JK ashiriki mkutano wa janga la uchumi duniani

Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ni miongoni mwa viongozi sita duniani walioalikwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown jana usiku (Jumatano, Septemba 24, 2008) kujadili zahama ya sasa ya kiuchumi na kifedha, inayoubakili uchumi wa Marekani, uchumi mkubwa zaidi duniani.


Viongozi wengine walioalikwa na Brown kwenye mjadala huo wa chakula cha jioni kwenye Hoteli ya Astoria Waldorf mjini New York, Marekani, ni pamoja na Waziri Mkuu wa Australia, Kevin Rudd.

Viongozi hao wako New York kuhudhuria Kikao cha 63 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) na mkutano juu ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) unaofanyika leo (Alhamisi, Septemba 25, 2008).

Mbali na Rais Kikwete. viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo wa Brown ni Rais wa Brazil, Lula de Silva; Waziri Mkuu wa Hispania, Jose Luis Rodriguez Zapatero; Waziri Mkuu wa Denmark, Anders Fogh Rasmussen na Rais wa Tume ya Ulaya, Jose Manuel Barosso.

Katika mkutano huo, viongozi hao walikubaliana kuwa makosa yamefanyika katika mfumo wa fedha duniani, na kwamba baadhi ya taasisi za kimataifa zilizotakiwa kusimamia makosa hayo yasifanyike, sasa zimekaa kimya.

Viongozi hao pia wamekubaliana kuwa kuna umuhimu wa kutafuta dawa ya haraka ya janga hilo, na pia upo umuhimu wa kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais wa Marekani, George W Bush katika kuthibiti hali isiweze kuwa mbaya zaidi.

Miongoni mwa hatua thabiti zilizokubaliwa kuchukuliwa katika mkutano huo ni pamoja na kuunga mkono hatua za kurekebisha hali hiyo katika Marekani kupitia utaratibu wa RTC, kubuni na kupitisha haraka mfumo wa usimamizi wa masuala ya fedha duniani, na kuweka utaratibu ambao unazilazimisha bodi za wakurugenzi wa mabenki mbali mbali duniani kubeba wajibu mkubwa zaidi.

Hatua nyingine zilizokubaliwa kwenye kikao hicho ni kufanya mageuzi katika mfumo wa utoaji bonasi kwa wakuu wa mashirika ya kimataifa ya kibiashara, na pia kufunua usiri na hivyo kuongeza uwazi katika taratibu zote za kifedha duniani na hasa kuhusu malipo makubwa ya fedha.

Viongozi hao pia walikubaliana kuitisha haraka mkutano wa nchi ambazo zinashililia asilimia kubwa zaidi ya mfumo wa kifedha duniani.

Zahama katika mfumo wa kiuchumi na kifedha katika Marekani unatishia kuvuruga uchumi wa dunia nzima, na viongozi walioko mjini New York kwa ajili ya mikutano ya UN wana wasiwasi kuhusu suala hilo, na hivyo wanataka kuchukua hatua za haraka kuthibiti hali hiyo.

Zahama hiyo katika uchumi wa Marekani imekuwa ikijionyesha kwa namna mbali mbali kukiwamo kuyumba kwa mfumo na soko la nyumba, na kufilisika kwa taasisi za kifedha yakiwamo mabenki.

Utawala wa Rais Bush umekuwa unachukua hatua kadhaa za dharura kupunguza zahama hiyo ikiwa ni pamoja na kuyaokoa baadhi ya mabenki ya nchi hiyo katika janga la kufilisika.

Kwa sasa, Rais Bush amewasilisha katika Bunge la nchi hiyo, mpango wa kutumia dola za Marekani bilioni 700 zaidi kuyaokoa mabenki na mashirika makubwa ya nchi hiyo katika janga la kufilisika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...