'JUISI YA MUWA GHALI'
Bahati niliipata, Unguja hatembelea,
Hajionea sakata, sepatapo kablia,
Muwa tabu waipata, wanywaji kuwaridhia,
Juisi ya muwa ghali, si tunavyofikiria.
Muwa wao huushika, mezani ‘kautandaza,
Huanza kwa kuukosha, muwa upate pendeza,
Kisha maji hukaushwa, tayari kutumikizwa,
,Juisi ya muwa ghali, si kama tunavyodhani.
Kisu hwisha andaliwa, kupara miwa kuanza,
Kwa makali kilotiwa, chapara na kuparuza,
Kwa hamu wasubiriwa, muwa upate maliza,
Beiye haifanani juisi ya muwa ghali.
Baada kuhakikisha, nywele zote metolewa,
Muwa huusimamisha, mashineni ukatiwa,
Kwa nyuma huupitisha, na mbele kuutolea,
Katu haifananipo, juisi ya muwa ghali.
Mara kadha’ hurudisa, ili juisi itoke,
Tena huubiringisha, kusudi ulainike,
Kwa nguvu pumzi kushusha, maji yapate yatoke,
Adhulumiwa muuza, juisiye bei ghali.

Mashine nazo hubana, hasa zile za asili,
Cha moto muwa huona, hadi badilika hali,
Hapo muwa huungama, haliye I tadhilili,
Madhulumu muuzaji, aongezewe beiye.

Muwa sasa ‘chopolewe, kwa mbwembwe na kwa madaha,
Hali ya utokajiwe, wengi huona karaha,
Maana siyo haliye, lipongia kwa furaha,
Jamani tukubalini, juisi ya muwa ghali.

Siri moja negundua, forodhani ‘lipokwenda,
Mashine si zote sawa, ziko nene na nyembamba,
Kuna zinazooshewa, ukatamani ziramba,
Ujira aogezewe, si rahisi kukamua.

Kuna zinazopuuzwa, holela zikatumiwa.
Viambazani hubanzwa, kazi zikishafanyiwa,
Hazikumbukwi kutunzwa, hata kwa maji kutiwa,
Huyu yuastahiki, bei ya chini kupewa.

Binafsi napata hoja, na haja ya kuuliza,
Muwa, mashine pamoja, na anaesukumiza,
Ni kipi kivikwe koja, kwa kazi kuitimiza?
Malenga saidiani, jibu hapa kupatiza.

Beti ihida ’ashara, zakifu kusimulia,
Kuelezea tijara, ya wanao para miwa,
Ombi kwao mshahara, nivyema kuongezewa,
Tusifanye masihara, kazi yao kazi ngumu.
Wakatabahu,
H. Hamad
MSc. Development & International Relations
Aalborg University
Denmark
zanzibaricon@hotmail.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. mzee wa libeneke kule kwa michuzi jr na haki kuna stori ya fitina za itv na radio one, mbona wewe huitoi? watu wana hamu nayo sana itoke kwenye ukumbi mpana kama huu waijadili aaah!

    ReplyDelete
  2. Bw. Hamad, hiyo dawa yake ndogo. Huku bara miwa bei ndogo tu. Unanunua muwa wako unatafuna na kutema fundo. Ndivyo wengi twafanya huku Bara, yakhe.

    ReplyDelete
  3. HH shairi lako zuri. ni kweli juisi ya muwa aghali na hususan wakati kama huu wa mwezi mtukufu. lakini uaghali wake hauna budi kuangaliwa katika mchakato wa kanuni za utashi na ugavi. kwa mfano, wakati kama huu wa mwezi mtukufu mashine nyingi hufungwa na hivyo utashi huwa mkubwa kuliko ugavi, na hivyo kusababisha bei ghali zaidi!!!! kwa kifupi, ndivyo kanuni za uchumi zinavyoelekeza!!!

    ReplyDelete
  4. Anon wa sep 07, 10.59PM Unayosema ni kweli kabisa kwa kipindi hiki cha ramadhani juisi ya miwa inakuwa ghali sana kutokana na mashine nyingi kufungwa .na nilipata kuongea na wapara miwa wa visiwani (Zanzibar)wanasema wao wanapendelea sana juisi ya miwa kutoka Bara zinakuwa nzito na sukari nyingi kuliko za zanzibar nyingi zinatengenezwa na mabua . mie ushauri wangu kwa wale wapara miwa wangetumia zile mashine za kisasa zenye matundu madogo pale wangejua hasa ladha ya sukari (utamu ) iliyoko kwenye miwa na biashara yao ingetoka kwa sana na faida mara dufu .
    mdau maalim Kifundo Uk.

    ReplyDelete
  5. "Juisi ya muwa ghali-Jawabu"

    Bismillah naanza
    Ubeti huu wa kwanza
    Nami nipate jifunza
    Utamu wa huo muwa

    Ila nataka kujuwa
    Vyereje wasifu muwa
    Ukaicha mashine
    Inayojuwa kamuwa

    Nisawa kusifu jino
    Ukauacha ufizi
    Au kusifu mlezi
    Ukasahau mzazi

    Bila mashine kubana
    Muwa hauna maana
    Utazimaliza zana
    Juisi kuikamuwa

    Sifa zende kwa mashine
    Isiyojuwa chaguwa
    Uwe Mnene, mwemba
    Yenyewe inakamuwa

    Uwe kutoka mahonda
    Mtibwa au kilosa
    Juisi hutokikosa
    Mashine ikiamuwa

    Asili ya shengejuu
    Au kutoka majuu
    Pumzi takwenda juu
    Muwa unapoutia

    Tena huminya vifundo
    Vilivyo vishinda nyundo
    Kwa madaha na maringo
    Juisi huikamuwa

    Ajabu ya rahmani
    Tena isiokifani
    Muwa huwa watamani
    Mashineni kuingia

    Mengine ya toka bara
    Lindi pia mtwara
    Hata ile isoparwa
    Mashineni yaingia

    Mashine na uchafuwe
    Si muwa na utamuwe
    Muhimu ni ikamuwe
    Juisi tujipatie

    Tamati nna maliza
    Kama sijakutatiza
    Lengo langu kuuliza
    Mashine waipuuza?

    Mahadhy!

    ReplyDelete
  6. Kaka Hamadi kama kweli unaongelea muwa basi hamna neno, ila kama huu muwa ni tafsida tu itakuwa balaa!

    ReplyDelete
  7. mashine ndio jawabu
    malenga ameshajibu
    asili ya muwa ugumu
    mashine kuziharibu

    ........
    Nawakilisha
    Mdau
    Trondheim - Norway

    ReplyDelete
  8. Kassuwi, S.ASeptember 08, 2009

    Kaka Hamadi, wastahil pongezi. Kwa mtazamo wangu wa haraka ni TAFSIDA nzito uloitumia kutoa ujumbe wako.Ama kwa hakika ujumbe umefika kwa wenye kuelewa maana.

    ReplyDelete
  9. Ahh Bableee nawe wamo????
    Keep it up
    Kakio

    ReplyDelete
  10. wajameni hiyo mi-verse mimi chali.
    muwa+machine=juice???????
    baghosha

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...