa.Pia amewashauri Warundi waendelee kushirikiana katika kujenga nchi yao kwani ina rutuba nzuri, madini ya kutosha na ina amaani.

Dk.Magufuli amesema wamezungumzia madini ya Nicol ambayo yapo katika eneo Msangati nchini Burundi na kwa upande wa Tanzania yapo eneo la Kabanga."Katika eneo hili la madini ya Nicol tutajenga kiwanda cha kuchenjua madini ya Nicol ili kuyaongezea thamani na kisha kuyauza na kupata fedha.

"Leo nimezungumza na Rais Ndayishimiye kuhusu kuruhusu madini ya Burundi kama dhahabu yawe yanakuja kuuzwa hapa Kigoma, kwa bahati nzuri sisi tunayo maduka ya kuuza madini,"amesema Rais Magufuli.

Akizungumzia ujenzi wa reli, Rais Magufuli amesema kupitia watalaam wa reli nchini Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Masanja Kadogosa , hawatashindwa kufanikisha ujenzi wa reli hiyo ambayo itatokea Uvinza hadi Itega na reli hiyo itakapokamilika itatumika kusafirisha madini ya Nicol.

Hata hivyo amesema bidhaa za Burundi zinasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salam kwa asilimia 98 na kwamba itakuwa vema zaidi iwapo bidhaa za nchi hizo zitakazopitishwa bandari ya Dar es Salaam ikafikia asilimia 100 ili wafanyabiashara wasiwe wanapata tabu.

Rais Magufuli amefafanua kuwa katika mwaka 2016 biashara kati ya Burundi na Tanzania zilikuwa ni bilioni 115.15 na kwa sasa imefikia bilioni 20.

Amesema kituo cha uwekezaji nchini kimesajili takribani miradi 16 kutoka Burundi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 29.42 na imetoa ajira kwa zaidi ya watu 544 huku kampuni 10 kutoka Tanzania yamewekeza nchini Burundi.

"Burundi bidhaa zake zote na mizigo yake kwa asilimia 95 inasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam, leo tumepata fursa ya kuzungumza kwa pamoja juu ya kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya Burundi na Tanzania, tunataka biashara iwe kubwa,"amesema Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na mgeni wake Rais wa Burundi,Mhe.Evariste Ndayishimiye mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...