Tunapenda kutumia nafasi hii kuwaomba radhi jamii ya Watanzania wote waliojitokeza kwa mamia yao kwenye sherehe ya "OldSkool Party" mjini Columbus tarehe 5/7/2008.

Hakuna kina cha maneno au upambaji wa hoja unaoweza kuelezea masikitiko yetu kwa kushindwa kufanya siku hiyo kuwa ya kukumbukwa kwa uzuri wake, burudani yake na zaidi ya yote muziki wake mzuri, muziki wa zamani ambao wengi waliutarajia.

Licha ya maandalizi yetu yote tunaweza kukiri kwamba jukumu la kuandaa shughuli hiyo lilizidi mara nyingi sana uwezo wetu kama waandaji na hilo peke yake limekuwa funzo kubwa kwetu.
Funzo la kwamba, tukitaka kuandaa kitu kizuri kwa Watanzania wenzetu hatuna budi kufanya na zaidi ya kufanya maandalizi yetu kuwa ya hali ya juu, bora, na ambayo yanaendana na viwango vya kimataifa.

Tulishindwa katika kuwapatia burudani ya muziki ambao wengi waliutarajia.
Licha ya kwamba nyimbo zenyewe zilikuwa ni zile zilizopendwa miaka "ile" tatizo la uwezo mdogo wa nguvu ya umeme katika jengo tulilofanyia tafrija ilisababisha vyombo vilivyotumika kutumia nguvu nyingi ya umeme na hivyo kusababisha muziki kukatika katika. Hii ilikuwa ni kero ya dhahiri na jambo ambalo liliongeza kero zilizotangulia.

Kuna mengine mengi ambayo tungeweza kuyaeleza na kuwaomba radhi kwayo lakini kwa kifupi ni kuwa kama waandaji tunabeba mzigo wote wa kuwajibika kwa kushindwa kufanikisha kwa kiwango cha kuridhisha na zaidi ya kuridhisha yaani kuzikosha roho zenu pale Columbus siku ile ya Jumamosi.
Funzo tulilolipata ni kubwa, na kwa pamoja na mmoja mmoja tunakubali makosa na mapungufu yote na ni sisi tu wenye kustahili kubeba lawama hizo zote.

Tunawashukuru kwa moyo wenu wa ukarimu na ukaribu, na zaidi ya yote kuchukiliana nasi katika mapungufu hayo.
Tunawashukuru zaidi kwa kuja kwenu na kuweza kujumuika na kukutana na watanzania wengine katika mkusanyiko huu.
Tunawashukuru wale wote waliojaribu kwa namna yao kutengeneza kilichoharibika. Mapungufu ya muziki yaliyojitokeza si kosa la Ma DJ tuliowaalika bali ni makosa ambayo hata wao yalikuwa nje ya uwezo wao, na kwa niaba yao tunawaombeni radhi ninyi nyote.
Tunaahidi kuwa kabla ya kuandaa kitu kingine kama hiki tutakaa chini na kujifunza (take a course) na kuhakikisha kuwa katika uchanga wa shughuli zetu hizi tutaweza muda si mrefu ujao kufanya tafrija ambayo siyo tu itakidhi matarajio ya wageni wetu bali itapita kila njozi yao na kufanya ndoto zao za tafrija zote kutimia. Tunahakikisha tunapata mawazo ya watu wengine waliobobea katika mambo kama haya.

Hilo tunawaahidi na mapungufu ya safari hii tunaomba mtuchukilie kama uchanga wa shughuli hizi kubwa lakini pia msisite kutupa nafasi inayostahili tutakapoweza kuwathibitishia pasipo shaka kuwa tumekomaa kufanya shughuli kama hizi.

Tunatanguliza Shukrani Zetu za dhati kwa uwezo wenu mkubwa wa kuelewa suala hili kwani Kufanya Kosa Sio kosa bali kurudia kosa ndio kosa.
Akhsanteni nyote
Waandaji:
Tina Lupembe,
Phanuel Ligate,
Peter Kirigit,
Lucas Mukami

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 37 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 10, 2008

    Duuh washkaji biashara hamuwezi. Yaani hata mkifungua Funeral Home nobody will die!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 10, 2008

    Nimewasamehe.
    Tumepokea na tunashukuru.
    Next year tutarudi Columbus na tungependa iwe kubwa na nzuri zaidi.
    Hili hall(bwalo) linajulikana kila miaka mnafanyia hapo. Sasa tunataka hoteli au sehemu yenye hadhi ya kuheshimika, maana watu wanaipa JULY 4TH heshima yake hapo OHIO.
    Thanks, kwa kuomba samahani.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 10, 2008

    andaeni party ya kuomba radhi kwa pesa mlizozipata kwa hii mliyochemsha,

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 10, 2008

    IF YOU REALLY REGRET TANGAZA PROFIT ULIYOPATA THEN GIVE IT TO SOME CHARITY
    OTHERWISE KAA KIMYA TAKE YOUR COURSE KAMA ULIVYO-SUGGEST AND OMBA UPATE OTHER FOOLS MUWAIBIE SAWA!

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 10, 2008

    Kitendo mlichofanya cha kuomba msamaha na kuchukua lawama hili ni cha ustaarabu wa hali ya juu sana. Maisha ni fundisho, na tumieni funzo hilo kwa maandalizi ya mbeleni.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 10, 2008

    Alie andika hapa amejaaliwa kwa ufasaha wa lugha. Msamaha umekubalika.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 10, 2008

    kalagabaho!!!!!!!!

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 10, 2008

    Huo kweli ndio uzalendo mimi nawapongeza kwa huo moyo wa kukubali makosa, kitu ambacho wabongo kwa ujumla hata mawaziri wetu kule afrika huwa wanakuwa wabishi kukubali, apology accepted we always learn from our mistake, and no body is perfect good job. Va in tha house represent.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJuly 10, 2008

    angalau wameomba msamaha

    ReplyDelete
  10. AnonymousJuly 10, 2008

    Kaeni chonjo maana Michuzi kalala. Akiamka hizo koments mtazoona, nawaonea huruma. Lakini mimi nakubali apology yenu na naamini imetoka rohoni.

    ReplyDelete
  11. AnonymousJuly 10, 2008

    MMETUBOA .....PERIOD!

    ReplyDelete
  12. AnonymousJuly 10, 2008

    Ndugu waandaaji,
    Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa kwa kuwa na wazo la kutukutanisha watanzania kwa lengo la kusalimiana na kufahamiana.Hilo pekee ni jambo la kupongezwa na kila mstaarabu.Maana mimi binafsi nilipata kukutana na jamaa ambaye tulisoma wote sekondari "O" level miaka ya "80".Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba mkusanyiko ule kimsingi ulituwezesha kukutana na wakongwe wa zamani katika fani mbalimbali,jambo ambalo tulilifurahia sana.

    Sasa mengi yamesemwa na wahudhuriaji juu ya mapungufu yaliyojitokeza.Kimsingi nakubaliana na malalamiko yote kwani hata mimi niliyashuhudia.Mapungufu hayo yameanishwa na wadau mbalimbali,na wandaaji pia mmegusia baadhi hasa suala umeme kuwa mdogo na hivyo kusababisha kukatika katika kwa muziki.Nasikitika kuwa hamjazungumzia sababu zilizopelekea kutowepo kwa nyama choma na mpambano wa soka kati ya Simba ya Yanga.Mimi binafsi nilikuwa nimejiandaa kikamilifu kusakata kabumbu siku hiyo kwa lengo la kurejesha hadhi mtaa wa Msimbazi kufuatia kipigo tulichopewa katika mechi ya awali mjini DC.Nilikuwa nimejifua kwelikweli.Siku ya jumamosi nilijinyima kula na kunywa ili niwe mwepesi ndani ya uwanja na kupeleka majonzi mtaa wa Jangwani.Matokea yake sasa watani wa wajadi wakapata nafasi ya kututania Simba kuwa tumeingia mitini.Sawa hayo yamepita.
    Kilichonisukuma kuchangia leo ni kitendo cha moyo wa ujasiri na uungwana mlichokionesha leo kwa kuomba radhi kwa yaliyotokea.

    Hakika mmeugusa sana moyo wangu kwani binafsi nafurahi sana kama mtu anayaona madhaifu,anayakubali mapungufu,na kisha kuomba radhi.Nimeguswa sana na tabia hiyo ya kiungwana na ya kijasiri sana.Mimi na mke wangu tunapenda kutamka kuwa tumewasamehe kwa moyo wa dhati kabisa hasa kwakuwa pia hamkumun'gunyamung'uya maneno katika waraka wenu wa kuomba radhi.Mmekuwa wawazi sana na mmeweza hata kuanisha mikakati mtakayotumia katika kuboresha matukio mengine mtakayoweza kuyaandaa siku za usoni.Hongereni sana kwa hatua hiyo na wala binafsi nadhani hamjachelewa kuchukua hatua hiyo muhimu katika kuleta suluhu kwa wadau.Na katika hali ya kustaajabisha mmeweza kwenda mbali zaidi hata kuweza kuyaanika majina yenu(naamini ni majina yenu halisi).
    Kwangu mimi hili linanishawishi kuamini kuwa hamjatoa waraka huu kwa unafiki bali kama watu wazima(pengine wengine mna familia)mmedhamiria kwa dhati kukiri mapungufu.
    Napenda niwape pole sana kutokana na maneno makali yaliyotumiwa na baadhi ya wadau katika kuelezea kutofurahishwa kwao na mapungufu yaliyojitokeza.Nadhani jazba ilitawala zaidi na hivyo kupelekea kupoteza subira.Na wala siwalaumu katika hilo.Binadamu tunatofautina katika kukabiliana na masuala mbalimbali.
    Nawashauri wadau wote waliotoa kauli za laana,vitisho,kashfa na kejeli za kila aina,basi kwa waraka huu wa kuomba radhi kwa ndugu zetu waandaaji, tujirudi na kufuta kauli zetu.
    Na kwa wale mtakaoendelea kuwepo hapa Marekani,naomba muendelee kuwapa ushirikiano kwa siku zijazo kwa maana waandaaji wamekiri kuwa kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa.
    Kila la kheri!

    ReplyDelete
  13. AnonymousJuly 10, 2008

    Sasa mnaomba msamaa baada ya watu kuja juu? Pesa zetu je?

    Itakuwa safi kama mkiandaa shughuli nyingine ya bure.

    Na wewe kibiriti sijui kigiriti..whatever your name is umezidi tamaa ya pesa.

    Ni hayo tu kaka michuzi.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJuly 10, 2008

    huo ndio uungwana,mimi binafsi nimewasamehe na nita kuja kuona pary nyingine mtakayo andaa.


    mdau

    ReplyDelete
  15. AnonymousJuly 10, 2008

    Ningekuwa ni mtu nisiyekosea na mwenye haki kuliko ninyi kwa kweli ningewakandia na kuwalaani kuliko wengine waliofanya hivyo tangu sherehe ipite.

    Lakini mmeonesha kitu nadra katika jamii yetu ambapo mara kadhaa waliojuu na wenye makosa hawaombi msamaha na hawataki hata kutambua kuwa wamekosea. Wapo wale ambao hata ubovu wa kazi zao unawakodolea macho na kuwatumbulia kama chura aliyekanyagwa na raizoni lakini bado watabisha.

    Ni kweli shughuli ilienda kombo na ni haki kabisa kwa watu kuwalaumu na kuwasema. Mmekubali makosa yenu na mmeonesha uungwana wa kuomba radhi.

    Laiti viongozi wetu wangejifunza hilo. Hata hivyo binadamu wana kikomo cha kuvumilia, msiwasukume watanzania wenzenu wakakata tamaa nanyi.

    Radhi yenu ni mwanzo wa kuinuka tena kwani kwa Columbus mlianguka. Binafsi licha ya kuchapwa na Parking ticket - natoa msamaha wangu wa dhati, na sina baya ninalowatakia bali mema na fanaka mtakapojaribu tena. Na wakati wowote mkihitaji msaada wangu hata wa wazo moja tu la kufanikisha mnachopanga mimi na jamii nzima ya mashabiki wa klhnews.com na wasikilizaji naamini tutawapa nafasi angalau moja nyingine kututhibitishia kuwa ya colombus ilikuwa ni kuteleza tu na si kuanguka.

    Katika mapambano ya fikra na burudani tele!

    Next time mkiweza kulipa hiki: mgharimie wenyewe nyama choma, au ulabu, au chakula. Just to say "yaliyopita".
    M. M. M.

    ReplyDelete
  16. AnonymousJuly 10, 2008

    hamna lolote....haya mambo kila siku mbona ndo hivyo hivyo.....

    ReplyDelete
  17. AnonymousJuly 10, 2008

    hii bado haitoshi. kwanza kabisa mnatakiwa ku-jiuzuru nyadhifa zenu zote, ili hii kamati iliyo undwa hapa D.C iweze kuwa chunguza kwa undani ,ili kujua huu ufisadi wa kisanii kama kweli ilikuwa bahati mbaya au vipi. Tayali kamati ya watu kumi imeshafika culumbus Ohio ili kuonana na yule Mchina ambaye ndiye mwenye warehouse mliyotuweka. Na nasikia hakuwa na habari zozote za disko, anacho jua ni kwamba kuna watu wanne walikodi warehouse yake tarehe 4 na 5 mwezi wa saba Mwaka huu ili kuweka mizigo yao. bado tuna subiri mambo makubwa zaidi yasemwe.wakati kamati inaendelea na uchunguzi, mnatakiwa kuto kuonakana katika mikusanyiko yote ya Wabongo hapa Washington DC na kwenye state zote.Ili msiigilie uchunguzi. baada ya hapo kamati itawaita pale kwenye kabaa ka Safari ambako mlipanga tena kuwaibia Wabongo. Mtakapo kuja mje na maelezo ya matumizi ya mshiko wetu mliotuibia, na vile vile mje na orodha ya mali zenu zote na jinsi mlivyo zipata. Ndipo kamati itaamua kama kuukubali msamaha wenu au vipi. wakati wowote munaweza kuitwa Safari na Mzee safari ameahidi kuto kunywa ili awe mashahidi sababu kila siku yeye ni Tungi tu.Hahahahahaaaa.

    ReplyDelete
  18. AnonymousJuly 10, 2008

    No NO No ,Hapana , hapana, ngojeeni kwanza kamati iliyotumwa kuongea na Mchina mwanye warehouse itoe taarifa, kwa sasa wana mahojiano na Mchina, please wait-msamaha wenu tuna uweka katika suspension.
    Mudau

    ReplyDelete
  19. AnonymousJuly 10, 2008

    lol! Sishangai sana wabongo hawabadiliki hata mkiwa ugenini.

    ReplyDelete
  20. AnonymousJuly 10, 2008

    Here we go again. It Starts....
    Honestly, i love it when we get posts like this. Yani napenda kweli kusoma mijadala na majibizano. it sure makes my days. Kama nataka kujua news i can always read the papers lakini vitu kama hivi havipo huko! Ok guys, let's roll!

    ReplyDelete
  21. AnonymousJuly 10, 2008

    Tina Lupembe; mimi naomba nichukuwe fursa hii kukuomba wewe binafsi usijihusishe na uandaaji wa matukio. Rekodi zinaonyesha uwezo wako mdogo katika fani hii ya maandalizi. Itakumbukwa kwamba uliharibu kabisa party ya Mr. Nice Chicago Illinois na kutumia usanii huu huu wa kuomba msamaha. Mimi naona unajitia aibu na kama umeishiwa tafuta njia nyingine ya kuishi hapa Marekani na siyo kuibia watanzania wenzio. Binafsi nikiona jina lako kwenye maandalizi yoyote siji. Wajinga ndio waliwao endelea kuwalia fedha za watanzania na utakiona cha moto.

    ReplyDelete
  22. AnonymousJuly 10, 2008

    poleni sana kwa kuibiwa pesa zenu wasameheni hao magubeli wakubwa
    mafisadi wamelaanikwa toka kwenye vizazi vyao huko africa jamani

    sasa subilini watu wa d.c na tume yetu..
    ikimaliza uchunguzi.mwakani mn tunawaleta wanawangwasuma wazee wa pamba

    ReplyDelete
  23. AnonymousJuly 10, 2008

    Hivi nyie Columbus mambo gani ya kuchukua warehouse badala ya sehemu ya maana kama hotel or convention center ...trip nzima nilichofaidi ni hotel yangu na usafiri mzuri wa ndege lakini hapo Columbus ilikuwa ni disaster,hata wenyeji wenyewe mapozi tuu ya kibitozi yasiyo na maana yeyote,next time hire the party planner mumlipe kila kitu mtafanyiwa sio kufanya mambo kiswahili swahili kuchosha watu bila sababu....yaani ukumbi utafikiri manzese na hata AC hakuna na hata security hakuna,next time hire security la sivyo mtaishia jela huo ni mkusanyiko mkubwa anything can happen,fanyeni mambo hata mkicharge zaidi poa tuu na party kama hiyo hope hamfanyi kwa profit.na lazima muweke bartenders mba ni professional sio ubabaishaji tuu ili mpate faid tuu kwa kuuza wenyewe...mmeboa sana!

    ReplyDelete
  24. AnonymousJuly 10, 2008

    hivi kwa nini hizi party zisifanyike sehemu kama holiday in, marriott etc....

    ReplyDelete
  25. AnonymousJuly 10, 2008

    Hee Jirani, wenzio mwanangu yuko Marekani anfanya kazi huko. Mwanangu siyo kama watoto wengine wanaohangaika na kutangatanga na maisha hapa Bongo. Msinionee wivu kwani DJ huko Marekani.

    Mzazi Njombe.

    ReplyDelete
  26. AnonymousJuly 10, 2008

    Jamani eeeh!! week end imekwisha, rudini makazini,wengine hatukwenda Columbus kusikiliza mziki au kumuona Bony, we went there to meet with old school friends and we had fun bigxxxxxxxxxxxxxxxxx time. Go back to work masikini nyinyi, eti mnataka kupigiwa nyingine ya bure you guys are so cheap, ningekuwa mimi next time ningewapigia mchiriku!!!!!!

    ReplyDelete
  27. AnonymousJuly 10, 2008

    Binafsi nilisikitishwa sana na kitendo cha waandaaji kutokuwa makini katika suala la usalama. Walichojali ni pesa tu, suala la kuhakaikisha wabongo wanaokuja kwenye sherehe kufurahi na kucheza kwa usalama halikuwa muhimu kwao. Usiku wa Tarehe tatu, wasudani waliletafujo sana na kusababisha kumpiga kijana mtanzania mwenzetu hadi kuzirai baada ya kuishi disko.
    Wabongo tulikuwa tukiangalia tu.
    Hawa wasudani walianza kuleta vurugu muda watu wapo ukumbini, waandaaji wa shughuli hawakufanya juhudi zozote kuhakikisha wasudani hao wanadhibitiwa. Wakawaacha waingie ndani ukumbini na tulipokuwa tukitoka wakaendeleza vurugu hadi kumpiga na kumuumiza kijana mmoja wa kitanzania.
    Kimsingi suala hilo lilinisikitisha mno.

    Iweje shughuli ya watanzania turuhusu wasudani waiharibu? Ok, walipoanza kuleta vurugu kwa nini hatua hazikuchukuliwa kuwadhibiti ili kuhakikisha usalama kwa watanzania? Watu walikuwa so busy kukusanya mapato, usalama wetu hawakujali kabisa.
    Kuna sababu gani ya kuja kwenye sherehe ambayo unafahamu kuwa ukipatwa na shida ni yako pekee na hakuna wa kukuhakikishia usalama? Kwa nini tuje kujiua?

    Michuzi hii naomba uiwekee mjadala wake. Watu wanazungumzia muziki kukatika tu, je maisha ya wabongo kuwa hatarini hiyo ni sawa?

    ReplyDelete
  28. AnonymousJuly 10, 2008

    Jamani wabongo!! The party was okay, watu walipata nafasi ya kukutana na watu waliowamiss long time. Ask yourself how many friends you met or made?! Party ni watu; na nakwambia wakiandaa nyingine watu wataenda. Old skool songs unaweza kusikiliza kwenye 'youtube' waliokwenda Columbus walienda ku-vacation na kuhave fun, meet wabongo, etc. Kama mziki ulikuwa mbovu mbona watu hawakuondoka mapema?? Watu walikuwa more interested kupiga stori kuliko muziki; and thats always the case kwenye party ya wabongo. Party ni watu!!

    ReplyDelete
  29. AnonymousJuly 11, 2008

    Asante kwa ku come clean.Msamaha umepokelewa

    ReplyDelete
  30. AnonymousJuly 13, 2008

    Wabongo we try weeee but where.... Well lets move on now Party imepita. Fundisho: Next time don't go au andaa yako if you think you can do better.

    ReplyDelete
  31. AnonymousJuly 14, 2008

    Tatizo la hii sio wao ni kuwa kila mbongo siku hizi anafanya biashara hii ya party. Zimekua nyingi na kila mahali. Tuwaige waghana, waseraleone na waganda. Hawafanyi fanyi party uchwara kila siku ...wanafanya party moja au mbili tu kwa mwaka na ukienda kwenye moja ya party zao utaikumbuka na kuisimulia kwa miezi kadhaa....Nimehudhuria hizi za hawa watu basi tena mimi za wabongo si tii mguu. Ni heri nikalipishwe hela lakini nifurahie paty, chakula kizuri, ukumbi mkubwa na hewa ya kutosha, music mzuri...Niliwaonya watu waliokua wanaenda Ohio lakini hawakunisikia....Safari yote toka NY walichopata ni mateso ya hali ya juu......

    TUNATAKIWA TUJIFUNZE NA TUACHE KUWA MAGREEDY.

    Na ni heri ucharge watu so much money lakini huduma iwe nzuri kuliko kuchukua $10 $10 na party za kijinga jinga tu kila siku ....

    ReplyDelete
  32. AnonymousJuly 14, 2008

    Tatizo ni kuwa Watanzania we are so cheap! Niliposikia party ya dola 10 nikasema hiyo itakuwa kwenye GO-DOWN! Huku kuna ma-hall yapo presentable na yana bei nafuu. At least invest money ili upate pesa! Hata kama n i kucharge dola 50, lakini una uhakika wa kufurahi ITS O.K. Hapa D.C. Tunalipa hela kibao kuingia Zanzibar au H2O na upuku puku mwininge wa vi-night club zao. Kaka Lucas wewe uko mjini hapa unajua tunalipa kiasi gani kuijngia disco na wala hukuti miziki tuliyokuwa nayo. Next time please tafuteni hall la maana na mcharge zaidi, disco la dola 10 lilinitisha na ndiyo maana wengi wetu hatukuja. Bonny Love tumesoma wote and nilikuwa sikosi miaka ile Bongo kila week-end, kilichi niput off ni bei!!!

    ReplyDelete
  33. AnonymousJuly 14, 2008

    hebu acheni kulia-lia.Mmeliwa baada ya kupigwa sindano ya ganzi,sasa maumivu hayo yanatoka wapi?next time wataongeza dozi ya ganzi na still utaenda kupasuliwa.then what,utalia tena?hao waandaaji karibu wote wanaeleweka walivyo CHEAP.blah blah kibao utadhani TEJA la kinugu.wengineo hapo wana KASHFA juu ya mambo hayo ya "vijisenti" ktk state zao.
    kama pesa wamepata za kutosha na watajipanga ili kurudi upya soon,tena wanaweza kuja na style ya kumleta celebrity wa kibongo.LET'S wait and c.
    kwa sasa wasamehewe ila next time wakirudia DAWA ni kuwakaba pale pale ukumbini ili warejeshe senti za wadau.
    APOLOGE ACCEPTED!!

    ReplyDelete
  34. AnonymousJuly 15, 2008

    Ukienda bongo, "UFISADI"........ukirudi marekani, "UFISADI". in short ni kwamba kizazi cha waTZ kimelaaniwa, and thats that. SO cha kufanya ni kujikubali tu kuwa sisi ni wafisadi in blood.

    ReplyDelete
  35. AnonymousJuly 16, 2008

    Wabongo acheni kelele nyie mnataka kulipa $10 na kupata service za red carpet mmeyaona wapi. Mkilipishwa hela nyingi mnalalamika watu wezi oh sijuhi nini...$10 is exactly what it worth for what you got and you should be thankful you were even able to see your friends and here some music for that much...kuku nyie acheni kelele...na give these people a break unafikiri wataondoka na kiasi gani wivu tu nyie kila sehemu mnaona ni pa ukulaji.

    ReplyDelete
  36. AnonymousJuly 16, 2008

    Hapo mimi sielewi, kwani mvokosea inamaana OLD SCHOOL PART imegeuka na kuwa NEW SCHOOL part?

    ReplyDelete
  37. AnonymousJuly 16, 2008

    Ndugu Yangu Lucas. Mie Kamal nilikuwepo hapo Ohio na kwa kweli licha ya kuwa mziki ulikuwa unakatika katika, tabasamu ya roho ya kuwaona ndugu zangu na marafiki wengi peke yake lilikuwa ni mantiki ya uwezo wa mtu wa kufikiria. Na kwa kweli umetufikiria.

    Just for the idea I give you all the props brother, let them say what they want and what you couldnt help with, thats how it stayed.

    If the electricity capacity was low, thats not your problem and honestly NO NEED TO APOLOGIZE.

    I had a wonderful time checking out brothers and sisters, thats more than a replacement from music, as a matter of fact the night seemed to be short due to all friends who had gathered.

    This was big and the turn out was also awesome, we got to see oldskool and we laughed all night.

    Thank you for organizing this and I hope you will do this again in the near future..

    As for those who are claiming, you should post your earnings, I would like to ask them earnings from what?? cover charge?? GET OVER IT... IF YOU HAVE NOTHING TO SAY. PLEASE DONT SAY IT IF YOU WERE NOT PRESENT THAT WEEKEND....

    KEEP IT UP AND KUDOS BRO.
    THANK YOU.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...