SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA UUZAJI WA MAGOGO NJE YA NCHI.
Na Aron Msigwa – MAELEZO.

Serikali imewataka wafanyabishara wa mazao ya misitu kuwekeza hapa nchini kwa kujenga viwanda vitakavyosaidia kukuza ajira na kuongeza pato la taifa badala ya kukimbilia kuuza mazao ya misitu hususan magogo nje ya nchi kinyume cha sheria.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Felician Kilahama wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya usafirishaji wa magogo nje ya nchi.

Dkt. Kilahama amesema sheria Misitu ya Tanzania Namba 14 ya mwaka 2002 ambayo ilianza kutumika rasmi Julai 2004 inazuia na kupiga marufuku uuzaji na biashara ya aina yoyote ya magogo nje ya nchi.

“Sheria yetu ya mwaka 2002 iliyoanza kutumika Julai 2004 hairuhusu kwa namna yoyote kufanyika kwa biashara ya magogo nje ya nci na anayeuza magogo na rasilimali za misitu nje ya nchi ni mwizi, rasilimali ya misitu imehifadhiwa kisheria na ipo kwa ajili ya watanzania” Amesema.

Ameongeza kuwa kuna haja ya watanzania kuwekeza hapahapa nchini na serikali iko tayari kuwasaidia na hivyo kukuza pato la taifa na kuongeza thamani ya mazao yetu ya misitu badala ya kukimbilia kuuza nje ya nchi.

“Tunataka wasafirishe vifaa vilivyokamilika na sio magogo ili misitu yetu iwe na manufaa kwetu na kwa vizazi vijavyo” amesisitiza. Ameendelea kufafanua kuwa vitu vyote vinavyotokana na mazao ya misitu vinavyotakiwa kwenda nje ya nchi au hapa nchini kwa mfumo wa biashara ni lazima vifuate sheria na kanuni za nchi na kuongeza kuwa inaweza kuruhusiwa tu iwapo sheria zinazosimamia misitu zitabadilika.

‘Hatuzuii magogo kutoka Tanga kwenda Morogoro bali tunazuia wale wasiolipia ushuru na kukiuka masharti na leseni za biashara” Aliendelea kufafanua Dkt. Kilahama.

Akitoa taarifa za baadhi ya matukio ya uharibifu wa misitu hapa nchini Dkt. Kilahama amesema bado kuna wananchi ambao wanaendelea kufanya biashara ya magogo kinyume cha sheria akiitaja baadhi ya mikoa hapa nchini kama Rukwa, Kigoma ,Ruvuma, Tabora na Pwani kuwa wananchi walio wengi hawana uelewa wa kutosha wa utunzaji wa misitu.

Hata hivyo amesema serikali iko makini kuendelea kufuatilia maeneo yote ya nchi yakiwemo maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kuwa inadhibiti biashara haramu ya magogo na kuongeza kuwa hatua za makusudi zinaendelea kuchukuliwa akitoa mfano wa magogo 1500 yaliyokamatwa Rufiji mwaka huu 2009.

Kuhusu hali ya utunzaji wa misitu nchini amesema kuwa bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa Watanzania kuhusu utunzaji wa misitu akiyataja maeneo mengi ya nchi kuwa yanakabiliwa na tatizo la uhifadhi wa misitu.

Pia amezitaja changamoto mbalimbali zinazokwamisha usimamizi thabiti na utoaji elimu kuuhusu uhifadhi wa misitu zikiwemo uhaba wa watumishi ambao dhima yao kuu ni kuhakikisha kuwa eneo la Tanzania lenye takribani hekta milioni 13 ya misitu iliyohifadhiwa linakuwa salama.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa serikali inakabiliana na tatizo la walinzi hususani katika maeneo ya hifadhi za misitu serikali itaanzisha walinzi misitu ambapo mchakato unaendela kwa mwaka huu ili kuwapata walinzi 106 ambao watakuwa wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Elvis Kabagire (Austria)August 11, 2009

    Hii inafurahisha sana!

    Kidogokidogo watanzania mnaanza kuelewa matatizo yetu.

    Namuomba Dr shayo aiweke hadharani ule utafiti aliofanya wa uwiano wa uuzaji wa magogo south africa na China ambayo niliikuta hiyo report switzerland katika ofisi moja inaojishughulisha na utoaji wa misaada ya maendeleo.


    Nafikiri Dr Kilahama atanufaika sana na uelewa wa tafiti kama hizi ambazo mara nyingi tunakuwa hatupati nakala zake hapa nyumbani.


    Pia, tungemuomba Dr Kilahama atupatie msimamo wa serikali kuhusu magogo ya teak ya kule Tanga. Utafiti unaonyesha kuwa kulikuwepo na kutokuelewana ambako afisa fulani wa serikali ya Finland alipoteza kibarua.

    Msisahau, Dr shayo alikuwa miongoni mwa wataalamu waliokuja kuishauri tanzania ni kwa jinsi gani wanaweza kukabiliana na huu uuzaji wa kiholela wa magogo kwa njia ambazo hazitoi marudufu kwa serikali. Niligundua undani wa mchango wake nilipokutana naye pale Kilwa Masoko akiwa na wenzake wawili ambao wamekuwa wakiishauri serikali ya cameroon ambako tatizo la uuzaji wa magogo nje ya nchi ni kubwa.

    ReplyDelete
  2. Sawa kabisa lazima. Tuamke, kwani wanatucheka.Mataifa yaliyoendelea kwa kuariabu misitu, ni sawa na kuharibu mazingira, kwani misitu inafaida nyingi kwa mazingira na maisha ya mwanadamu,hii tabia ya kukatakata mitii ovyo inasababisha jagwa na isitoshe kama habari ilivyoandikwa hapo juu.Visafirishwe vifaa, sio magogo,kwani wanaenda wanatengeneza alafu wanaturudishia sisi, vifaa tena kwa bei ya juu, kuliko tulivyouza hayo magogo. kisa nchi za ulimwengu wa tatu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...