Waziri wa Fedha na Uchumi Mh. Mustafa Mkullo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari mjini Kilosa juu ya mchanganuo wa ugawaji wa misaada kwa waathirika wa mafuriko ya wilayani humo katika mkutano na waandishi wa habari . Misaada hiyo mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 51 imetolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na yeye baada ya kuipata kutoa Serikali ya China.
Habari na Picha
Na Tiganya Vincent- MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa misaada ya jumla ya shilingi milioni 51 kwa ajili ya wakazi wa Wilaya Kilosa walioathiriwa na mafuriko.

Misaada hiyo ni kwa ajili ya kusaidia maeneo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo elimu , ulinzi , michezo na ujenzi mpya wa makazi.

Akisoma taarifa ya Ikulu ya utoaji wa misaada hiyo juzi kwa waandishi wa habari wilayani Kilosa Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuwa Rais Kikwete aligawanya katika taasisi mbalimbali za umma zilizomo katika wilaya hiyo.

Alitoa ufafanuzi kuwa Rais Kikwete ameagiza kuwa mipira 1,500 itolewe katika Shule zote za Msingi zilizoko katika eneo lililoathiriwa na mafuriko na pikipiki tano zipelekwe katika vituo vya Polisi vya Kimamba , Mikumi, Dumila na Polisi wilaya ili kusaidia kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

Mkulo alisema kuwa redio 1,500 zitapelekwa katika shule za msingi na Sekondari katika maeneo yaliyoathiriwa ili wanafunzi hao waweze kutumia redio hizo kwa ajili ya kupata masomo waliyokosa katika maeneo ambayo hawakuyasoma kipindi cha mafuriko.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete pia ametoa baiskeli 80 kwa ajili ya ya kuwagawia kila Ofisa Mtendaji wa Kata na Waratibu wa Elimu Kata ili waweze kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu.

Mkulo alisema kuwa kwa upande televisheni 15 zitatolewa kwa Sekondari tatu zilizoko katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko ambapo kila moja itapata moja na nyingine mbili zitapelekwa katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi na Chuo cha Vijana wilayani humo kitapata televisheni mbili pia.

Aliongeza kuwa Chuo cha walimu kitapatiwa televisheni 4 na Chuo cha Utafiti cha Kilimo cha Ilonga (LITI) kitapatiwa televisheni mbili.

Aidha Mkulo alisema kuwa Rais Kikwete ametoa jozi 3,600 za kandambili kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari zilizoathirika na mafuriko na kutoa mabati 554 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za baadhi ya wananchi waliothirika na mafuriko.

Vile vile Rais Kikwete ametoa vyerehani 50 kwa vikundi vya akina mama katika maeneo yaliyoathirika na Jenereta tano(5)za umeme wa upepo kwa ajili ya kusaidia kusambaza umeme katika makambi ya watu walioathirika na mafuriko hayo.

Mkulo alisema kuwa pia Rais Kikwete ametoa seti 20 za vyombo vya muziki na kuagiza vitolewe katika vyuo vilivyopo katika maeneo yaliyoathiriwa na pia ametoa mashine za maji tano kwa ajili ya vituo vya Afya vilivyoathiriwa na mafuriko.

Msaada hiyo ni sehemu ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete aliyowapa waathirika hao alipowatembelea mapema kwa huu.

Kiasi cha watu 23,000 bado wanaishi katika makambi ya muda katika maeneo ya Kibamba na mji wa Kilosa kufuatia mafuriko hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Jamani tuache kuwa ombaomba.

    ReplyDelete
  2. ndoto ya mchanaApril 04, 2010

    Rais hajatoa misaada ila serikali ya China imetoa misaada na imepitia kwake.

    ReplyDelete
  3. Mbona sekta ya Afya haijakumbukwa katika mgao huo? Ina maana hakuna Zahanati au hospital ya Wilaya ambazo kwa namna moja au nyingine walishiriki katika kutoa huduma katika kipindi cha mafuriko kwa kushirikiana na mashirika kama Red Cross. Nashauri nao wakumbukwe katika mgao huo.

    Mdau Ughaibuni

    ReplyDelete
  4. Kichwa cha habari hakiendani na ukweli wa hiyo habari "Mchango wa Misaada ya JK kwa waathirika wa mafuriko kilosa" huo mchango unatoka mfukoni kwa huyo jk? ama ni wa wachina? michuzi hii imekaa kiudakuudaku.usiibanie

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...