📍 Apandisha mishahara kwa asilimia 35


Na Mwandishi Wetu, Arusha

SERIKALI ya Awamu ya Sita imefanya mageuzi makubwa ya kiutumishi nchini kwa kupandisha madaraja watumishi wa umma 219,042, huku ikiongeza mishahara kwa asilimia 35.1, hatua inayotajwa kuwa ni kielelezo cha uongozi unaoweka mbele ustawi wa mfanyakazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameyabainisha hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na Maafisa Tawala na Rasilimali Watu katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa AICC.

Mhe. Kikwete alisema maamuzi hayo ya kimkakati yaliyopata ridhaa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanalenga kuleta "furaha na neema" kwa watumishi wa umma ili nao waweze kutoa huduma bora na kupeleka furaha kwa Watanzania wote kupitia utendaji wao.

Ongezeko la Mishahara na Sekta Binafsi

Akifafanua kuhusu neema hiyo ya kiutumishi, Waziri Kikwete alibainisha kuwa mbali na ongezeko la 35.1% kwa watumishi wa umma mwaka 2025, Serikali pia imeimarisha sekta binafsi kwa kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa 33.4% kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Alisema maboresho hayo yanagusa sekta mbalimbali za kimkakati nchini ikiwemo Afya, Elimu, Kilimo, Mawasiliano, Usafirishaji, Nishati, Viwanda, Biashara, Madini, na Utalii.

"Nimezungumza na maafisa rasilimali watu na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao wa kuleta furaha kwa watumishi. Uamuzi wa Rais Samia kupandisha madaraja watumishi zaidi ya laki mbili ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha utumishi wa umma nchini Tanzania," alisema Waziri Kikwete.

Waziri Kikwete aliongeza kuwa takwimu hizo zinaonyesha kasi ya mageuzi chini ya uongozi wa Rais Samia, ambaye amedhihirisha kwa vitendo kuwa ufanisi wa taasisi za umma unategemea sana kuimarika kwa maslahi na hali ya maisha ya watumishi.

Aliwataka Maafisa Tawala nchini kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Serikali kwa uadilifu ili watumishi wapate haki zao kwa wakati, jambo litakaloongeza morali ya kazi na tija katika kuwahudumia wananchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...