Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema akimtunuku nishani heshima Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam William kutokana na mchango wake wa kushirikiana na Jeshi la polisi kukabiliana na masuala mbalimbali wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani maafisa polisi, askari na raia (wafanyabiashara) waliotoa michango mbalimbali kulisaidia jeshi la polisi leo jijini Dar
Askari polisi mwenye cheo cha Koplo ,Deogari Maro (katikati) akipokea zawadi ya pikipiki kutoka kwa kamanda wa kanda maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani maafisa polisi, askari na raia (wafanyabiashara) waliotoa michango mbalimbali kulisaidia jeshi la polisi. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema akishuhudia makabidhiano hayo leo jijini Dar
JESHI LA POLISI KUENDELEA KUTOA TUZO KWA ASKARI NA WANANCHI.
Picha na Habari Aron Msigwa – MAELEZO.
Jeshi la Polisi limesema kuwa litaendelea kutoa tuzo kwa askari , raia na wafanyabiashara wanaotoa michango mbalimbali na kushirikiana na Jeshi hilo katika kufanikisha vita dhidi ya vitendo vya uhalifu nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani maafisa polisi na askari walioshiriki katika oparesheni za kulinda amani nchi Comoro na raia wema (wafanyabiashara) waliotoa michango mbalimbali ili kuliwezesha Jeshi la polisi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Amesema mpango huo wa utoaji tuzo kwa wafanyakazi bora wa jeshi la polisi, raia na wafanyabiashara wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi unatokana na jeshi kutambua mchango mkubwa walioutoa na wanaoendelea kuutoa katika kuboresha utendaji kazi ndani ya jeshi. Amefafanua kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwathamini askari wake kwa kuwapa motisha ili kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama ndani ya nchi unaimarishwa.
“Hata tukiwa na magari, tuwe na ndege ni lazima tuthamini askari wetu kuliko kitu kingine ili kuhakikisha ulinzi na usalama pamoja na maisha bora kwa kila mtanzania yanapatikana” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi wa Jeshi wataendelea kukaa pamoja ili kuvipima, kuviibua na kuviendeleza vithaminiwa vya polisi pamoja na kutoa zawadi kwa askari wanaofanya kazi nzuri ya kulinda mali na maisha ya raia ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wao na kuwapa sifa stahiki.
Kuhusu Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na raia wote katika Nyanja ya ulinzi shirikishi amesema kuwa Jeshi la Polisi linaandaa utaratibu ili kuhakikisha kuwa raia wote wanashiriki kikamilifu katika kujilinda wenyewe mahali wanakoishi pamoja na kuaandaa askari na maafisa wa polisi wa kudumu watakaoshirikiana na vikundi maalum vya ulinzi vitakavyoanzishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Kwa upande askari waliotunukiwa nishani kwa kushiriki harakati za kulinda amani nchini Comoro Generali Mwema amesema ni mfano wa kuigwa kwani walifanya kazi katika nchi tofauti na waliyoiazoea pamoja na kushirikiana kikamilifu na askari kutoka katika nchini nyingine zilizoshiriki operesheni za ulinzi wa amani nchini Comoro.
Hata hivyo amesema Jeshi la Polisi liko makini kuhakikisha kuwa mafunzo ya askari yanaboreshwa ili kuwawezesha askari kufanya kazi kikamilifu watokapo mafunzoni hatua hii ikijumuisha mpango wa kuongeza mafunzo kivitendo zaidi kwa askari kwenye maeneo ya raia.
Mbali na hilo amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya marekebisho kwa kuwawezesha kielimu askari wake ili kuwajengea uwezo na kulifanya kuwa la kisasa zaidi na lenye wataalam wa kutosha na hivyo kuongeza ufanisi katika majukumu ya kila siku.
Aidha ametoa wito kwa wananchi na kushirikiana na jeshi la Polisi katika kutimiza wajibu wake kwa ulinzi shirikishi na kuongeza kuwa mpango wa utoaji tuzo kwa wafanyakazi wa jeshi la polisi, raia na wafanyabiashara wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi utaboresha mawasiliano na ushirikiano zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Hongera jeshi la polisi, lakini bado naamini mchango mkubwa wa kuliimarisha jeshi la polisi unaweza kutoka kwa wananchi wenyewe,

    mchango hasa naamanisha wa hali na wa rasilimali,

    mfano, utaratibu wa police patrols hasa kwa kutumia pikipiki mimi nimeona kama una manufaa sana,

    pamoja na rasilimali zinazotoka serikalini ambazo ni dhahiri kuwa hazitoshelezi na hazitaweza kutosheleza kamwe (kwa maana ya asilimia 100, na hii ni kweli hata kwa nchi zilizoendela ambapo si ajabu bajeti za maendeleo kwenye sekta mbalimbali hukatwa kutokana na ufinyu wa bajeti)

    hivi jeshi la polisi haliwezi kuwa na deliberate efforts za kuhamasisha ulinzi kwa kupitia wananchi wenyewe?

    wananchi wanaendelea kulipa gharama kubwa za ulinzi kwa makampuni binafsi ambayo yanatoa huduma bora, lakini vipi ambao hatuwezi ku afford?

    hivi IGP hapawezi kuanzishwa kitengo pale makao makuu ya jeshi la polisi (au kipo? kiongezewe nguvu na kuongeza ubunifu) ambacho kitashughulikia kwa undani zaidi ulinzi shirikishi?

    Mi naamini watu wanaweza sana kushiriki katika ulinzi HASA kwa maana ya rasilimali endapo watahamasishwa na jeshi lenyewe

    mfano, mimi nna wazo kuimarisha patrols, jamii zinaweza kujipanga katika mipaka ya serikali za mitaa within wilaya zao na kuchangia ununuzi wa vyombo vya kurahisisha doria, kwa urahisi pikipiki na kuendeleza michango hio kuzi mantain hizo pikipiki kuziwekea mafuta kwa gharama zao,

    hivi tunatumia shilingi ngapi kuchangia harusi na sherehe?

    si kwamba sijui, kuwa jukumu hili kimsingi ni la serikali, nafahamu,

    natoa changamoto kwa jeshi la polisi kuendelea kujiimarisha, (ikiwa ni pamoja na kujisafisha: masuala ya rushwa na nidhamu; kwa suala la nidhamu naamini JWTZ ni mfano wa kuigwa,ukiondoa incidents za kupiga raia na polisi), lakini wakati jeshi linaendelea kujizatiti (tena big up kwa afande Mwema, jeshi linabadilika sana), tunaona mabadiliko hasa ya vitendea kazi( makao makuu, ujenzi wa nyumba kule kurasini n.k, ubunifu huo uendelee na maeneo mengine mfano vile "vibanda mfano wa nyumba pembeni ya mgulani JKT": ila mkishajenga MSIZIUZE,

    wakati jeshi linaendelea kujizatiti, je watanzania hatuwezi kuanza hizi jitihada zetu wenyewe?

    na je iwapo polisi hawatoshi, je hatuwezi kutumia JKT vile vile?

    wadau mnasemaje?

    Kaka michu hivi ujumbe huu unaweza kumfikia IGP?

    Mtanzania

    ReplyDelete
  2. kwa nini glovu na mapambo?

    ReplyDelete
  3. tanzania inajulikana sana kwa mchango wake iliotoa kulikomboa bara la afrika, lakini haya yote yanakwenda na wakati .tuliweza kufanya haya yote kwa sababu haya yote tunayoshuhudia sasa kama vile wimbi la ufisadi, kuanguka kwa uchumi duniani nk hayakuwepo, lakini naamini kabisa kwamba tanzania ya leo haistaili kabisa eti kujihusisha na mambo ya humanitarian eti kupeleka jeshi kusaidia comoro, ndani ya nchi yetu kwenyewe hakuna amani ya kutosha, umasikini ndio usiseme wananchi wetu wanaishi kama vile wanyama, hakuna umeme, hakuna uhakika wa maji safi, huduma za afya ndio usiseme, wananchi wetu ni masikini wakutupwa halafu tunajifanya kifua mbele kujenga ofisi za ubalozi za gharama nje, tunajifanya kusaidia eti kupeleka majeshi yetu kulinda amani nchi za nje kwa kweli inasikitisha sana na sijui vizazi vyetu vijavyo vikituuliza hivi kwa nini tulifanya hivi na tutajibu nini, kwa hareaka haraka tu hebu angalieni hizi nchi tulizozisaidia kujikomboa kutokana na ukoloni au kujikomboa kutokana na utawala dhalimu afrika ziko wapi leo? ni aibu tupu zinatushinda kiuchumi!!! angalia angola, mozambique, south africa nk...vijana wetu wanarudishwa mipakani mwao eti ni masikini na wakiwa huko wataiba? wamesahau kuwa sisi ndio tuliwasaidia kupata uhuru ambao wanalingia sasa/ je kuna ulazima wowote kwa tanzania kuendelea kupeleka majeshi yake kulinda amani afrika? inauma sana tena sanaa..tuende na wakati ya leo sio ya jana..kuna usemi usemao jisaidie na mungu atakusaidia, nitalisaidia jeshi la polisi nikiona jeshi lenyewe linajisaidia mfano kutokomeza vitendo vya rushwa, uonevu kama vile kubambikia watu kesi, umangimeza katika jeshi la polisi, kuonea raia wema mfano jeshio la polisi lilivyofanya kule zanzibar huko nyuma ,kupiga raia wasio na hatia kama vile wanawake, kutumia siraha za moto kutawanya wananchi wasio na siraha nk...tanzania, tanzania nakupenda kwa moyo wote ila vitendo vya watawala wako sivipendi...kama nimekosea wadau naomba msamaha na nikosoeni...

    ReplyDelete
  4. mnachekesha!!! majambazi na wezi wanatutesa kila siku kukicha, usiku na mchana pamoja na asilimia kuwa ya polisi kunyanyasa raia kwa kulazimisha makosa ili wakutowe rushwa, mimi naona bado kazi kubwa inatakiwa kufanywa na polisi hasa swala na rushwa kwao, majambazi na wezi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...