Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam

Wanafunzi watatu wa Shahada ya Uzamili ya Taarifa na Menejimenti ya Maarifa (MIKM) kutoka Idara ya Infomatiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (DIIT) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameng’ara kwenye tuzo kubwa zinazotambua mchango wa wanahabari kwenye kuandika taarifa za sayansi na bioteknolojia Afrika kwa upande wa Tanzania (OMAs).

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo akikabidhi tuzo kwa washindi wa jumla wa tuzo hizo Bi Rebecca Kachembeho na Bi. Jackline Martine. 

Wanafunzi hao ni Rebecca Kachembeho na Jackline Martine ambao wameibukwa kwa pamoja washindi wa jumla wa tuzo hizo (Overall winner) kwa kuandika taarifa nzuri iliyohusu nafasi ya bioteknolojia kwenye kutatua changamoto za ugonjwa mnyauko wa migomba Mkoani Kagera, Changamoto za wadudu wa Pamba wanaokwamisha tija pamoja na makala kuhusu Bungua wa Mahindi na Viwavijeshi vamizi wanavyorudisha maendeleo ya wakulima nchini.

Mwandishi mwingine ambaye pia ni Mwanafunzi aliyeng’ara kwenye tuzo hizo ni Martinius Sospeter ambaye ameshika nafasi ya pili kwa upande wa magazeti kwa kuandika Makala nzuri iliyoonesha mchango wa Sayansi hasa Bioteknolojia katika kutatua changamoto za upungufu wa chakula zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, wadudu na magonjwa na nafasi ya Bioteknolojia katika kuboresha afya nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya washindi na washindi wote kwenye hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es salaam Mshindi wa jumla Bi. Rebecca Kachembeho amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kufundisha kozi ya namna ya kuandika habari za sayansi na kutafsiri matokeo ya kisayansi kwa lugha rahahisi kwa jamii ili waweze kuelewa na kutumia matunda ya sayansi.

“Tunakishukuru Chuo Chetu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuona umuhimu wa kutufundisha kozi hii na kutupatia mbinu nyingi za namna ya kuwasilisha sayansi kwa jamii, hakika imetupatia mbinu nyingi na maarifa ya kutuwezesha sasa kuitumiakia jamii yetu vizuri kwa kuwafikishia matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi ili wayatumie kutatua changamoto zinazowakabili na kuongeza ustawi wao katika nyanja mbalimbali.” Alisema Bi. Kachembeho.

Awali akieleza kuhusu tuzo hizo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu amesema tume imekuwa ikifanya kazi na Waandishi wa habari kwa miaka mingi hasa kwa kuwajengea uwezo kuhusu Uandishi wa habari za sayansi na nafasi yao katika kusaidia kufikisha matokeo ya tafiti kwa jamii.

“ COSTECH kupitia Jukwaa la bioteknolojia za Kilimo Afrika (OFAB Africa) tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana katika kuwajengea uwezo Wanahabari nchini kwa zaidi ya miaka 15 ya jukwaa hili lakini pia katika kuongeza ari ya kuhamasisha uandishi huo tumekuwa tukitoa tuzo maalumu kutambua mchango wao kila mwaka hapa Tanzania na baadae washindi huenda kushindanishwa Afrika na wamekuwa wakifanya vizuri na wengine kunyakua Tuzo hizo barani afrika kama tulivyosikia Calvin Edward Gwabara kutoka SUAMEDIA aliyeshinda Tuzo ya Afrika mwaka 2018” alifafanua Dkt. Nungu.

Aidha amewahakikishia Wanahabari ushirikiano wa kina katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao lakini pia kuendelea kuwajengea uwezo zaidi katika kuandika habari za sayansi nchini ili sayansi iweze kutoa mchango unaostahili kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Nae Mgeni rasmi katika Tuzo hizo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo amewapongeza washindi hao wote kwa kuandika habari na makala nzuri ambazo zimeweza kushawishi majaji kuzipatia ushindi hasa baada ya kutimiza vigezo vingi vilivyowekwa kuchuja ubora na kuona mchango wake katika maisha ya watu.

“Niwapongeze wote mlioshinda na wale wote zaidi ya 50 mlioshiriki kutuma kazi zenu kwenye tuzo hizi, ninaamini kama hukupata leo basi umefungua mlango wa kujipanga vizuri ili uweze kushinda kwenye tuzi zijazo, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhabarisha jamii kwenye kutumia matokeo ya sayansi kutatua changamoto zao na kuongeza tija kwao na maendeleo ya Taifa leo” alieleza Prof. Kandalo.

Aidha amesema kuwa maendeleo ya taifa lolote duniani yanategemea matumizi ya Sayansi na teknolojia na ubunifu lakini yatatokea endapo matokeo hayo ya tafiti yatafahamika kwa jamii na kuyatumia kikamilifu kama ambavyo mataifa mengi yaliyoendelea duniani yanavyofanya.

Awali tuzo zilitanguliwa na mafunzo kwa waandishi wa habari ambapo Watafiti nguli wa Bioteknolojia na wabobevu kwenye masuala ya Uandishi wa habari za Sayansi nchni walifundisha mada mbalimbali na kutoa nafasi ya mjadala mpana wa fursa zilizopo, changamoto na hatimae kuweka mikakati ya pamoja.

MATUKIO WAKATI WA UTOAJI WA TUZO HIZO.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu  akieleza kuhusu tuzo hizo na mchango wa COSTECH kwa wanahabari na sayansi.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo akizungumza kabla ya kutoa tuzo hizo. 

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia mafunzo hayo kabla ya utoaji wa tuzo kuanza.

Bwana Calvin Gwabara akipokea cheti cha ushiriki kutambua mchango wake kwenye tuzo hizo na uandishi wa habari za sayansi.

Mohamed Gojo mmoja wa wanafunzi wa SUA aliyeshiriki kwenye tuzo hizo akipokea cheti chake cha ushiriki.

Mwanafunzi Martinius Sospeter aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa magazeti akipokea cheti chake kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamsheni ya COSTECH.

Washindi wa tuzo hizo kutoka SUA  Bi. Rebecca Kachembeho (wa kwanza kushoto)  Jackline Martine (katikati) na Martinius Sospter (Kulia) wakiwa kwenye piocha ya pamoja mara baada ya kupokea tuzo zao.

Mshindi wa Jumla Bi. Rebecca Kachembeho akiwa ameshika tuzo yake mara bada ya kukabishiwa

Mshindi mwenza Bi. Jacline Martine akiwa kwenye picha na tuzo yake mara baada ya kukabidhiwa kwenye hafla hiyo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...