Uzee kitu adhimu, huo ninauingia
Ujana sasa adimu, Shabani aliusia
Maungoni mwangu humu, uzee unanijia,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mbali ninamuachia, rafiki yangu ujana,
Miaka inakimbia, ya leo siyo ya jana,
Nabaki nakumbukia, nilipokuwa kijana
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Shabani aliandika, kaulilia ujana,
Ni vipi unamtoka, kashindwa kuung’ang’ana,
Meno yalimdondoka, na nguvu tena hamna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Taratibu waingia, uzee wabisha hodi,
Siwezi kuukimbia, hata niwe mkaidi
Hata nikitukania, ndivyo napigwa baridi,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee

Mvi sasa zanijia, nimejaribu kung’oa
Kidevu zasalimia, na miye nazichomoa,
Nikitoa zazidia, nami nazidi kutoa!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mapensi nayaachia, na macheni ya shingoni,
Hereni nilivalia, kwenye sikio jamani,
Mwendo nilibadilia, nilivyonesa njiani,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Niliwapata mademu, tena wengine kwa zamu,
Nikaitwa mtaalamu, wa mambo yale matamu
Sasa yanitoka hamu, nanyimwa hata salamu!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nilenda nilipotaka, wasiponitaka nilenda,
Sikuwa na hata shaka, ati mtu kunidunda,
Leo naogopa paka, ninavutwa kama punda,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mwendo wa kudemadema, nikishika natetema,
Uso umenikunjama, natembea nikihema,
Magoti nayo yauma, uzee si lele mama!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kumbe maisha ni hivi, uzee haukwepeki,
Ninazikubali mvi, hata kama sizitaki,
Uzee siyo ugomvi, ujana haushikiki,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kweli nilifurahia, enzi zile za ujana,
Kamwe sintoyarudia, yalopita naagana,
Uzee nakumbatia, kwani lingine hakuna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nasubiri wajukuu, nione na vitukuu,
Nakunja miguu juu, na mshukuru Mkuu
Kuona umri huu, enzi hizi ni nafuu,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Na. M. M. Mwanakijiji
(Sauti ya Kijiji a.k.a Vuvuzela Matata)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 01, 2010

    Mwanakijiji
    Bonge la shairi, nicheka kweli maana
    hizi mvi basi tena. Lakni wengine wanazipenda a little gray you know! U Remember BillyJean? Enzi za DarHot!!

    Vuvuzela Oyee!!

    Mdau N. America

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 01, 2010

    swadakta mtunzi! umeongea kweli tupu! ujana haushikiki! binafsi kila nikiufikiria uzee nahisi kuchanganyikiwa! uzee kuukubali c kazi rahisi! lkn hatuna budi kwani haubishi hodi! nilazima ukuingie upende usipende!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 01, 2010

    Shair zuri tena limetulia mhh jamani uzee kila mtu anauogopa.ankal jamaa anapatikana wapi huyumwambie atutungie shairi la libeneke.vuvuzela oyee

    Yabinty

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 01, 2010

    Ni shairi zuri linalotukumbusha tunakotoka na tunakokwenda. Ukiweza kufikia uzee ni kweli mshukuru Mungu. Ni kweli usemavyo Mwanakijiji uzee ni kitu adimu. Nami nakusalimu kwa miaka 58 niliyofikisha karibu mgeni wangu uzee.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 01, 2010

    Superb! - Bonge la shairi.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 01, 2010

    Haya mashairi ndio wasanii wetu wanatakiwa waimbe kuwahamasisha watu wakubaliane na uzee, maana siku hizi bana watu hawataki kabisa uzee, hadi kwenye mavazi utakuta mmama mtu mzima kabisa lakini anapiga kimini nywele sijui zimepakwa rangi nyekundu kama yondo sister lol! ukiangalia uso unachungulia mboga iliyochacha hivyo vipedo vyake na vibukta hakuvivaa ujana wake huko, mambo ya kuiga wazungu tu sisi hatuna utamaduni huo heshimu watoto wako na vibabu kwenda disco na vibinti vidogo kama watoto wao lol! mtu mzima hovyoooooooooooo!! Mithupu rusha hiyo.

    Mdau wa Vuvuzela

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 01, 2010

    Wee Anon unaekandia WAZEE-FULL-KUJIACHIA.....KOMA KABISA......kila mtu ana hiari ya kuvaa anachokipenda.....KOMA KABISA....tena naona umesindilia kashwa zako zaidi kwa wakina mama.....BABA TUACHE TUZEEKE KWA RAHA ZETU.....nani avae gauni usawa huu.....kama mifweza ipo kwanini nijizeeshe bwana....I AM A PRETY YOUNG LADY IN MY LOVELY 50 YEARS OF AGE........HABARI NDIYO HII....................

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 01, 2010

    I agree with ano:3:15PM. Age is just a number dear. if you can handle it show it. uzee hauna maana kujiachia na kujionea huruma. Kama vitu vinatinga then viweke!!! these days 40s is the new 20s and 50s new 25s. Hey
    Go GIRL. I am in my 30s but trust me come see me in my 70s if GOD WILLING! NITAVIWEKA AS USUAL!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...