MABADILIKO YA SIKU YA TAIFA KUPANDA MITI

Serikali imebadilisha Siku ya Taifa ya Kupanda Miti kutoka Januari Mosi ya kila mwaka na kuwa Aprili Mosi. Mabadiliko hayo yametokanana Waraka wa Waziri Mkuu Na 1 wa mwaka 2009 kuhusu kubadili Siku ya Taifa ya Kupanda Miti kutoka Januari Mosi na kuwa Aprili Mosi ya Kila mwaka.

Kwa mujibu wa waraka huo, kuanzia mwaka 2010 Siku ya Taifa ya Kupanda Miti itaadhimishwa Aprili Mosi ya kila mwaka. Waraka huo unaanza kutumika rasmi tarehe 01 Juni, 2009 na unafuta waraka wa Waziri Mkuu Namba 1 wa Oktoba, 2000.

Uamuzi wa kubadilisha siku hiyo unatokana na mapendekezo yaliyotolewa na Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Januari Mosi 2008 aliposhiriki maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti na kutaka maadhimisho hayo yahamishiwe kipindi ambacho sehemu nyingi za nchi zitakuwa zinapata mvua.

Kwa mujibu wa waraka huo, Aprili Mosi itakuwa ni siku ya Taifa kuhamasisha upandaji miti huku kila mkoa ukiendelea kujipangia Siku ya Kupanda Miti kutokana na majira ya mvua yatakavyoruhusu. Ili kazi ya kupanda miti iwe inatekelezwa na wadau wote, Waraka huo umeagiza Wizara, Mikoa, Wilaya, Viongozi wa wilaya, Halmashauri za Jiji, Manispaa na Mamlaka za Miji midogo, Tarafa, Kata, Vijiji na mitaa kuandaa programu za utekelezaji mapema iwezekanavyo.

Maafisa Misitu walioko mijini, mikoani, wilayani na vijijini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu aina ya mbegu na miche inayofaa katika eneo husika na kushauri utayarishaji wa vitalu vya miche kwa wakati unaofaa.

Waraka umemtaka kila kiongozi ahakikishe zoezi la upandaji miti linatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo kwenye eneo lake. Aidha, pamoja na masuala mengine kiongozi atapimwa kutokana na juhudi zake za kuhamasisha, kutekeleza na kusimamia wananchi kupanda miti. Halmashauri zote kwa kushirikiana na mamlaka husika, zihakikishe kuwa upandaji miti ni pamoja na kupanda kando kando ya barabara zote nchini.

Waraka huo umetahadharisha kuwa kupanda miti pekee hakutoshi kukabiliana na jangwa kama hatua za makusudi za kutunza na kulinda uoto wa asili hazitachukuliwa. Siku ya Taifa ya Kupanda Miti iliadhimishwa kitaifa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 katika eneo la Jangwani mkoani Dar es Salaam.


Ezekiel Maige (Mb)
NAIBU WAZIRI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. WAKATI WATANZANIA TUNAJITAHIDI KUPANDA MITI, WENZETU WASIA WENYE MAKAMPUNI YA MABANGO YA BIASHARA WAO WAMEONGEZA KASI YA KUKATA MITI ILI MABANGO YAO YAONEKANE KWA MBALI; NA SASA TEMESHUDIA BARABARA YA NYERERE AMBAPO DUKA MOJA LILILOANZISHWA HIVI KARIBUNI KWENYE BARABARA YA HUDUMA, WAO PIA WAMEKATA MITI ILIYOOTESHWA KATIKATI YA HIZO BARABARA MBILI ILI DUKA LAO LIONEKANE KWA MBALI. UPANDAJI WA MITI HAUTAKUWA NA MAANA KAMA JIJI HALITATUMIA SHERIA INAYOKATAZA UKATAJI MITI HOLELA KWA WENYE MABANGO WAMEKUWA TA TABIA YA KUNG'OA MITI ILIYOPANDWA KANDO YA BARABARA KAMA INAVYOTOKEA NJIA PANDA YA KAWAWA NA NYERERE.

    ReplyDelete
  2. Inakuwaje tupande miti siku ya wajinga duniani?

    ReplyDelete
  3. Itakuwa siku ya mapumziko kama ilivyokuwa Januari Mosi??

    Hata hivyo, naona hakuna haja ya kuwa na siku maalum ya kufanya mambo fulani ambayo ni wajibu wetu kuyafanya!! Ni kiwango tu cha ustaarabu wetu kiko chini ndio maana tunaona kuwe na siku ya kutimiza wajibu fulani!! Hivi mtu akikwambia kuna siku ya kuoga, itakuwa na maana gani?? Nonsense!!

    Miti mingi inayopandwa wakati kamera zinatumulika inaishia kunyauka (na kuteseka bure heri isingepandwa kabisa). Tujifunze utaratibu wa kutimiza wajibu wakati kaera zinaangalia sehemu nyingine au zimezimwa!!

    Aprili mosi ibakie siku ya waji.... (anyway, another funny thing).

    ReplyDelete
  4. Haina maana kupanda miti 1st April:

    *Ni siku kuu ya wajinga. Kwa nini kitu cha maana kiadhimishwe na siku kuu ya wajinga?

    *Kuna maeneo mvua zimekwishaanza- Mbeya, Tukuyu, Sumbawanga n.k. na serikali ya Mwalimu Nyerere (Rais pekee wa nchi hii aliyewahi kuwa na upenzi na uchungu wa dhati wa nchi hii) ilikwisha sema mvua za kwanza ni za kupandia, na tunakumbushwa mara kwa mara kwenye TBC radio pia (Wosia wa Baba). Inaleta maana zaidi kwa hiyo kwa kanda mbali mbali kuwa na siku yao kufuatana na mvua zinaanza lini kanda hiyo.

    *Kuna haja ya kuwa na siku ya kitaifa kuadhimisha ya kupanda miti pia kwa sababu swala lenyewe lina umuhimu wa kitaifa, kama sio kidunia.Lakini siku hiyo haiwezi kuwa siku ya wajinga kamwe! 1 januari inapendeza kwa maana wananchi tunaweza kuaswa, kukumbushwa, kuhamasishwa na kutakiwa n.k. kupanda miti ya idadi fulani katika mwaka huo kabla ya tarehe maalum ambayo wataalam wanaweza 'kuidetermine' ili nchi yetu iepukane na madhara ya kimazingira fulani (Jangwa?)au ipate mafanikio au manufaa fulani katika kipindi fulani.
    *1st April seems definetely foolish. What's the logic? Kuna mtu anampoteza na kumpindisha Pinda?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...