Mwita Kemaronge wa timu ya Mkoa wa Mara akienda kufunga mbele ya msitu wa mabeki wa timu ya Mkoa wa Kilimanjaro katika mechi iliyochezwa jioni hii ndani ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha katika mashindano ya Kili Taifa Cup yanayoendelea katika vituo sita nchini.


na mwandishi maalumu,
Arusha

MARA ilianza vyema kampeni ya kuwania Kombe la soka la taifa, Kili Taifa Cup baada ya kuilaza Kilimanjaro, mabao 3-2 katika mchezo wa ufunguzi wa kituo cha hapa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa.

Shukrani kwao, Noel Makunja, Mwita Kamaronge na Furumence Tungaraza wafungaji wa mabao ya washindi katika mchezo huo- wakati mabao ya kufutia machozi ya Kilimanjaro yalitiwa kimiani na Ben Rafael na Victor Ndozero.

Kilimanjaro walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 34, baada ya Ndozero kuuwahi mpira uliorudi na kufumua shuti kali lililogonga mwamba wa juu ndani kabla ya kutua kwenye mikono ya kipa Msafiri Shaibu, lakini mwamuzi Peter Mujaya aliyehamishia makazi yake Mwanza kutoka Pwani, akasema mpira uwekwe kati.

Makunja aliisawazishia Mara dakika mbili baadaye kutokana na shambulizi lao kali la kushitukiza, kabla ya Ndozero kuifungia Kilimanjaro bao la pli dakika ya 43.

Hadi mapumziko, Kilimanjaro walikuwa mbele kwa mabao 2-1- na kipindi cha pili, Mara ilianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika tatu tangu kuanza ngwe hiyo, kabla ya Tungaraza kufunga la ushindi dakika ya 56, akitumia udhaifu wa mabeki wa Kilimanjaro kudhani ameotea.

Katika mchezo huo, wachezaji wawili wa Mara walitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu, hao ni Ismail Fundi aliyempiga kiwiko Amro Guya akilipa kisasi cha kukwatuliwa na dakika ya 88, kipa Emanuel Mseja naye alipewa adhabu hiyo, baada ya kumkwatua Philipo Alando wakati anakwenda kufunga.

Wakati huo, tayari Kilimanjaro walikuwa wamekwishakamilisha idadi ya wachezaji wa kubadilisha, hivyo Ndozero akavaa glavu na kumalizia mchezo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...