Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Batilda Burian akizungumza na washiriki wa mkutano wa Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Tanganyika wakati wa ufunguzi (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine amesisitiza uimarishaji ushirikiano katika kuhifadhi na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira ya ziwa Tanganyika kwa nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Tanzania, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia. Washiriki wa mkutano wa Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Tanganyika wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Batilda Burian (wa tatu kutoka kushoto, mbele) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.

Na Aron Msigwa

Imeelezwa kuwa ziwa Tanganyika linakabiliwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa kina cha maji kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wakazi wanaoishi kuzunguka ziwa hilo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Tanganyika ulioanzishwa miaka 10 iliyopita leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Batilda Burian amesema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika katika kuyanusuru mazingira ya Ziwa hilo.

Amesema hali ya kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kandokando ya Ziwa Tanganyika zikiwemo uchimbaji wa madini, Kilimo, uvuvi haramu na ongezeko la taka, sumu za viwandani na maji machafu kutoka majumbani yanayoelekezwa ziwani inachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa maji katika ziwa hilo .

Ameendelea kufafanua kuwa hali ya kuongezeka kwa joto, ongezeko la tope katika ziwa hilo na hali ya kupungua kwa kina cha maji kwa takribani mita 2.5 ni miongoni mwa changamoto ambazo zinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi kupitia wadau mbalimbali na nchi zote ambazo zinatumia maji ya ziwa hilo.

“Hivi sasa kina cha maji katika ziwa Tanganyika kinaendelea kupungua katika maeneo ya ziwa hilo hasa eneo la manispaa ya Kigoma ujiji ambalo Mr. Stanley na Dkt. Livingstone walikutana miaka 140 iliyopita kingo za ziwa Tanganyika zilianzia pale lakini hivi sasa ziwa Tanganyika limesogea kwa umbali wa mita 700 kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika eneo hilo” amebainisha.

Dkt. Burian amefafanua kuwa hivi sasa kuna juhudi mbalimbali zinazoendelea katika kuhifadhi Mazingira ya ziwa Tanganyika hasa kupitia mradi huo ambapo wadau mazingira kutoka Tanzania na nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia wanaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabia nchi katika ziwa Tanganyika.

Ameongeza kuwa serikali kwa kuzingatia umuhimu wa ziwa hilo duniani na uhifadhi wa aina 700 ya viumbe wanaopatikana katika ziwa hilo inaendelea kushirikiana na wanasayansi na watafiti mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kupata taarifa za kisayansi za mabadiliko ya ziwa Tanganyika na hivyo kuandaa mkakati wa kukabiliana nazo.

Pia amesema serikali inaendelea kutekeleza na kuandaa mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti, uanzishaji wa miradi ya uvuvi na ukaushaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya jua, uanzishaji wa mradi wa usafishaji wa maji machafu yanayoingia ziwani na utoaji wa tope katika ziwa hilo.

Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo kikuu Huria cha Tanzania Prof. Tolly Mbwete mshiriki wa mkutano amesema ushiriki wake katika mkutano huo unaowashirikisha wadau wa sekta mbalimbali ni moja ya juhudi za uimarishaji wa mkakati wa utunzaji wa mazingira katika ziwa Tanganyika.

“ Sasa tutaweza kuimarisha tafiti zetu kwa wanachuo ambao wanaishi mazingira ya ziwa Tanganyika na pia kuwa tayari kutoa mchango katika uhifadhi wa mazingira na kufanya tafiti zitakazowasaidia wakazi wa mikoa hiyo” amesema.

Kufanyika kwa mkutano huo unaolenga uboreshaji wa Uhifadhi Endelevu wa ziwa Tanganyika jijini Dar es salaam ni matokeo ya mkutano wa kamati ya uhifadhi wa mazingira na viumbe wanaopatikana katika ziwa Tanganyika uliofanyika mjini Nairobi mwaka 2000.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hizo nyumba zilizoezekwa kwa nyasi zingehimizwa huko vijijini!

    Nyumba inaweza kuwa ya tembe...lakini iwe na madirisha!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...