JK ameondoka nchini mchana wa leo, Jumamosi, Machi 20, 2010, kwenda Namibia kwa ziara ya siku tatu ambapo miongoni mwa mambo mengine, atashiriki katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hifikepunye Pohamba.

Aidha, JK na ujumbe wake ambao ni pamoja na Mama Salma Kikwete, utadhuhuria sherehe za miaka 20 tokea uhuru wa Namibia mwaka 1990. Sherehe zote mbili zitafanyika kwa pamoja mjini Windhoek, kesho, Jumapili, Machi 21, 2010.

Mheshimiwa Pohamba na chama chake tawala cha SWAPO alishinda Urais wa Namibia kwa mara ya pili katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 27-28, mwaka jana, 2009, kwa asilimia 75 ya kura zote.

Huo ulikuwa uchaguzi mkuu wa nne tokea Namibia kupata uhuru na matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa Desemba 4, mwaka jana.

Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa viongozi wengine kutoka nchi wanachama cha Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) walioalikwa kushiriki katika sherehe hizo wakiwamo Rais Bingu Mutharika wa Malawi, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Jose Eduardo Do Santos wa Angola na Rais Rupiah Banda wa Zambia.

Serikali ya Namibia pia imewaalika Watanzania wengine ambao walitoa mchango mkubwa katika Vita vya Ukombozi wa Namibia na hivyo kuchangia uhuru wa nchi hiyo.

Miongoni mwa Watanzania hao ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika (OAU) Mheshimiwa Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU, Brigedia (mstaafu) Hashim Mbita na Mama Maria Nyerere, Mke wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mheshimiwa Rais Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kurejea nchini keshokutwa, Jumatatu, Machi 22, 2010.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

20 Machi, 2010

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...