Huku ni kuwadhalilisha viongozi wa Afrika –JK
Na Mwandishi Maalum, New York, Marekani

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameyaonya mataifa ya Bara la Ulaya kuacha mtindo wa kuwadhalilisha viongozi wa Afrika, kupitia mfumo wa mpya wa utawala wa sheria wa kimataifa unaolenga kuwafungulia mashitaka viongozi wa Afrika, na kuwafikisha katika mahakama za kimataifa.

Rais Kikwete pia amesema kuwa Afrika inaunga mkono, moja kwa moja, mageuzi makubwa katika mfumo wa Umoja wa Mataifa (UN), ili mradi Bara hilo lipewe nafasi mbili zenye kura za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja huo.

Mwenyekiti huyo wa AU pia ameutaka Umoja wa Mataifa kuongoza jitihada za kupunguza makali ya bei ya mafuta na bei ya chakula duniani, kama njia ya kuzilinda nchi changa zaidi, hasa zile za Afrika, dhidi ya makali ya bei hizo.

Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Afrika wakati anahutubia Mkutano wa 63 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo (Jumanne, Septemba 23, 2008) kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani.

Rais Kikwete alikuwa kiongozi wa 12 kuzungumza katika kikao cha mwaka huu cha UN yenye nchi wanachama 192 na alitoa msimamo wa Afrika baada ya ripoti ya utangulizi ya Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki Moon uliofuatiwa na hotuba za Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Rais George W Bush wa Marekani, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, Rais Gloria Macapagal-Arroyo wa Philippines na Sheikh Hamad bin Khalifa Al-Thani wa Qatar.

Wengine waliozungumza kabla ya Mwenyekiti huyo wa AU ni Rais Daniel Ortega Saavedra wa Nicaragua, Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Rais Abdallah Gul wa Uturuki, Rais Cristina Fernandez de Kirchner wa Argentina, Rais Marc Ravalomanana na Rais Boris Tadic wa Jamhuri ya Serbia.

Katika hotuba yake ya kusisimua, iliyotolewa kwa uchangamfu mkubwa na kupokelewa vizuri, Rais Kikwete ameonya kuwa mtindo wa baadhi ya nchi za Ulaya kuwafungulia mashitaka kwa nia ya kuwakamata viongozi wa Afrika na kuwafikisha kortini kwa sababu mbali mbali ni hatua ya kuwadhalilisha viongozi hao.

“Kabla ya kumalizia, ninayo mambo matatu… Jambo la pili ni kuhusu mfumo mpya wa utawala wa kisheria wa kimataifa unaoendeshwa na nchi za Ulaya. Mfumo huu sasa umekuwa na silaha ya kuwadhalilisha viongozi wa Afrika,” amesema Raia Kikwete na kuongeza:

“Tulilijadili suala hilo katika kikao kilichopita cha Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika, na tunakusudia kuliwasilisha jambo hilo kwenye Umoja wa Mataifa, ili lichukuliwe hatua mwafaka.”

Kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete amesema kuwa Afrika inaunga mkono moja kwa moja mageuzi hayo.

Hata hivyo, Rais ameongeza kuwa AU inaamini kuwa mageuzi katika UN hayawezi kuwa yamekamilisha bila kufanya mageuzi katika Baraza la Usalama la UN.

“Kwa upande wa Afrika, tumewaruhusu wawakilishi wetu wa kudumu mjini New York kuanzisha mjadala na pande zote zinazohusika kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama,” amesema Rais Kikwete.

Amesisitiza: “Hapa sasa nataka kusisitiza msimamo wa Afrika wa kuomba nafasi mbili za kudumu na zenye kura ya turufu, na mbili za kudumu bila kura ya turufu kwenye Baraza hilo. Matakwa yetu lazima yatiliwe maanani kwamba ni kweli kuwa Afrika linabakia Bara pekee lisilokuwa na uwakilishi wa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama pamoja na wingi wa nchi wanachama wa UN kutoka Afrika.”

Kuhusu ongezeko la bei za mafuta na chakula duniani, Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa katika wiki za karibuni bei hizo zimeteremka kidogo, lakini bado ziko juu sana.

“Zahama ya bei za mafuta na chakula zikichanganywa na zahama inayokua kila siku katika masoko ya fedha duniani, inatupa kila aina wasiwasi sisi katika Afrika. Hatuwezi kusisitiza kiasi cha kutosha haja ya kusitisha mwelekeo huu. Tunaitaka jumuia ya kimataifa na mataifa makubwa katika uchumi wa dunia kuchukua hatua za haraka kurekebisha jambo hilo. Tunaamini kuwa Umoja wa Mataifa unatakiwa kuongoza mchakati wa hatua dhidi ya zahama hizo.”

Rais pia amezungumzia na kujadili kwa undani hali ya kisiasa na usalama katika Afrika ambako ameelezea jinsi Afrika inavyotatua matatizo yake, hali ya Darfur, hali ya Somalia, hali ya Mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali ya Zimbabwe, mahitaji ya maendeleo ya Afrika, hali ya Sahara Magharibi na mchakato wa Helsinki, ambao uliongozwa na wanachama wenza, Rais Kikwete na Rais wa Finland, Tarja Halonen.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. "Jakaya sema..sema usiogope semaaa...sisi vijana hatuogopi vibaraka semaaa...."

    ReplyDelete
  2. Suala la kuongezeka bei ya mafuta na chakula haliwezi kutatuliwa na UN. Jibu lake ni Supply and Demand. Karibu kwenye ubepari mr. President.

    ReplyDelete
  3. Hapa JK amelitoa bara letu la Afrika Kimasomaso.
    Big up man.

    ReplyDelete
  4. Jk anaposema Bara la Afrika lipewe kura ya turufu ni kucheza makida makida bila kamba.Nchi kama Japan,German na nyingine zenye Viwanda vingi zimeshindwa katika hili jambo(kupewa veto power)unafikiri sisi vinyangarakata tutapewa?
    Sijasoma hotuba yote,hapo ndipo nilipoishia.

    ReplyDelete
  5. Raisi wetu JK kwa yote nakuunga mkono ila hilo la kusema kama viongozi wanadhalilishwa kwa mtazamo wangu ninyie wenyewe viongozi wa afrika ndio mnata kudhallishwa maana mambo mnayofanya mikiwa madarakani sio ya kiubinadamu mmekaa kupendealea 2 ndio kuendeshanchi kama za kwenu hata ulaya ya mashariki wanafunguliwa mashtaka mbona hatuoni south america au asia wakifunguiwa hayo mashtaka hiyoo yote kwa ajili africa hatuna demokrasia ya kweli ndio maana mnadhalilishwa na mtaendelea kudhalilishwa sana mpaka mtapo lta demikrasia ya kweli katika bara letu la africa ndio mtapona.

    ReplyDelete
  6. JK hajasema kitu hapo. Kama kweli viongozi wa africa hawataki kushtakiwa na nchi za ulaya wanapojihusisha na mauji ya wananchi wao kwa makusudi kabisa basi kwanza watawale nchi zao kwa mingi ya kuheshimu haki za binadamu bila kujali rangi wala hali zao kiuchumi au elimu yao. La pili lazima viongozi wa africa waache kuomba omba na wajitahidi kuzalisha katika nchi zao na kufanya biashara baina yao au na nchi ambazo wao wanaziona ni rafiki. kama una muomba omba mtu kitu kila wakati ni lazima na yeye atakutaka ufanye mambo fulani fulani.

    La tatu ni lazima viongozi hao wa africa waachane na kulalamika kuonewa kila wakati ili hali hawafanyi kitu chochote ili kujikwamua, kila siku wanasingizia ukoloni kwa kila tatizo linalotukabili hadi chakula utazani wakoloni wametukataza kulima. Hata USA ilikaliwa na UK na Ufaransa nk lakini huwaskii wakiwalalamikia kila siku, Je unajua hata ubeligiji ilikaliwa na Holland pia? lakini bado wanasonga mbele. Ni vizuri kukumbuka kuwa ni kweli jamaaa walitunyonya lakini je unafanya nini ili usiendelee kunyonywa? Kulalamika UN hakusaidii kama Elibashiri na janjawiti wanaendeleea kuaa wasudani wenzao kisa wana rangi nyeusi!

    ReplyDelete
  7. Kuwafungulia mashtaka kwa ijili ya kuwakamata Viongozi wa Afrika ambao wanakwenda kinyume na uongozi. Hilo si jambo baya wala si udhalilishaji. Watashitakiwa wale tu wanaokwenda kinyume au wanaotumia madaraka yao kinyume na wakiwa na hatia wanahukumiwa. Hilo litafanya viongozi wawe makini sio wafanye wanavyotaka kwa mfano MAFISADI NK.Mhesimiwa raisi asiwalinde hao na asiwatetee hao.
    MCHAMBUAJI

    ReplyDelete
  8. Mwandishi anaonekana kumpongeza J.K, lakini sijui ni nini hasa cha kumpongeza! Labda hilo lakutaka uwakilishi wenye 'veto'.

    Hata waafrika tuliochoka na ufisadi na uonevu wa baadhi ya viongozi wa Kiafrika tunataka wakamatwe na KUSHTAKIWA. Kama hawana makosa si watashida kesi?! Wanaodhalilishwa ni wananchi wa kwawaida ambao baada ya miaka zaidi ya 45 ya uhuru wanakufa kwa 'malaria'.

    J.K acha kubembeleza kupewa misaada na Wazungu wakati tuna raslimali ya kutosha kujitegemea! Nasikia hata kipande cha Serengeti tumewapa hao hao Wazungu. Afrika inahitaji 'free trade' ya kweli ili tushindane katika masoko ya kimataifa, tuuze 'chocolate' na sio 'cocoa'. Hatuhitaji misaada. Huko ndio kudhalilishwa!

    ReplyDelete
  9. Angalia hawa marais chad,uganda,zimbabwe,sudan,angola,burkina faso na mwai kibaki walivyo fanya alafu unasema wanawadhalilisha viongozi wa africa au wenyewe ndio wanatudhalilisha sisi wananchi wa bara la africa wanafanya nchi kama za kwao sawa sawa kufunguliwa mashtaka tu na pili mmezidi corruption za wazi wazi japo kuwa ni tatizo la dunia nzima katika corruption lakini nyinyi mmezidi viongozi wa africa.jiangalie mwenyewe raisi katika serikali yako kwanza mnavyofanya rushwa wazi wazi na unawaangalia kisa marafiki zako ndio maana wazungu walisema kwamba waafrika bado sana kujitawala hiyoo yote nia kwa ajili ya viongozi wachache wa afrika ila mna jumuishwa wote.

    ReplyDelete
  10. Maraisi woote duniani wanauwa, kwa nini wa kiafrica au wa nchi masikini za ulaya ndo washitakiwe peke yao. Au kosa lao ni kutouwa kwa kutumia majasusi.

    ReplyDelete
  11. Simuungi mkono hili jambao la marais kufunguliwa mashitaka wanapoua wananchi wao sasa yeye anataka nini, anataka wafanywe nini? sidhani kama wanafunguliwa mashitaka kwa kuonewa tu, ni kwa vile wamefanya maonevu kwa raia zao, sasa alitaka yule wa Libearia aendele kula kuku tu, najuwa hapa anamtetea swahiba wake wa Sudan, acha hizo, kama hawataki kushitakiwa basi waache kuua watu.hotuba ni mbovu hamna lolote alilosema hapo. ni lazima ashitakiwa akifanya maovu.

    ReplyDelete
  12. TATIZO LA JK NI KUPENDA KUWAKUMBATIA MAFISADI WA KISIASA NA KIUCHUMI NDIYO SABABU INAYOMFANYA KUSHINDWA KUWASHUTUMU WAZIWAZI. YEYE KUONA WANANCHI WANANYANG'ANYWA HAKI ZAO ZA KISIASA NA KIUCHUMI SI TATIZO.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...