JK akiongea na meneja mkuu wa Shelys Pharmaceuticals, Ashok Gupta, baada ya kumkabidhi kombe la ushindi tuzo ya uzalishaji bora wa mwaka jumla nchini wa chama cha wenye viwanda (CTI) usiku huu katika hafla iliyofanyika hoteli ya Movenpick jijini Dar
JK akipozi na washindi pamoja na mwenyekiti wa CTI aliyemaliza muda wake Mh. Reginald Mengi na Mwenyekiti mpya wa CTI Mh. Mosha
JK akippozi na wafanyakazi wa makao makuu ya CTI

JK akiwa na watendaji wakuu wa CTI

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MHE JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE UFUNGUZI WA HAFLA
YA UTOAJI TUZO KWA WAZALISHAJI BORA WA VIWANDANI
WA MWAKA 2009 TAREHE 06 AGOSTI, 2009
MÖVENPICK ROYAL PALM HOTEL,
DAR ES SALAAM


Ndugu Felix Mosha, Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda, Tanzania;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi;
Mhe. William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Makatibu Wakuu mliopo jioni hii;
Wajumbe wa Baraza la Utawala la Shirikisho la Viwanda;
Wanachama wa Shirikisho;
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana:

Awali ya yote, napenda kukushukuru kwa dhati wewe, Ndugu Felix Mosha, Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda, kwa kunipa fursa nyingine tena ya kujumuika nanyi katika hafla hii ya kuwapongeza washindi wa Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora Viwandani.

Niruhusu Ndugu Mwenyekiti, nikupongeze sana, kwa kuchaguliwa kwako kuwa mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Viwanda Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili ijayo. Wenzako wamekupa heshima kubwa ambayo naamini unaistahili. Uzoefu wako wa uongozi katika sekta binafsi na uzoefu wako wa kufanya kazi katika taasisi za kimataifa na hapa nyumbani unanipa matumaini makubwa kwamba utaliongoza shirikisho hili kwa mafanikio makubwa. Napenda kukuhakikishia ushirikiano wangu na wa wenzagu Serikalini, pale utakapoona kuwa tunaweza kuwa wa msaada, katika kutekeleza majukumu yako mapya.

Kwa nafasi yangu ya Mlezi wa Shirikisho hili, nakuahidi kuwa karibu nawe katika kufanikisha malengo ya Shirikisho. Wakati wowote utakaponihitaji niite, nitakuitika.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wana-CTI;
Niruhusuni pia nimpongeze Mwenyekiti aliyepita, Ndugu Reginald Mengi kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uongozi wa Shirikisho. Alilitumikia Shirikisho hili kwa bidii, juhudi na maarifa. Ni matumaini yangu kwamba ataendelea kutumia hazina ya uzoefu wake kwenye Shirikisho kuusaidia uongozi mpya katika kutimiza majukumu yao.
Msukosuko wa Uchumi Duniani
Ndugu Mwenyekiti;
Tunakutana tena mwaka huu wakati dunia ikipita katika kipindi kigumu sana kiuchumi. Kama mnavyofahamu, msukosuko mkubwa wa kifedha na uchumi duniani ulioanza kuuma katikati ya mwaka 2008 bado tunao na hakuna dalili za kuisha hivi karibuni. Sote tunatambua jinsi msukosuko huu ulivyoathiri na unavyoendelea kuathiri uchumi wa mataifa, makampuni, wajasiriamali na watu mmoja mmoja takriban katika mataifa yote duniani.

Hakuna haja ya kuchukua muda wenu mwingi kufafanua athari zake kwani nyote mnajua jinsi viwanda na makampuni makubwa kwa madogo yalivyoathirika au hata kuanguka kabisa. Mnatambua watu walivyopoteza ajira zao. Mnawajua watu waliokuwa matajiri ambao sasa ni maskini. Mnatambua ugumu wa kupata mikopo kutoka katika mabenki na kwamba hata pale benki inapokuwa tayari kukukopesha masharti ya kulipa ni magumu na gharama ni kubwa. Ninyi mnatambua ugumu wa kupata masoko kwa bidhaa za kilimo na za viwandani pia. Aidha, mnajua kuwa hata kwa hizo bidhaa kidogo zipatapo soko bei huwa ndogo na kusababisha hasara kwa wazalishaji au wauzaji. Katika jumla ya yote msukosuko wa uchumi umesababisha uchumi wa nchi nyingi duniani kudorora au hata kusinyaa (shrink). Kwa ajili hiyo malengo ya ukuaji wa uchumi katika nchi nyingine duniani yamekuwa chini ya matarajio.

Ndugu Mwenyekiti;
Hali hiyo ya jumla niliyoieleza kwa uchumi wa dunia inaelezea kwa ufasaha hali iliyotukuta hapa nchini. Na sisi tumeathirika kutokana na msukukosuko wa uchumi wa dunia. Sina haja ya kueleza kwa kina jinsi tulivyoathirika kwani ninyi mliopo hapa mnaelewa vizuri zaidi hata kuliko mie.

Kwa sababu na sisi tumeathirika ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua za kujaribu kukabiliana na athari zake. Kama nilivyoeleza tarehe 10 Juni, 2009 pale Dodoma wakati wa kutangaza hatua za kunusuru uchumi kuwa nilikuwa nimeunda Kamati ya Ushauri chini ya uongozi wa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu. Kamati hiyo ilikuwa na kazi ya uchambuzi wa hali ilivyo duniani na nchini na kupendekeza juu ya nini tufanye kujihami na kunusuru uchumi wa nchi yetu. Tuliyajadili kwa kina mapendekezo ya Kamati hiyo na kukubaliana juu ya hatua za kuchukua. Hatua hizo tumeanza kuzichukua na tunaendelea.

Ndugu Mwenyekiti;
Napenda kurudia niliyosema siku ile kuwa, mpango huu ni wa muda mfupi, wa miaka miwili, ambao lengo lake kuu ni kusaidia zile sekta ambazo zimeathirika zaidi na hasa zile ambazo kama zisiposaidiwa madhara yake kwa uchumi wa nchi yetu yangekuwa makubwa. Miongoni mwa mambo matatu ya msingi ambayo tumekusudia kufanya katika mpango huu ni:-

a. Kusaidia kuyalipia madeni makampuni yaliyopata hasara kutokana na msukosuko wa uchumi hususan makampuni yanayonunua mazao ya kilimo na kuuza nje;
b. Kusaidia Benki zilizokopesha makampuni ambayo yanashindwa kulipa madeni yao kwa sababu ya machafuko ya uchumi wa dunia. Serikali iliamua kudhamini mikopo kwa miaka miwili ili kuyapa makampuni fursa ya kupumua na kujijenga; na
c. Kuyawezesha mabenki kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa Serikali kutenga fedha za kuzipa benki hizo kwa sharti kwamba benki zitachangia.

Ndugu Mwenyekiti;
Nafahamu pia kwamba huenda zipo sekta nyingine ambazo zimeathirika lakini wakati wa tathmini ya awali matatizo yao yalikuwa hayajajitokeza. Tuko tayari kupima athari zake na kuangalia kitu gani tunaweza kufanya kusaidia.

Lakini, muhimu ambalo napenda kuwaomba mtambue ni kwamba sisi ni Serikali ya nchi maskini kwa hiyo uwezo wetu wa kusaidia si mkubwa. Kwa kweli ni mdogo sana.
Tumejibana sana mpaka kutenga shilingi bilioni 1.7. Hatuna uwezo wa kumsaidia kila mtu au kila kampuni itakayoathirika kwa kila kitu. Hii ina maana kwamba tuwe wabunifu na kujitengenezea mikakati na mbinu za kukabiliana na hali hii hata bila ya msaada wa Serikali. Huu si wakati wa kawaida, hivyo tusifanye mambo kama tulivyozoea.
Waingereza wana msemo usemao kwamba “hata kwenye wingu jeusi kuna ukanda wa fedha”. Hivyo hivyo katika machafuko haya yaliyoukumba uchumi wa dunia bila ya shaka zipo fursa ambazo mtu akizibaini na kuzitumia anaweza kuibuka tajiri mkubwa wakati wengine wanafilisika. Je, fursa hizo ni zipi na zitumike vipi, ndiyo changamoto ambayo nawaachia nyie mabingwa muitafiti na kuifanyia kazi.

KILIMO KWANZA
Ndugu Mwenyekiti;
Hivi majuzi nilizindua Azimio la Kilimo Kwanza ambalo bahati nzuri wewe na baadhi ya wanachama wa Chama chenu mlishiriki kwa ukamilifu katika matayarisho yake. Kama mjuavyo shabaha ya azimio lile ni kuongeza chachu katika kuleta mageuzi katika kilimo chetu ili tija iongezeke, mavuno yaongezeke na mapato ya wakulima nayo yaongezeke.

Katika Azimio la Kilimo Kwanza, mambo ya kufanya kuongeza tija katika kilimo yametambuliwa na kuainishwa vizuri. Hapakufanyika uvumbuzi wa jambo jipya la ajabu. Yaliyoainishwa kuwa mambo ya msingi ni mambo tunayoyajua sote, mambo ambayo tunayafanya au kuyazungumza kila siku lakini hatujafanya vya kutosha au kwa namna ambayo yakaleta mabadiliko tunayoyatarajia. Azimio la Kilimo Kwanza lina nia ya kuleta msukumo mpya ili sasa iwezekane kufika pale tunapopataka kwa kuwezesha yale mambo ya msingi kufanyika.

Nilieleza siku ile ya uzinduzi wa Azimio la Kilimo Kwanza pale Dodoma kwamba mageuzi katika kilimo chetu yamechelewa sana kwa sababu ya kuachwa mikononi mwa wakulima wadogo ambao hawana raslimali wala ujuzi, maarifa au elimu ya kutosha ya kupokea na kufanya mageuzi tunayatarajia. Matokeo yake sehemu kubwa ya kilimo chetu ni cha kujikimu tu, tija ndogo, ziada ni ndogo mno (sawasawa na hakuna) na wakulima wenyewe wamebaki kuwa maskini wanaoishi maisha duni. Serikali imekuwa inafanya juhudi kubwa kwa miaka mingi tangu uhuru na mafanikio ya kutia moyo yamekuwa yanapatikana na kuonekana lakini bado ufanisi siyo mkubwa.

Azimio la Kilimo Kwanza ni juhudi mpya zinazojumuisha Serikali na sekta binafsi katika kulisukuma mbele, kwa kasi zaidi kwa nguvu zaidi na kutumia maarifa mapya na mwamko mpya, gurudumu la mageuzi ya kilimo nchini. Sasa tunataka kuhusisha sekta binafsi kwa karibu zaidi na kwa nguvu zaidi. Huko nyuma sekta binafsi haikuhusishwa na kushirikishwa vya kutosha. Isitoshe, baada ya Azimio la Arusha, ilienguliwa, mashamba makubwa yalitaifishwa na waliondolewa katika ununuzi wa mazao na badala yake kazi hiyo ilifanywa na mamlaka za mazao au mashirika ya umma.

Baada ya mageuzi ya kisera yaliyoanza katika Awamu ya Pili, na kuruhusu uchumi wa soko badala ya ule wa dola, milango ilifunguliwa kwa sekta binafsi kushiriki katika kilimo. Lakini bado ushiriki wake ni mdogo mpaka sasa. Katika Azimio la Kilimo Kwanza tunataka wenzetu wa sekta binafsi washiriki zaidi. Walime mashamba makubwa wao wenyewe lakini pia wawajumuishe wakulima wadogo katika kilimo chao kama wafanyavyo wenye viwanda vya maziwa. Wakifanya hivyo, itasaidia kuboresha kilimo cha wakulima wadogo. Wanunue mazao ya wakulima, yaani wawapatie soko la uhakika, lakini pia, wawape bei nzuri kwa mazao yao. Wasiwalalie kama wafanyavyo baadhi ya wafanyabiashara wanaonunua mazao hivi sasa.
Aidha, tunawategemea waanzishe viwanda vitakavyotengeneza bidhaa zinazohitaji kuendeleza kilimo na viwanda vitakavyotumia malighafi kutokana na mazao ya kilimo. Vile vile, wataanzisha asasi za fedha zitakazotoa mikopo kwa wakulima.

Mimi na wenzangu katika Serikali tumefurahia sana mwelekeo huu mpya, na kilichonifurahisha zaidi ni ukweli kwamba wafanyabiashara mmekuwa mstari wa mbele katika kubuni azimio hili . Nawaomba wafanyabiashara na wenye viwanda mjitokeze kwa wingi tena kwa nguvu kushiriki katika utekelezaji wake kama ilivyo matumaini ya Kilimo Kwanza. Nilisema kwamba kutokushiriki kwenu ndiyo goroli pekee iliyokuwa inakosekana katika gurudumu letu la mageuzi ya kilimo. Sasa goroli hiyo imeshapatiwa mahali pake stahiki naamini kasi ya gurudumu letu kuzunguka itaongezeka na kuwa ya hakika zaidi. Sasa mageuzi ya kilimo yatawezekana. Haya Shime jitokezeni. Nawahakikishia ushirikiano wangu na wenzangu wote Serikalini.

Soko Huria la Afrika Mashariki
Ndugu Wanashirikisho;
Kuanzia Januari 1, 2010, Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utatekelezwa kwa ukamilifu. Kuanzia siku hiyo, bidhaa za Kenya ambazo, kwa miaka 5 mfululizo, zilikuwa zinauzwa katika nchi yetu na Uganda kwa kulipiwa ushuru, zitakuwa nazo hazilipiwi ushuru. Aidha, kama mazungumzo yatakamilika kama tunavyotarajia, wakati huo Soko la Pamoja la Afrika Mashariki litakuwa linaanza. Ni wakati wa mabadiliko makubwa kwa mfumo wa biashara hapa kwetu hivyo ni vyema tujiandae vizuri kuyapokea na kuyatumia kwa manufaa yetu. Hivyo nawaomba mkae chini, muitafakari na mpange mikakati na mbinu za kuishi na kunufaika katika mazingira, hayo mapya.

Kubwa zaidi ninalowaomba mimi ni ninyi kujipanga vizuri kuzalisha bidhaa kwa gharama ndogo lakini zenye ubora wa hali ya juu. Yapo ya Serikali katika kuwasaidia kufanya hivyo ambayo napenda kuwaahidi kuwa tutafanya kila tuwezalo kutoa mchango wetu stahiki. Lakini, kwa yale mengi mbayo ni yenu, na ni mambo ambayo yapo kwenye uwezo wenu kufanya nawaomba mfanye bila ajizi.

Napenda kuwatahadharisha kuwa, epukeni tabia ya kutojiamini, woga na kujidharau wenyewe kuwa hamuwezi. Tabia hii ndiyo adui yetu mkubwa kuliko wote hapa Tanzania. Pale mwanzoni tulipoanza mchakato wa kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki hofu kubwa ilikuwa Tanzania kugeuka kuwa soko. Baadhi ya watu waliiamini dhana hiyo kiasi cha kutufanya baadhi yetu tuliokuwa tunaongoza harakati za kuunda Jumuiya tuonekane wasaliti. Lakini ukweli sasa unawasuta. Leo hii biashara kati ya Tanzania na Kenya imekua sana, tena sasa sisi tunauza zaidi Kenya kuliko Kenya inavyouza Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania, mwaka 2008 Tanzania iliuza Kenya bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 277,820, wakati Kenya iliuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 233,967. Zamani hali haikuwa hivi. Biashara ilikuwa ndogo na Tanzania tulikuwa tunanunua zaidi kutoka Kenya kuliko tunavyouza. Haya yote yametokana na kufunguliwa kwa milango kulikotokana na Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naamini hata Soko la Pamoja likija tutaendelea kunufaika, bora tu tupange mikakati yetu vizuri na tuhakikishe kuwa tunaitekeleza. Naamini tutaweza. Kama tumefikia hapa bila ya shaka tunaweza kufanya vizuri zaidi.

Ofisi za Shirikisho
Ndugu Mwenyekiti;
Ninayo faraja kusema kwamba nimetimiza ahadi niliyoitoa katika hafla kama hii mwaka 2006, ahadi ya kuwapa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Shirikisho zenye hadhi ya Shirikisho lenyewe. Nafurahi kwamba tumeweza kupata kiwanja kizuri katikati kabisa ya Jiji. La muhimu sasa ni kuhakikisha kuwa mnajenga jengo hilo bila kuchelewa. Nisingependa kuona miaka inapita bila kazi za ujenzi wa jengo kuanza huku kiwanja kikiwa kimezungushiwa mabati tu. Nawakumbusha masharti ya kupewa kiwanja hicho - ujenzi wa jengo kubwa la kisasa lenye urefu usiopungua ghorofa ishirini!

Taasisi za Udhibiti
Ndugu Mwenyekiti;
Nimesikia ombi lenu la kuitaka serikali iangalie mfumo mzima wa taasisi za udhibiti (regulatory agencies) kwa madhumuni ya kuondoa urasimu, mwingiliano wa majukumu na kuwepo tozo mbalimbali na kubwa ili kuvipunguzia gharama viwanda. Hisia zenu kuwa taasisi nyingine zina matumizi makubwa sana tutazifanyia kazi. Tutaangalia wenzetu katika nchi nyingine wanaendeshaje taasisi kama hizi ili nasi tufanye marekebisho pale panapostahili.

Fursa ya Kushauriana
Ndugu Mwenyekiti;
Nimelisikia pia ombi lenu la kutaka kuonana nami na kupata muda mrefu wa kushauriana nje ya hafla kama hii. Utaratibu wa kukutana nanyi ili kubadilishana mawazo na kushauriana ni mzuri, hivyo napenda kukuhakikishia kwamba kadri muda utakavyoruhusu, nitajitahidi kukutana na wawakilishi wa Shirikisho.

Tuzo za Rais 2009
Ndugu Mwenyekiti;
Kilichotuleta hapa jioni hii ya leo ni kuwatambua na kuwatunukia tuzo wenye viwanda vilivyofanya vizuri kwa mwaka 2009. Kama nilivyosema mwaka jana, mashindano ya uzalishaji bora viwandani ni kichocheo muhimu cha kuongeza tija viwandani na kuzalisha bidhaa bora ambazo zitaweza kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi na kuhimili ushindani.

Nawapongeza washindi wote wa mwaka huu. Msibweteke na ushindi, endeleeni kuimarisha tija, uzalishaji na ubora wa bidhaa. Wale ambao hawakufanikiwa mwaka huu, watambue tu kwamba haya siyo mashindano ya mwisho, fursa ipo tena mwakani. Msikate tamaa, anzeni maandalizi sasa ya kushinda mwakani.

Hitimisho

Ndugu Mwenyekiti, WanaShirikisho;
Nawashukuru tena kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika hafla hii. Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa maendeleo ya nchi yetu, tena wakati mwingine katika mazingira magumu ya upungufu wa miundombinu muhimu. Serikali itaendelea kuweka jitihada katika kuimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini. Napenda kuwahakikishia ushirikiano wangu. Mlango wangu upo wazi wakati wote, sio tu kama mlezi wa Shirikisho bali kama mtu anayependa sekta ya viwanda ikue ili uchumi wa nchi uzidi kukua na Tanzania iondokane na umaskini mapema iwezekanavyo.

Asanteni sana kwa kunisikiliza!



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Nilifikiri JK angekuwa kwenye shamra==shamra za 88 kwanza...kwa sababu hii ni wiki ya nane nane? Michu mdogo wangu naomba kutoa hoja

    ReplyDelete
  2. Wapi kina Subash Patel, yeye ni mzalishaji mkuu wa chuma hapa Tanzania,

    ReplyDelete
  3. Jibu kwa anony wa kwanza,JK amefungua maonyesho ya 88 tayari, au unataka akae huko huko katika maonyesho kila siku mpaka yaishe kama mkata ticket.kabla huujaandika update information zako.

    ReplyDelete
  4. Hii picha inaonyesha taswira tofauti na ile ya madawati ya Vodacom kwa shule za msingi kwanza ndani ya jiji la Dar es Salaam ambako kuna taasisi karibu zote nyeti za serikali. Hapa watu wamepiga suit wanapongezana kwa kupeana vikombe huku kwa upande ule watoto wa shule wanasoma wakiwa wamekaa chini.

    Hivi viongozi wa TZ kweli hamna aibu. Viongozi punguzeni idadi ya suit angalua mnunue madawati kadhaa. Viongozi wa TZ mnafanya nini jamani???

    Angalia Rwanda walikuwa wanapigana vita wenyewe hivi karibuni lakini wameshaanza kutaacha kwa mbali. Jamani Bongo kuna nini hapa??????????.

    Embu tuache blaa blaa jamani. Miaka 48 ya uhuru lakini bado watoto wanasoma wakiwa wamekaa chini.

    Msituambie serikali haina hela, hela zipo nyingi tu, tatizo matumizi mabaya, blaa blaa, na ubinafsi umezidi.

    Hivi viongozi mnapo kwenda kutembea nchi za watu wengine hamjifunzi wao walivyoendelea????. Maendeleo ya nchi yanaletwa na viongozi wa nchi husika kwani viongozi wana madaraka ya kupanga sera na kutekeleza. Hapa kikubwa zaidi ni kuhakikisha serikali inakusanya kodi sawa sawa, ambacho tayari kwa kiasi kikubwa kinafanyika sasa, na hela inayopatikana inatumika vizuri na sio kutumiwa na watu wachache kama ilivyo kwa EPA, Richmond,majengo tata ya BOT, ufisadi mali asili n.k.

    Tuamke sasa jamani tufanya mambo kwa umakini tuendeleze nchi yetu.

    Kwani nchi yetu ikiwa kama chini za Ulaya, USA, Singapo na nyingine zilizoendelea kutakuwa na shida gani?? Hakuna shida, ila kila mtu atafaidi matunda,barabara nzuri, shule nzuri, huduma za matibabu, maji, nishati zitakuwa mzuri na kila mwananchi atafaidi.

    Mungu ibariki Tanzania yetu, ishalla, siku moja tutapata kiongozi ambaye atatusaidia kuleta maendeleo ya kweli. Sio hawa wa sasa wa kuchukua chako mapema.

    ReplyDelete
  5. JK why standing near that man kushoto kwako aghhhh

    ReplyDelete
  6. Anony wa hapo chini ndio tulitaka akae huko huko ili kuleta msisitizo katika slogan yao ya kilimo kwanza au hata angeenda mikoa mingine kwenye maonesho ya nanenane kama Arusha, Mwanza, Morogoro, mbeya na kwingineko...

    ReplyDelete
  7. Alifaa apewe mengi.

    ReplyDelete
  8. Namuona mr.mahenda close to jk huyu jamaa tulikuwa tunaimba naye kwaya pale catholic chang'ombe, ni mtu mzuri anayempenda mungu katika kulitangaza jina la mungu kwa njia ya utume wa uimbaji!!! keep it up Africanus!!! we miss you alot parish of chang'mbe!!!!!!!!

    ReplyDelete
  9. Blah blah blah tuuuuuuuuuuuuu hiiii....hakuna kipya hapa
    Michu mdogo wangu naomba kuwasilisha, Mtoa Hoja (MH)

    ReplyDelete
  10. Chichia chichia JK. Michu mdogo wangu naomba kutoa hoja MH

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...