Uboreshaji wa viwanja vya ndege unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeivutia Kampuni ya Usafiri wa Anga ya Auric Air, ambayo imeanzisha rasmi safari mpya kati ya Kahama na Dar es Salaam, pamoja na Kahama na Mwanza.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kurahisisha usafiri wa anga na kufungua fursa mpya za biashara na utalii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari hizo, Mkurugenzi wa Mauzo wa Auric Air, Deepesh Gupta, amesema safari hizo zilianza rasmi Desemba 12, mwaka huu, na kwamba ni hatua muhimu kwa kampuni katika kuboresha upatikanaji wa usafiri wa anga ulio wa haraka, salama na wa kuaminika nchini.
Gupta amesema safari hizo mpya zimebuniwa mahsusi kukidhi ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga wenye ufanisi katika ukanda wa Ziwa na maeneo ya kati nchini.
“Kuimarishwa kwa miundombinu ya usafiri wa anga, hususan katika
Uwanja wa Ndege wa Kahama, kumetuwezesha kuongeza safari hizi. Tunaamini hatua
hii itaongeza ufanisi wa shughuli za kibiashara na kurahisisha ufanyaji wa
biashara kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa ujumla,” amesema Gupta.
Ameeleza kuwa safari hiyo itaendeshwa kwa kutumia ndege ya Auric Air aina ya Dash 8-300, yenye uwezo wa kubeba abiria 50, inayotambulika kwa uimara wake, ufanisi wa kiutendaji, mpangilio mpana wa ndani na rekodi nzuri ya usalama.
Gupta amesisitiza kuwa Kahama ni kitovu muhimu cha uchumi, hususan katika sekta ya madini na biashara, hivyo kupitia safari hiyo mpya, Auric Air inalenga kuunga mkono moja kwa moja shughuli za kiuchumi na kuboresha upatikanaji wa masoko.
Aidha, amesema mbali na safari hizo mpya, Auric Air inaendelea kuendesha safari nyingine muhimu za ndani ya nchi ikiwemo Dar es Salaam–Iringa, Dar es Salaam–Arusha na Dar es Salaam–Zanzibar, ambazo amesema ni nguzo muhimu kwa sekta za biashara, serikali na utalii.
Kwa upande wake, Ofisa wa Teknolojia, Usimamizi wa Kumbukumbu na Mipango wa Auric Air, Asha Mzuri, amesema uzinduzi wa safari hizo mpya utawawezesha wasafiri kusafiri kwa haraka, usalama na urahisi zaidi, hali itakayochochea shughuli za kiuchumi na kukuza utalii.
“Auric Air tumejikita katika kuunganisha maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuchangia maendeleo ya kitaifa kupitia usafiri wa anga. Uzinduzi huu ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kupanua mtandao wa huduma zetu ili kukidhi mahitaji ya wasafiri wote. Tunaendelea kuishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya anga nchini,” amesema Mzuri.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...