Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMUIYA ya Khoja Shia Ithna-Asheri Mkoa wa Dar es Salaam imeandaa Kambi ya Afya na Macho pamoja na Mafunzo ya Imam Hussein (a.s), yatakayofanyika kwa Agasti 14 hadi Agasti 16 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo inayotolewa bure inalenga kuwafikishia wananchi huduma muhimu za afya, hususan wale ambao hawana uwezo wa kuzipata kwa urahisi.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithna-Asheri Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mohamedraza Dewji, amesema shughuli hiyo ni sehemu ya jitihada za jumuiya hiyo za kutoa huduma kwa jamii bila kujali dini, kabila wala hali ya maisha.
Amesema kambi hiyo, ambayo mwaka jana ilihudumia maelfu ya wananchi, itawakutanisha wataalamu wa afya, taasisi mbalimbali pamoja na mashirika ya tiba kutoka ndani ya Tanzania kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Huduma hizi zitatolewa bila gharama yoyote na zinalenga kuwahudumia wananchi wote bila kujali dini, kabila au hali ya maisha,” amesema Mohamedraza.
Amesema katika kambi hiyo wananchi watapata huduma mbalimbali, zikiwemo uchunguzi wa macho, vipimo vya sukari, shinikizo la damu, uzito na urefu (BMI) pamoja na uchunguzi wa ugonjwa wa mtoto wa jicho (cataract).
Aidha, amesema wananchi wenye uhitaji watapatiwa miwani na dawa bure, huku wanawake wakipata huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, pia kutakuwa na elimu kuhusu afya ya akili pamoja na zoezi la uchangiaji damu litakalofanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Damu Salama.
KUMBUKUMBU YA IMAM HUSSEIN
Mohamedraza amesema jina la kambi hiyo limechukuliwa kutoka katika historia ya Imam Hussein (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w), ambaye alifariki katika tukio la Karbala lililotokea mwaka 61 Hijria (A.H).
Amesema tukio la Karbala limeendelea kuwa kumbukumbu muhimu kwa wafuasi wa Ahlulbayt na watu wengine, likisisitiza misingi ya haki, huruma, utu na kujitolea kwa ajili ya wengine.
“Lengo ni kugeuza mafunzo ya Karbala kuwa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya watu, hasa walioko pembezoni,” amesema.
Amesema utoaji wa huduma za afya bila malipo ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na jumuiya hiyo kuhuisha mafunzo na urithi wa Imam Hussein (a.s) kwa vitendo vinavyomnufaisha mwanadamu.
Kwa mujibu wa baadhi ya washiriki wa kambi hiyo katika miaka iliyopita, shughuli hiyo imekuwa zaidi ya utoaji wa huduma za afya, kwa kuwa imekuwa pia sehemu ya kuwakutanisha watu kutoka makundi mbalimbali kwa msingi wa utu, huruma na kusaidiana.
Jumuiya ya Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaat Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa miongoni mwa jamii za Waislamu wa Shia na wafuasi wa Ahlulbayt, imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii kwa kusaidia wagonjwa, wahitaji na makundi yenye uhitaji.
Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, kambi hiyo ni sehemu ya kuendeleza dhamira ya kusaidia jamii kupitia matendo ya huruma na huduma za kibinadamu, huku ikisisitiza kuwa huduma hizo zinapaswa kupatikana kwa heshima na bila ubaguzi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...