Michanganuo ya mahitaji
itaongeza ufadhili kwa vituo vya afya
BENKI ya KCB Tanzania imevitaka vituo vya afya nchini kutengeneza michanganuo ya mahitaji ya vifaa wanavyovihitaji jambo litakalosaidia kuvutia wahisani na taasisi mbalimbali nchini kujitokeza kuvichangia vituo hivyo. 
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Janet Mbene kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya milioni 4.3 kwa kituo cha afya cha Buguruni.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mbene alisema kuwa ingawa wafadhili wana nia ya dhati kujitokeza kuvisaidia baadhi ya vituo nchini lakini kukosekana kwa michanganuo inayoainisha mahitaji kumechangia kwa kiasi kikubwa wengi miongoni mwao kuhofia kuchangia katika masuala ya kijamii kama hayo.
“Kutokana na hilo natoa rai kwa uongozi wa Kituo cha Afya Buguruni kutengeneza orodha ya vifaa wanavyovihitaji kutoka kwa wafadhili ili kusaidia taasisi zingine kama KCB kujitokeza kuchangia. Nami natumia fursa hii kuwaagiza watendaji wangu kuandaa programu ya kuendelea kukisaidia zaidi kituo hiki,” alisema Mbene.
Mbali na hayo Mbene ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mbunge alisema KCB itaendelea kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia wajibu ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii inayowazunguka jambo litakalosaidia kupunguza umaskini nchini.
“Kwa kutambua tatizo la uhaba wa vifaa benki yetu imeona haina budi kusaidia kidogo. Ni imani yetu kubwa kuwa vifaa hivi vitaongeza ufanisi wa kazi hospitalini hapa na kusaidia wagonjwa mbalimbali,” Mbene alisema.
Awali Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dk Mwajuma Mbaga alisema kituo hicho kinachohudumia wagonjwa takribani 700 kwa siku kutoka mitaa 17 ya Buguruni, Kiwalani, Vingunguti na Tabata inakabiliwa na mfumo wa jengo uliozidiwa na huduma wanazotoa na idadi kubwa ya wagonjwa.
“Tunaomba wafadhili wengine wajitokeze kutusaidia kama mlivyofanya nyinyi KCB, kwani bado tunakabiliwa na uhaba wa watumishi na upungufu wa vitendea kazi. Hali ya uchangiaji ikiendelea hivi ni matarajio yangu baada ya miaka mitatu hali inaweza kutengamaa,” alisema Dk Mbaga. 
Baadhi ya vifaa hivyo vilivyokabidhiwa na benki hiyo kwa Dk Mbaga ni mashine ya kuchapisha picha za mionzi (Ultra Sound Printer), mashine ya kupima mapigo ya moyo ya mtoto aliyeko tumboni (Dottla Machine) na mashine ya kutoleo Oxygen (Oxygen Concentrator).
Kituo cha afya Buguruni kimekuwa kikitoa huduma za tiba mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu (TB), kambi ya wagonjwa wa kipindipindu, huduma za mama na mtoto, kujifungua, kuwahudumia wenye VVU (CTC) na ikiwemo upimaji wa hiari ugonjwa wa Ukimwi.


 
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...