Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kuongoza mbio za Dar Mr UK ili kusaidia uchangiaji wa fedha za watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa.
Mbio hizo zitawashirikisha viongozi wengine mbalimbali akiwemo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Viwanda na Biashara na viongozi wengi zitakazofanyika Julai 24 mwaka huu.
Katika kuokoa maisha ya watoto hayo, Mbio hizo zimelenga kukusanya kiasi cha Shilling Milioni 100 zitakazosaidia upasuaji kwa watoto wengi zaidi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, Mratibu wa Dar Mr Uk Marathon George Kohoyeo amesema mbio hizo kwa mwaka huu zinalenga kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa ambapo limekuwa kubwa kwa watoto wengi.
Amesema, huu ni mwaka wa kwanza kuanzishwa kwa mbio hizo na wameanza na uchangiaji kwa watoto hao na wanatarajia kuwa na wakimbiaji zaidi ya 3000.
"Mbio hizi zitakuwa ni endelevu na kwa mwaka huu tumeanza na uchangiaji wa kiasi cha Milion 100 kwa ajili ya matibabu ya watoto na zitakuwa endelevu kila mwaka na lengo likiwa ni kusaidia jamii,"amesema.
Kohoye amesema, kutakuwa na mbio za km 21, km 10 na km 5 zitakazoanzia Viwanja vya Leaders Club hadi Masaki na kuishia Leaders tena na washindi watapata zawadi mbalimbali kulingana na mbio alizokimbia.
Kwa upande wa Daktari Bingwa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu Dr Juma Mzimbiri amesema kuna uhitaji mkubwa sana kwa jamii kufahamu kuhusiana na ugonjwa huo ambao wakina mama wengi wamekuwa wananyanyapaliwa na kutengwa pindi mtoto wake anapokuwa anaumwa.
Amesema, watoto wengi wanaokuja katika kitengo cha Mifupa MOI wamekuwa wanapatiwa huduma kwa wazazi kununua vifaa tiba na kulipia vipimo.
"Kwa wiki tunapokea karibia wagonjwa 100 wenye matatizo ya kichw kikubwa na mgongo wazi wengine wakiwa wameshafanyiwa upasuaji na wengine wapya kwahiyo uhitaji ni mkubwa san na kipindi wakitokea wahisani tunaweka kambi na tunaweza kuwafanyia upasuaji watoto 30," amesema.
Mzimbiri amewashukuru waandaji wa Dar Mr Uk Marathon kwa kuwakumbuka watoto hao kwa kuandaa mbio zitakazotoa fursa ya uchangiaji wa fedha kiasi cha milioni 100 zitakazoweza kuweka kambi 20 nchi nzima.
Ameongezea, mataifa mengi Afrika yameathirika na ugonjwa huo unaosababishwa na ukosefu wa lishe kwa mama kipindi mjamzito kwa kukosa vitamini B Folic Acid na hivyo wameweka mkakati wa kushirikiana na taasisi ya Lishe kutoa elimu .
Mbio hizo zitakazohusisha watu mbalimbali zitakuwa na zawadi kwa washindi sambamba kupata medali, vikombe na pesa taslimu na wamewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuchangia fedha hizo.
Mratibu wa Dar Mr Uk Marathon George Kohoye (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mbio hizo zitakazofanyika Julai 24 Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...