Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akihutubia Mkutano wa IFAD kuhusu maendeleo ya kilimo jijini Rome, Italia, leo akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete. WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema ruzuku inayotolewa kwa wakulima wa nchi tajiri inasababisha ughali wa chakula duniani na ndiyo inayowateketeza
wakulima wadogo wadogo katika nchi masikini hasa Afrika.
Alikuwa akitoa kwa niaba ya Rais Kikwete hotuba muhimu ya mkutano wa 33
Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (*International Fund for
Agriculture Development – IFAD)* mjini Roma, Italia leo (Jumatano Feb. 17,
2010).
Mhe. Pinda alisema kuwa ruzuku kubwa inayotolewa kwa wakulima katika nchi zilizoendelea inafanya mazao ya kilimo kutoka nchi zinazoendelea yashindwe
kushindana katika soko.
Alisema kuwa, kwa bahati mbaya suala la ruzuku hiyo ndiyo kikwazo kikubwa
kinachochelewesha majadiliano ya Doha kuhusu maendeleo ya ya kiuchumi na
biashara dunaini (Doha Development Round).
“Kwa hiyo, ruzuku kwa kilimo ndiyo sehemu ya sababu za kupanda kwa bei ya
chakula duniani na kuteketeza kilimo cha wakulima wadogo wadogo katika nchi zinazoendelea, hasa katika bara la Afrika,” alisema.
Mhe. Pinda alisema tatizo jingine ambalo ni kikwazo cha kuendeleza kilimo
katika Afrika ni ukosefu wa huduma za kifedha za kuongeza mitaji na
uwekezaji kwa wakulima wadogo.
“Pamoja na mtazamo kuwa sekta ya kilimo haina uhakika katika uwekezaji,
kutoa mikopo kwa wakulima wadogo siyo jambo linaloafikiwa na benki yoyote
ile ya kibiashara,” aliongeza.
Wengine waliohutubia mkutano huo ni Rais Giorgio Napolitano wa Italia na
Rais wa IFAD, Bw. Kanayo Nwanze.
Mapema, Waziri Mkuu alifanyiwa mahojiano maalum na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Televisheni la CNN la Marekani, Bw. Jim Clancy na baadaye akashiriki katika mdahalo uliowajumuisha watalamu mbalimbali wa masuala ya kilimo na uchumi ulioendeshwa na mtangazaji huyo.
Wengine katika ujumbe wa Waziri Mkuu ni Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Mhe. Stephen Wassira; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Mazingira wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Burhan Sadat Haji na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje, Balozi Seif Iddi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...