-Asema vilifanya kazi kubwa kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama hadi sasa 

-Asisitiza CCM imesikitishwa na vifo 518 vilivyotokea wakati wa vurugu, madhara mbalimbali


Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro amesema sababu kubwa ya chama hicho kupongeza vyombo vya ulinzi na usalama baada ya matukio ya Oktoba 29,2025 ni kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na vyombo hivyo katika kudhibiti vurugu na kulinda usalama wa taifa.

Amesema kazi iliyofanywa na vyombo hivyo Oktoba 29 ndio ambayo imewezesha hadi sasa Taifa la Tanzania kuendelea kuwa Taifa moja na imara licha ya kuwepo kwa dosari katika wakati ule lakini kwa sehemu kubwa vimefanya kazi nzuri ,hivyo wanapongeza.

Dk.Migiro ameyasema hayo leo Mei 28,2026 alipokuwa katika kipindi cha Kasri la Kikeke, ambapo ametumia nafasi hiyo kujibu maswali mbalimbali aliyoulizwa na alijibu kwa ufasaha mkubwa.

Balozi Dk.Migiro amesema  pamoja na changamoto na dosari zilizoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, vyombo vya dola vilifanya kazi kubwa kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama katika kipindi kigumu kilichoshuhudia vurugu katika maeneo mbalimbali nchini.

"Pamoja na dosari zilizoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, bado kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya dola ilisaidia kuzuia madhara makubwa zaidi ambayo yangeweza kulitikisa taifa," amesema Dk.Migiro.

Aidha amefafanua kuwa jukumu kuu la vyombo vya ulinzi na usalama kwa Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania jukumu lao ni kulinda mipaka ya nchi.

“Tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vilifanya kazi kubwa ya kuhakikisha nchi inakuwa salama, pamoja na kuwepo kwa dosari ndogo lakini vilifanya kazi kubwa.”

Dk.Migiro pia alitumia nafasi hiyo kukanusha madai ya kwamba vyombo hivyo hasa Jeshi la Polisi linaingia katika siasa kwa ajili ya kukilinda Chama Cha Mapinduzi ambapo alisisitiza sio kweli na kwamba vyombo hivyo ni vya Taifa na vinahudumia  Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kisiasa.

Wakati huo huo Dk.Migiro amesema CCM inaendelea kuamini katika umuhimu wa maridhiano kama msingi wa kudumisha umoja, amani na mshikamano wa Taifa baada ya matukio yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana.

Ameongeza Chama hicho kinaunga mkono juhudi zote zinazolenga kuimarisha mshikamano wa Watanzania huku kikisisitiza kwamba maridhiano ni mchakato endelevu wa kujenga taifa imara lenye amani na maendeleo.

Kuhusu ripoti ya tume ya uchunguzi iliyoundwa kufuatia matukio hayo, Dk.Migiro amesema CCM iliipokea kwa umakini mkubwa kutokana na uzito wa tukio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika miaka yote nchini ambapo amesisitiza ni tukio ambalo limeitia doa nchi na limeshutua.

Amesema  chama kilichukua muda kutafakari kwa kina yaliyotokea kabla ya kutoa msimamo wake rasmi kuhusu ripoti hiyo iliyoongozwa na Jaji Chande.

Pia alipongeza kuundwa kwa tume hiyo pamoja na kazi iliyofanywa na wajumbe wake kwa weledi mkubwa huku akiwashukuru wananchi waliojitokeza kutoa ushahidi na maoni yao yaliyosaidia kukamilika kwa uchunguzi huo.

Kuhusu  vifo vilivyotajwa kwenye ripoti hiyo, Dk.Migiro amesema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 518 akisisitiza kuwa hata kifo cha mtu mmoja ni pigo kubwa kwa taifa.

Amesema  chama hicho hakina sababu ya kupinga takwimu zilizotolewa na tume kwa kuwa zimetokana na taarifa kutoka hospitali, Msajili wa Vizazi na Vifo pamoja na vyanzo vingine rasmi.

Dk.Migiro pia alieleza kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana kulikuwa na hali ya utulivu na vyama vyote vilifanya shughuli zao kwa amani kufuatia wito wa Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan wa kufanya siasa za kistaarabu.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...