tovuti ya jambo forum imerejea hewani kwa kishindo na hii ni mojawapo ya picha zake za mwanzo toka ipigwe loba, ikionesha siku mbunge wa monduli mh. edward lowassa alipowasili jimboni kwake. ukitaka zaidi nenda www.jamboforums.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Wadau Waziri Mkuu wa Zamani ametoa kauli yake kuhusu Richmond, kama nilivyoinukuu kutoka freemedia.co.tz. Kauli yake kwa kweli inaonyesha kwamba kuna mengi yaliyojificha kuhusu Richmond. Tafadhali soma hapo chini na toa maoni yako

    WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema aliponzwa na uaminifu wake dhidi ya watendaji waliokuwa chini yake, wakati wa ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kupitia Kampuni ya Richmond.
    Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wapiga kura wake katika Jimbo la Monduli, mkoani Arusha, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kuachia madaraka ya uwaziri mkuu, hivi karibuni, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya hiyo ya Richmond.

    Alisema hakuhusika kwa namna yoyote katika mchakato mzima ulioipa Richmond ushindi wa zabuni ya kuagiza mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura.

    Badala yake Lowassa alisema waliosimamia mchakato mzima wa kupata Kampuni ya Richmond walikuwa ni wajumbe wa kamati maalumu ya serikali aliowateua yeye ambao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika; Wizara ya Nishati na Madini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

    “Mimi sihusiki kabisa na suala hili, kwani wapo wanaopaswa kubebeshwa mzigo huu - Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha; Mwanasheria Mkuu wa Serikali na BoT…mimi nimewajibika ili kulinda maslahi ya chama changu,” alisema Lowassa.

    Alisema kamwe yeye hana uhusiano na Kampuni ya Richmond na wala hakuchukua hata senti moja kutoka katika kampuni hiyo, bali kilichomponza ni suala la kuwaamini zaidi watendaji waliokuwa chini yake.

    Mbali ya hilo, Lowassa alisema katika hatua fulani mwanzoni kabisa mwa mkataba huo wa Richmond, alifikia uamuzi wa kuuvunja mkataba huo baada ya kuanza kuwapo kwa taarifa za utata wake, uamuzi ambao, hata hivyo, alisema ulikataliwa na wataalamu wa masuala ya nishati na wanasheria serikalini.

    Akitoa mfano, Lowassa alisema katika kikao kimoja cha kutaka kuvunja mkataba wataalamu hao waliomba awape muda wa saa moja kutafakari pendekezo lake hilo, na waliporejea walimweleza wazi kuwa hatua hiyo ingeweza kuigharimu sana serikali.

    Alisema hata alipowaeleza wataalamu hao kwamba alikuwa ana uzoefu wa kuvunja mkataba wa kuboresha miundombinu ya maji kati ya kampuni ya Uingereza ya City Water na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) wakati akiwa Waziri wa Maji na Mifugo, bado wataalamu hao walikataa pendekezo lake hilo.

    Alisema kwamba aliamua kuachia ngazi kwa sababu ya kukubali kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na watendaji walio chini yake. Kwamba kuwajibika kwake si kwa sababu alihusika katika kuipendelea Richmond kupata zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura, wakati nchi ilipokumbwa na uhaba wa nishati hiyo muhimu.

    Lowassa alisema kama Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe, ingempa nafasi ya kujieleza, angetoa mchakato mzima ulivyokwenda na taarifa isingekuwa kama ilivyo sasa hadi kuwafanya baadhi ya watu waamini kuwa alihusika moja kwa moja kwenye kashfa hiyo.

    “Mimi sikuwa mtu wa kukaa ofisini na kupokea taarifa, bali nilikuwa nafuatilia kwa ukaribu na kwa umakini taarifa za watendaji wangu, ambao kuwaamini kwangu ndiko kulikoniponza,” alisema Lowassa.

    Alisema kwa mara ya kwanza aligundua kuwa mambo hayakwenda vizuri kama alivyokuwa akiwaamini watendaji wake baada ya kupata taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza suala hilo.

    “Baada ya kugundua kuna matatizo kwa watendaji wangu katika kulishughulikia suala la Richmond, niliamua kuachia ngazi kwa moyo mweupe bila kushinikizwa…nawaombeni wapiga kura wangu mnielewa hivyo,” alisema Lowassa.

    Alisema wakati wa mchakato huo, mara kadhaa alitumia muda wake kuingilia kati suala hilo alipoona kuna dalili za hujuma ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyokuwa chini ya uongozi wa Kampuni ya Netgroup Solutions kutoka Afrika Kusini.

    Alionya kuwa kujiuzulu kwake kusitumiwe kama kete ya kisiasa kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, bali kutumike kuijenga CCM na kusimama imara dhidi ya hoja zitakazokuwa zikitolewa dhidi yake.

    “Najua mengi yamesemwa na yataendelea kusemwa, lakini cha msingi kwa wana-CCM ni kukaa imara na kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika harakati zake za kuleta maendeleo ya nchi yetu ili kufikia malengo aliyojiwekea,” alisema Lowassa.

    Bila kuingia katika undani wa suala hilo, aliwataka wana-CCM kuwa macho na wale wote wanaofanya kila linalowezekana kukivuruga chama hicho tawala.

    Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Rubeni ole Kunei, alisema wanajivunia kuwa na kiongozi imara kama Lowassa anayekubali kuwajibika kwa makosa ya watendaji walio chini yake.

    Alimtaka Lowassa kutonyong’onyea, kwani kujiuzulu kwake kulitokana na kukubali kubeba dhamana ya uwajibikaji wa pamoja na hatua hiyo iwe mfano kwa viongozi wengine panapotokea matatizo.

    “Sisi wana-Monduli tunaamini kujiuzulu kwako hakutokani na kosa ulilolifanya wewe binafsi, bali kwa kukubali kwako kuwajibika kwa makosa yaliyotendwa na watendaji walio chini yako.”

    Lowassa alipokewa na msafara wa magari zaidi ya 100 na mkutano wake ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa, wafanyabiashara, jamii ya wakulima na wafugaji kutoka wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro.

    Hii ni mara ya kwanza kwa Edward Lowassa kujitokeza hadharani tangu
    alipotangaza kuachia ngazi Februari 7, mwaka huu, mjini Dodoma, kuzungumzia sakata la Richmond, kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura, baada ya kuhusishwa na vitendo vya ufisadi na Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza suala hilo.

    ReplyDelete
  2. Kaka Michuzi, nina swali moja. Hivi hiyo ndege ya kwenye picha ndio tuliokua tukisikia kua ndege ya lowassa imepaa? Kwahiyo hii picha ndio inatuonyesha kua ndege yake imetua kwa sasa? Ebu nipe ufafanuzi.

    ReplyDelete
  3. Kuna watu wengine mazero kweli yani unaona ndege kabisa ya costal airline alafu unauliza ndio ya lowassa jinga kabisa wewe. Bongo ndio private jets hizo watu wanakodisha wenye pesa zao

    ReplyDelete
  4. Wewe annon wa Sunday, February 24, 2008 8:52:00 PM EAT, unamsema annon wa juu yako ni zero kumbe wewe ndio zero zaidi. Soma alichokiandika then ulizia watu ujue huyo annon wa juu yako alikua anamaanisha nini. Usirukie tu kujibu vitu bila ya kujua una jibu nini.

    Kwa kukusaidia tu... Lowassa alishasemaga kua uchumi wa bongo uko katika stage iliyoelezewa na huyo annon wa juu yako.

    ReplyDelete
  5. Mie nimesikiliza hiyo hotuba ya lowasa na kusoma karibia mara nne hivi,,kuna ufisadi umetendeka mkubwa sana,sio kwa yeye lowasa bali kuna wizara nyingine imejionesha hapo kuwa ndio chanzo kikubwa,,kwa upande wangu mie binafsi naona waziri mkuu lowasa hakutendewa haki,kujiuzulu sio kwamba umekula hella,kajiuzulu kama waziri mkuu kwa kosa lililotendeka....kwa upande wangu nampongeza waziri mkuu lowassa kwa kuweza kuwa jasiri na kuachia uwaziri mkuu kwa kosa ambalo hakutenda yeye,hongera waziri...mdau toka Norway

    ReplyDelete
  6. Hivi huyu jamaa anaeitwa gray Mgonja ni jamaa wa wapi??

    maana kila skendo anatajwa "LIVE" lakin jamaa anadunda tu.

    Ningejua anatokea kiji gani ningeenda huko kuwaona wataalam maana mi kuna mambo flani hayaendi poa hapa job, nahitaj kuwaona "WATAALAM" wanitengenezee kama huyu jamaa ili mabos wapige kimya, wasipige kelele

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...