Asalaam Aleikhum kaka Michuzi

Sijui nijiite mdau au vipi bali ni mmoja kati wafuatiliaji wazuri wa blog yako, japo sijawi kuchangia lakini nakubali ni mengi nimefaidia kupitia kwako na ndoo maana ata mida hii (about 04:00Am) niko kwenye blog.

kwa leo ninfepenga kurespond utenzi wa mwana kijiji lakini kama Anonymous au H.Q.

Asante na kazi njema

YAKUBALI MATOKEO KUTWANGA HUWEZI TENA

Hodi hodi we balozi, na mzee mwa-kijiji
Nisije kuwa baguzi, kama mpanda Bajaji
Japo mi si mchambuzi, najua mji si jiji
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Mchi ni kama pumzi, zina mwanzo pia mwisho
Haihitaji ujuzi, kulipata suluhisho
Usimtafute mwizi, bure utatokwa jasho
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Hauhitaji mhunzi, wala mchonga vinyago
Watakujaza simanzi, pasi kuona kinyongo
Utawona ni wezi, au wasema uongo
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Kutwanga huwezi tena, yakubali matokeo
Usihisahau jana, ukang'nga'na na leo
Umepitwa na ujana, japo bado una cheo
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Hayakuanzia leo, yalikuwepo awali
Tumia wako upeo, kukabili hii hali
Huitaji pembejeo, wala zile kemikali
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Yaliwakuta wahenga, wewe huwezi hepuka
Usitumie mapanga, kuvifukua vichaka
Muhimu ni kujipanga, uihepuke zihaka
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Kiweke bayana kinu, pia usione soni
Zitumie zako mbinu, usiingie mitini
Ipokee kama tunu, tena ukiwa yakini
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Usipokuwa makini, wajanja watafaidi
Utaingizwa mjini, na hofu itakuzidi
Utapokuja baini, utajiona fisadi
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

Ata ukiwa makini, mchi budi uvunjike
Hakitupwi lawamani, kinu kwa yake makeke
Usijishushe thamani, kwa kushindwa libeneke

Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

10. Naweka kalamu chini, ili nipishe wengine
Wenye mawazo makini, fikira zilizo nene
Wasiotuacha chini, Kwenye giza lilo nene
Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.


Mdau H.Q.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Hii Kiboko. Wabongo mna vipaji kama Obama vile. Du!

    ReplyDelete
  2. Unajua michuzi ushairi ni kama mafumbo au majungu flani hivi. Hapo mtunzi anaongelea mwanaume ambaye jongoo wake ameishiwa nguvu au hawiki tena lakini yeye hataki kukubali matokeo, Pia ushairi huu unaweza kuwa na maana nyingi zaidi ya hiyo niyoieleza.
    Ila mshairi asisahau siku hizi kuna dawa za kuongeza nguvu na ni effective.

    ReplyDelete
  3. Kaka misupu kam sikumalizii nafasi tafadhali kwa heshima yako hebu naomba urudie kuweka hilo origino shairi la mwanakijiji na majibu yake haya mawili kwa mlolongo nisome vizuri man nimevutiwa na majibu lakini shairi lenyee lilinipita tafadhali sana. Sema tuu hongera kwa Wahenga mliochangia jibu sio mchezo kwa kweli mmenikumbusha mbali sana ......

    ReplyDelete
  4. wewe anony wa pili 10:47 hatujakuomba ututafsirie tafadhali , sisi watu wazima and the whole point of mashairi is to leave it to "someones's imagination " mtu atafsiri anavyotaka mwenyewe sasa wewe usituletee maana hapa. Ila kwa kweli wabongo mna bongo jibu yametulia haya ....ingawa shairi silikumbuki kaka Michuzi kam bado unalo litoe tena pls.

    ReplyDelete
  5. Wadau

    Haya mashairi binafsi yananifurahisha sana...hongera H.Q, Mwanakijiji na wengine.

    Duh..Ningeweza kuandika mashairi kama hivi, ningejisikia fahari sana.

    ReplyDelete
  6. Kinu ni letu taifa, mchi ni yake serikali.
    Imepatwa na maafa, au malaria kali
    Inataswira ya kufa, wapo kukejeli.

    Ina taswira ya kifo, kushindwa kuhimili,
    Eti mchi haupo, kwa nyingi dalili,
    mfano eti ni dampo, la ufisadi na dili.

    Jirani Kongo wametoka, Sauzi na Somali
    Jerumani na Amerika, watwanga mali
    Wenyeji walalamika, faida huenda mbali
    Maendeleo ni nafaka, kutwanga na serikali

    maji safi wayataka, elimu na hospitali
    mwananchi nufaika, mazingira wayajali
    maendeleo ni nafaka, itwange zote hali

    ReplyDelete
  7. Michuzi,hapa pa mashairi umenikumbusha mbaaali sana.Akina Mzee Andanenga,Pazi na wengineo.Naomba nimtumie Mzee wa kijiji kama hivi!

    Kuvunjika kwa mpini, Sio mwisho wa kulima.
    Kujifukiza ma-JINI, Pia simwisho wa tiba.
    kuteleza baharini, Si maana yake kifo.
    Kama huwezi kutwanga, Ukimbilie dukani.

    Nafaka kila aina, kila kona madukani.
    Kutwanga huwezi tena, kilio chako cha nini?
    Kama TOROLI hakuna,nenda MADUKA MAWILI.
    Kama huwezi kutwanga,Ulizia madukani.

    Walitwanga zama zile,mababu zetu wa kale.
    Wakatwanga kwa bambile,Duka hazikuwa tele.
    Iweje wewe ulie,Na kupiga mikelele?
    Kama huwezi kutwanga, kanunue madukani.

    Au waishi porini,Na si kule kijijini?
    Nipe jibu la makini, liingie akilini.
    Watwanga nafaka gani?,Zisokuwepo dukani?
    Kama huwezi kutwanga ulizia madukani.

    Unaweza kufa njaa, Kwa kuvunjika kwa mchi?
    Au unashinda baa, ukiuhujumu mchi?
    Usinywe tena chang'aa, Au watwanga chikichi?
    Kama huwezi kutwanga, Ukanunue dukani.

    Kaditamati nafika,We Mzee wa kijiji,
    Jibu linahitajika, Ta kama uko ujiji.
    Usije ukalanika, Na kuanza kunywa uji.
    Huwezi tena kutwanga?Tembelea madukani.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...