Katibu Mkuu wa wizara ya Habari na Mawasiliano nchini Kenya Dr. Bitange Ndemo akifungua mkutano wa siku mbili kuhusu wajibu wa vyombo vya habari katika kuleta maendeleo barani Afrika uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Laico Regency jijini Nairobi.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya chuo Kikuu cha Daystar Dr. Levi Oboyo (katikati) akimuonyesha kitu Katibu Mkuu wa wizara ya Habari na Mawasiliano nchini Kenya Dr. Bitange Ndomo (kulia) wakati mkutano wa siku mbili kuhusu wajibu wa vyombo vya habari katika kuleta maendeleo barani Afrika uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Laico Regency jijini Nairobi. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho Dk. John Masso.
Wadau mbalimbali wa habari wakimsimkiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Mawasiliano nchini Kenya Dr. Bitange Ndemo (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa siku mbili kuhusu wajibu wa vyombo vya habari katika kuleta maendeleo barani Afrika uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Laico Regency jijini Nairobi.
Na Anna Nkinda - Nairobi
Vyombo vya habari barani Afrika vimetakiwa kuandika zaidi habari zinazohusu maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla na siyo kupendelea kuandika habari zinazuhusu mambo ya siasa pekee.
Dk. Ndembo alisema kuwa hivi sasa vyombo vingi vya habari vimekuwa nikikazania kuandika habari za siasa tu na kusahau kuandika habari zinazohusu maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.
“Wanasiasa hawawezi kuibadilisha jamii kwa maneno lakini vyombo vya habari vinaweza kuibadilisha jamii kupitia mabaraza ya habari ambayo yatawahimiza waandishi wa habari kuandika habari za maendeleo”, alisema Dk. Ndembo.
Katibu Mkuu huyo alitoa mfano wa madhara ya Internent vijijini na kusema kuwa katika kijiji fulani ambacho hakukitaja jina alimkuta mtu ambaye hana utaalamu wowote wa mambo ya afya akiwa anawafundisha wanawake jinsi ya kujikagua matiti yao na kugundua kama wanadalili za ugonjwa wa kansa ili waende hospitali kupata huduma na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni habari nzuri ya kuandikwa lakini waandishi wengi wamekazania mambo ya siasa tu na siyo mambo yanayohusiana na jamii.
Pia alitoa mfano wa machafuko yaliyotokea nchini Kenya mwaka 2007 na kusema kuwa waandishi wengi wa habari waliandika habari ambazo ni negative na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo kwa jamii .
Kuhusiana na Runinga nyingi nchini Kenya kuonyesha picha za nje ya nchi kama Nigeria, bara la Ulaya na Amerika alisema kuwa hivi sasa kazi waliyonayo ni kuhakikisha kuwa wanaimarisha uzalishaji wa filamu za ndani ambazo zitautangaza utamaduni wa Mkenya.
Alisema, “unapoangalia picha za kinaigeria mambo unayojifunza ni machache kwani mambo mengi yanayotendeka kule ni tofauti kabisa na hali halisi ya maisha ya wakenya hivyo basi Runinga zetu zinatakiwa kuonyesha filamu zinazuhusu maisha halisi ya mkenya”.
Kwa upande wa taarifa za habari za Runinga alisema kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kutafuta wakalimani ambao watawatafsilia wananchi walioko vijijini wasiojua lugha za Kiswahili na kiingereza kwa lugha ya makabila yao kwani wengi wao hawajui lugha hizo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Daystar Dk. John Masso alisema kuwa hivi sasa wananchi wanataka kujua mambo mbalimbali yanayoandikwa na vyombo vya habari na kutoa mfano kuwa mkulima anazalisha mazao ambayo watu wanataka kuyanunua ndivyo ilivyo na kwa vyombo vya habari wanazalisha vitu ambavyo watu wanataka kuvisoma, kuvisikiliza na kuona hivyo basi wanahabari wanatakiwa kutangaza maendelea ya nchi.
“Vyuo vya habari vinawafundisha wanafunzi kuhusu maadili na sheria za uandishi wa habari kama waandishi wa habari watayafuata waliyofundishwa chuoni ni lazima wataleta mabadiliko ya maendeleo na nchini kwani wataandika habari ambazo wananchi wakizisoma watapata elimu kuhusiana na kazi zao za kila siku”, alisema Dk. Masso.
“Kila mtu anahaki ya kupata habari hiyo ni sehemu moja wapo ya haki za binadamu vituo vya redio za jamii ni njia moja wapo ya kupambana na umaskini barani Afrika kama vitatumiwa ipasavyo katika kuwaelimisha wananchi lakini tatizo kubwa linalovikabili vituo hivi vya redio ni mahali pa kupata fedha ambazo watazitumia kutengeneza vipindi mbalimbali vya kuwaelimisha wananchi”, alisema Mutua.
Alisema kuwa hakuna maendeleo yatakayopatikana barani Afrika bila wananchi kupata mawasiliano ya habari hivyo basi ni muhimu kwa waandishi wa habari kuandika mambo yanayohusu maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Kuhusiana na matangazo mbalimbali yanayooneshwa katika runinga na mabango ya matangazo Joseph Nyanoti kutoka USIU alisema hivi sasa wananchi wananunua magazeti kwa bei naafuu na pia hawalipii huduma wanazopata za Redio na Runinga kwa kuwa kuna matangazo yanayovilipa vyombo vya habari lakini matangazo mengi hayasemi ukweli wa madhara ambayo watu watayapata baada ya kutumia bidhaa zao bali yanataja faida tu utakazozipata.
Nyanoti aliendelea kusema kuwa matangazo mengi yanawaonyesha wanawake ni watu wanaokaa nyumbani na watoto hawafanyi kazi jambo ambalo siyo kweli ukilinganisha na wanaume ambao wanaonyeshwa kuwa wanafanya kazi na wako makini kwa mambo wanayoyafanya.
Watoa mada katika kmkutano huo ambao ni wahadhiri kutoka vyuo vikuu vinavyotoa taaluma ya habari Afrika ya Mashariki walisema kuwa ni jambo la muhimu kwa mwandishi wa habari kujiandaa vya kutosha kabla hajaenda kutafuta habari hii ikiwa ni pamoja na kuchagua source mzuri wa habari yake ambaye atampa taarifa za kutosha na zenye uhakika.
Pia waliwataka waandishi wa habari wabalance habari zao wanazoziandika kila siku na kusema kuwa mahali ambapo mwandishi atapata mafunzo ya kutosha ni darasani na siyo mahali pengine.
Wataalamu hao wa mambo ya habari walishauri kuwa hivi sasa ni jambo la muhimu kwa Serikali pamoja na sekta binafsi barani Afrika kutumia vyombo vya habari ili kuleta maendeleo katika jamii kwani bila ya vyombo vya habari maendeleo hayawezi kupatikana .



Michuzi Hii habari imechukua page kubwa lakini hausiani na sisi waTz, nafikiri ingetakiwa iwe kwa blog ya Nation media na magazeti yake.
ReplyDeletehuo ndiyo ushauri wangu
Ni maoni yako, ila sisi wanahabari inatuhusu sana na hata jamii tunayoitumikia. Usiwasemee wenzako sema mimi mtanzania.Mdau
ReplyDelete