Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mh. Pius Msekwa, akihutubia wakati wa Sherehe za CCM Tawi la Uingereza za kutimia Miaka 33 ya Chama Cha Mapinduzi huko Reading, Uingereza, wikiendi ilopita. Kulia ni Balozi wetu Uingereza Mh. Mwanaidi Maajar Mh. Msekwa alipata nafasi ya kupeana mkono wa pongezi na viongozi na wanachama wa CCM tawi la Reading na mashina mapya ya London Mashariki na Kusini

Mh. Msekwa akikabidhi vitendea kazi kwa viongozi
wapya wa CCM mashina mapya ya London Mashariki na Kusini
Sehemu ya ukumbi ilikofanyikiwa sherehe hiyo
Mhe Msekwa akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wapya wa CCM Tawi la Uingereza.

MSEKWA AUNGURUMA SHEREHE ZA 33 CCM UINGEREZA.

Na Ripota wetu, Reading
Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Mheshimiwa Pius Msekwa amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi ndiyo chama cha siasa pekee kinachoweza kujizalisha ki muundo, itikadi na sera ili kukidhi mahitaji ya watanzania wengi kwa nyakati tofauti.

Akihutubia umati mkubwa wa wana CCM waliohudhuria kuadhimisha sherehe za miaka 33 ya CCM huko Reading, Uingereza, Mheshimiwa Msekwa alisema azimio lililounda CCM mwaka 1977 linabaki imara kutaka CCM kiwe chombo madhubuti kwa muundo, fikra na vitendo vyake ili kumkomboa mwananchi na kuinua maendeleo ya Taifa.

Alisema CCM imezidi kunufaika kifikra kutokana na kuendelea kuboresha muundo wake ikijumuisha pia matawi ya wasomi wa elimu ya juu na yale ya nje ya nchi.

Mheshimiwa Msekwa alitahadharisha kuwa Azimo la Zanzibar la Februari 1991 halikuvunja Azimio la Arusha isipokua lilitazama upya masharti ya uanachama wa CCM na hasa ibara ya 8(7) ya katiba ya CCM toleo la 1987.


Azimio la Zanzibar liliondoa miiko ya uongozi iliyowabana halaiki ya wanachama walio wakulima na wafanyakazi wa kawaida hasa baada ya mabadiliko ya uchumi na siasa ya vyama vingi.

Hivyo alionya kuwa CCM na serikali yake haitawavumilia watovu wa maadili wanaokighilibu Chama na kuhujumu uchumi kwa kutumia mwanya wa CCM kujisahihisha, kujiboresha na kujiimarisha.

Mheshimiwa Msekwa aliyeonyesha uwezo mkubwa wa kukifahamu Chama, Bunge na Serikali, alijadili kwa kina changamoto mbali mbali ambazo CCM imepitia baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.


Akizungumzia mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, Mhe Msekwa alisema mfumo wa uchaguzi uliokuwepo ulitoa mwanya wa rushwa kwa watu wasio waadilifu na wenye uwezo mkubwa wa fedha kununua kura.

Huku akishangiliwa umati wa Watanzania, Mhe Msekwa alibaini kuwa ukiukwaji wa maadili utakwisha baada ya CCM kupanua wigo wa demokrasia katika uchaguzi na kupitishwa kwa sheria mpya ya gharama za uchaguzi mwaka huu.

Awali akimkaribisha Mheshimiwa Msekwa, Mwenyekiti wa CCM Tawi la UK ndugu Maina Owino alisema hatua za makusudi zinazo chukuliwa na CCM kuboresha, muundo, fikra na sera ili kukidhi mahitaji ya watanzania wa jinsia zote ni wa lazima kwa nyakati na uimara wa chama.


Alisema Serikali ya CCM ni lazima iwajibike kikamilifu na kwa ufanisi ili kusanifisha ridhaa na dhamana iliyopewa na wananchi.

Ndugu Owino alikumbusha kuwa watanzania wanaoishi nje ya nchi wamekuwa wanachangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu hususan katika sekta za kilimo na usafirishaji, vifaa vya elimu na utaalamu, afya na michezo na sasa umefika muda serikali iwatambue na kusajili rasmi mchango wao.

Alidokeza kuwa Watanzania wa ughaibuni wanakwamishwa na ukiritimba usio wa lazima na kusababisha kupoteza vifaa vingi, kulipa gharama ambazo zisingekuwa za lazima au kujengewa mazingira ya rushwa katika maeneo ya mamlaka za bandari, viwanja vya ndege, kodi ya mapato na uhamiaji.

Aidha aliziomba serikali na Bunge wazipokee na kuzifanyia kazi hoja za Diaspora bila walakini. Alimtaarifu mheshimiwa Msekwa kuwa wazaliwa wa Tanzania wenye uraia wa kufikia ughaibuni wanatambua kuwa mapenzi, malengo na hatima ya maisha yao yapo Tanzania.

Idadi kubwa ya watanzania kutoka miji mbalimbali walijiunga na Chama Cha Mapinduzi na walifurahia kukabidhiwa kadi zao na mheshimiwa Msekwa.

Mheshiwa Msekwa aliwaasa watanzania kuendeleza uzalendo, kuwa wabunifu na wajasiria mali.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...