Meli ya MV Fatih ikiwa imezama katika eneo la Bandari ya Malindi ndani yake ikiwa na abiria wanaokisiwa kuwa zaidi ya 100. Abiria 27 walikuwa wameokolewa na maiti watatu tu ndio waliopatikana. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam ilikuwa imebeba abiria pamoja na shehena ya mizigo mbalimbali. Picha na mdau Mwajuma Juma - Zanzibar.
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
WATU watatu wamekufa maji na wengine zaidi wanahofiwa kufa katika ajali ya meli ya abiria na Mizigo ya MV Fatih Zanzibar iliyopinduka na kuzama baharini, muda mfupi baada ya kuwasili katika Bandari ya Malindi ikitokea jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Mgharibi Unguja Bw. Bakar Khatib Shaaban, alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea saa 3:00 usiku na tayari baadhi ya maiti zimeanza kuopolewa.
Alisema kwamba meli hiyo ilikuwa na abiria 25 na mabaharia 13 lakini alisema takwimu hizo zinaonekana ni za uongo kwa vile inadaiwa kuwa meli hiyo imebeba watu kupita kiwango chake.
Kamanda huyo alisema kwamba hadi jana mchana maiti za watu watatu tu ndizo zilizoopolewa ikiwemo ya mtoto na mwanamke mmoja na kwamba watu 27 waliokolewa.
Aliwataja baadhi ya watu waliokolewa akiwemo Nahodha wa chombo hicho Ussi Ali, Maulid Abdallah, Zaidba Ali Khatib, Omar Ramadhan Mohammed, Haruna Omar, Kitiba Mussa, Halima Mussa, Hawa Juma Saleh, Sharif Hamad, Omar Khamis na Machano Mkui.
Hata hivyo alisema kuwa watu wengine majina yao bado hayajapatikana lakini walikimbizwa Hospitali matibabu.
Alieleza kuwa chanzo cha tukio hilo bado kinaendelea kufanyiwa uchunguzi lakini wanawasiwasi kwamba meli hiyo ilipinduka, baada ya kuzidiwa na mzigo upande mmoja, kwa vile ilikuwa imebeba shehena za mbao, gari moja trekta na vyakula.
Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Mustafa Aboud Jume alisema kwamba waokoaji 30 wakiwemo wazamiaji kutoka Kikosi cha KMKM walianza zoezi hilo saa 9:00 usiku juzi kwa kushirikiana na wazamiaji mbali mbali.
Hata hivyo alisema kwamba meli hiyo italazimika kujaza upepo ili iweze kuelea juu na kutoa mizigo na watu wanaosadikiwa kuwemo.
“Mashine ya kujaza upepo tunayo, na tunatarajia kujaza upepo ili iweze kuja juu, lakini zoezi hili litategemea na kina cha maji kitakavyokuwa na kama kitapungua italazimika tusubiri hadi usiku”, alisema Mkurugenzi huyo wakati akizungumza na Waziri Kiongozi Bw. Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo Waziri Kiongozi aliutaka uongozi wa Shirika la Bandari kufanya kila linalowezekana meli hiyo iweze kutolewa pamoja na watu wanaodaiwa kuzama katika melihiyo.
“Naomba munipe taarifa kila hatua mtakayokuwa mnafikia na pale mtakapokwama nitafurahi sana kama mtaiarifu Serikali”, alisema Waziri Kiongozi.
Nae Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Shariff Hamad, alisema kuwa watendaji katika Shirika la Bandari wanpaswa kuwajibishwa kwa vile chombo hicho kinajulikana siku nyingi kuwa hakina sifa za kubeba abiria, na hivi karibunikikitokea Pemba kilipotea na kuibukia Tanga wakati kilikuwa kikielekea Unguja.
“Hili jambo ni la kusikitisha sana kwani tangu awali chombo hiki kinajuulikana kuwa hakifai kwa vile hivi karibuni kiliweza kupotelea Tanga na badala yake abiria kulazimika kushushwa katika bandari ya Mkokotoni, naiomba Serikali iwachukulie hatuawahusika”, alisema Maalim Seif.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 31, 2009

    POLENI SANA NDUGU JAMAA NA MARAFIKI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...