Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameagiza Wakuu wa Wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanafuatilia na kudhibiti kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaokatisha masomo kutokana na tatizo la mimba.
Akizungumza
juzi (19.11.2021) mjini Sumbawanga Mkuu huyo wa Mkoa alionesha kutofurahishwa
na kasi ya kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaoshindwa kukamilisha masomo yao
sababu ikitajwa kuwa ni kupata ujauzito.
“Lazima
tuongeze mapambano kudhibiti mimba za utotoni .Sijafurahishwa kuona wilaya ya
Nkasi ikiwa na idadi ya wanafunzi Ishirini Tano (25) mwaka huu waliopata mimba
wakiwa wanasoma. Hii haikubaliki. Wakuu wa wilaya nendeni mkadhibiti vitendo
hivi” alisisitiza Mkirikiti.
Takwimu
za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa zimeonesha kuwa katika mwaka huu 2021 wilaya ya
Nkasi imekuwa na matukio 25 ya wanafunzi wa kike kupata mimba huku wilaya ya
Kalambo ikiripoti wasichana wanane (8) na Wilaya ya Sumbawanga nayo ikiwa na wanafunzi
wanane (8).
Mkirikiti
aliagiza pia Maafisa Elimu Kata kutimiza majukumu yao kwa kufuatilia walimu na
watu wanaojihusisha na kuwapatia mimba wanafunzi kwani zipo taarifa baadhi ya
walimu wanahusika na vitendo hivyo kinyume na maadili ya kazi.
“Maafisa
Elimu Kata mmepewa pikipiki na serikali ili zitumike kutekeleza majukumu ya
kusimamia elimu kwenye mashule ikiwemo kufuatilia wazazi na walezi wasiolea
watoto wao hatua inayopelekea baadhi ya watoto wa kike kupata mimba na watoto
wengine kuacha shule bila sababu” alisitiza Mkirikiti.
Aidha, Mkirikiti amemwagiza Afisa Elimu Mkoa
wa Rukwa Samson Hango kuhakikisha timu anayoingoza inajipanga kuchukua hatua
kali za kinidhamu na kisheria kwa walimu wote wanaoshabikia mimba za utotoni
kwenye maeneo yao.
Katika
hatua nyingine Mkirikiti ameagiza vijana wa skauti kote mkoani Rukwa kutumika
na halmashauri kubaini wazazi wanaotekelekeza watoto na kusababisha wahamie
mitaani na kuitwa ’watoto wa mtaani’ ambao wanazidi kuongezeka hususan Manispaa
ya Sumbawanga.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema atahakikisha
anashirikiana na vijana hususan skauti kufundisha vijana umuhimu wa maadili
mema ili waweze kuwa raia wema na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.
Waryuba aliongeza kusema jamii inatakiwa kuelimishwa juu ya umuhimu wa uzalendo hatua itakayosaidia kuwa na jamii bora itakayochukia maovu ikiwemo rushwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...