MAAFISA Utumishi/Utawala kote nchini wamehimizwa kujenga mahusiano baina ya ofisi zao na Wafanyakazi katika kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na kufahamu masuala yahusuyo fidia baada ya mfanyakazi kuumia au kuugua kutokana na kazi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma mjini Morogoro Jumatatu Novemba 22, 2021 kwenye kikao kazi cha kuwajengea uwezo maafisa hao walio chini ya TAMISEMI kuelewa huduma zitolewazo na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.
Alisema jumla ya washiriki 100 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Singida na Dodoma pamoja na kujifunza kuhusu usalama mahali pa kazi, pia wamejifunza namna ya kuwasilisha madai pindi mfanyakazi anapoumia kutokana na ajali, kuugua au kifo kinachotokana na kazi.
“Dhumuni kubwa la mafunzo haya ni kuwapa uelewa kuhusu , huduma zitolewazo na mfuko na hatua za kufuata wakati wa kuwasilisha madai hususan kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao (Online Notification System-ONS) inayopatikana kwenye portal.wcf.go.tz na masuala ya Usalama na Afya mahala pa kazi” Alifafanua Dkt. Mduma.
Dkt. Mduma alisema Dhamira ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwa na uchumi endelevu ambao utahakikisha Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa wa kati wa juu.
“Dhamira hii itawezekana pale ambapo tutakuwa na wafanyakazi wenye uhakika wa usalama wa afya zao katika maeneo yao ya kazi na endapo itatokea bahati mbaya wakapata madhara wakiwa wanafanya kazi basi wawe na uhakika wa kupata fidia stahiki na kwa wakati.” Alisema.
Awali Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema, mafunzo haya kwa Maafisa kutoka TAMISEMI ni endelevu kutokana na umuhimu wa maafisa hao katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na fidia kwa wafanyakazi.
Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo mmoja wa washiriki Bw. Khamisi Khatib Khamisi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Wilaya ya Mafya mkoani Pwani, alisema yamewasaidia sana kuwajengea uwezo wa kujua ni hatua gani za kufuata endapo mfanyakazi ataumia au kuugua kutokana na kazi anazozifanya.
“Na mimi nitakaporejea kwenye kituo changu cha kazi nitashirikiana na wenzangu tuwapatie elimu watumishi wilayani ili nao watambue kuwa WCF iko kwa ajili yao na endapo watapata madhara yoyote yatokanayo na kazi iwe rahisi kwao kufuata taratibu zitakazowezesha kupata haki zao kutoka WCF.” Alisema Khamisi.
Washiriki hao pia walijifunza aina za Mafao ya Fidia yanayotolewa na WCF kwa Mfanyakazi aliyeumia, kuugua kutokana na kazi na wategemezi wa mfanyaakzi aliyefariki kutokana na kazi.
Hali kadhalika walipata fursa ya kuona onyesho la hatua za kuchukua endapo mfanyakazi atapata ajali akiwa kazini na namna ya kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, akiongea na Maafisa Utumishi/Utawala kutoka TAMISEMI wakati wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo juu ya huduma zitolewazo na Mfuko Fidia kwa Wafanyakazi (WCF mjini Morogoro Novemba 22, 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...