Halmashauri ya Jiji la Dodoma imesisitiza kuwa hakuna utoaji wa fedha unaotambuliwa katika mchakato wa kupata maeneo ya kufanyia biashara katika soko la Umonga, huku ikionya kuwa yeyote anayelipia eneo kwa sasa anakuwa ametapeliwa.

Akizungumza Mei 4, 2026, katika ukumbi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, amesema ugawaji wa maeneo kwa wafanyabiashara waliokuwa katika Soko la Rehema Nchimbi utafanyika mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kupitia  rasimu ya mkataba, ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa utaratibu rasmi na ulio wazi.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali yaliyolenga kuwapatia wafanyabiashara hao eneo mbadala baada ya kufungwa kwa soko lao la awali kufuatia maamuzi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.

Gondwe alieleza kuwa eneo la Umonga lililopo Mtaa wa Kitenge, Kata ya Majengo, lilipatikana baada ya kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya kufanya tathmini ya maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na viongozi wa wafanyabiashara na wataalam wa halmashauri, na kupendekeza eneo hilo kama suluhisho la kudumu.

Kwa mujibu wa Gondwe, Halmashauri tayari imeanza maandalizi ya msingi katika eneo hilo ikiwemo ujenzi wa vyoo na uwekaji wa kifusi katika maeneo yaliyokuwa na changamoto ya maji kutuama, ili kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara watakaoanza shughuli zao.

Alifafanua kuwa mpango wa uendelezaji wa eneo hilo unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa vibanda vya muda vya mita 3x3 kwa gharama nafuu, huku awamu ya pili ikilenga ujenzi wa miundombinu ya kisasa kwa matumizi ya kudumu.

Aidha, Gondwe alibainisha kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, alifanya ziara Februari, 2026 na kutembelea eneo hilo la Umonga, ambapo aliagiza kuharakishwa kwa mchakato huo pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara wanapatiwa mikataba iliyo wazi na inayoeleweka kabla ya kuanza biashara.

Hata hivyo, amesema mchakato huo umekumbwa na changamoto baada ya baadhi ya wafanyabiashara kukataa kujadili rasimu ya mkataba na badala yake kuibua madai mapya ikiwemo kuongeza idadi ya wanufaika, kudai fidia ya miezi sita na kutaka kuanza biashara bila kukamilisha taratibu za mikataba.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa halmashauri hiyo, Nsubi M. Kapula, amesema endapo viongozi wa wafanyabiashara hawatajitokeza kushiriki katika kupitia rasimu ya mkataba, halmashauri italazimika kuchukua hatua ya kukutana moja kwa moja na wafanyabiashara ili kuhakikisha shughuli zinaanza bila kuchelewa.

Amesema hadi sasa wameendelea kutoa wito kwa viongozi hao kushiriki mchakato huo, lakini endapo watakaidi, hawatasita kuchukua hatua mbadala kwa manufaa ya wafanyabiashara wote.

Kwa ujumla, halmashauri imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia mchakato huo kwa kuzingatia sheria, taratibu na maelekezo ya serikali, huku ikiwataka wafanyabiashara kuepuka matapeli na kusubiri utaratibu rasmi wa ugawaji wa maeneo ili waweze kurejea katika shughuli zao bila migogoro.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...