Meneja wa Oiko Credit Tanzania Deus Manyenye (Kushoto) akimkabidhi mfano ya hundi yenye thamani ya milioni 500/- Mwenyekiti wa YWCA Moshi, Valentine Mwinga fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo kwa ajili ya ukarabati wa jengo la chama hicho lililokaa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo. Wakati wa hafla hiyo taasisi hiyo pia ilikabidhi hundi yenye thamani ya bilioni 1.6/- kwa Saccos ya Wazalendo ili kusaidia kuwawezesha watu wa hali ya chini. Katikati ni Katibu wa chama hicho, Frida Mbowe.
Meneja wa Oiko Credit Tanzania Deus Manyenye akisisitiza jambo kwa Mhasibu wa YWCA Moshi, Haidan Shayo na Dk Henry Nyamubi ambao ni wanachama wa chama cha watu wenye ulemavu kutokana na uti wa mgongo mara baada ya hafla ya kukabidhi hundi kwa zenye thamani ya bilioni 2.1/- kwa YWCA Moshi na Saccos ya Wazalendo zote za mjini humo.
Katibu wa YWCA Moshi, Frida Mbowe akitoa ufafanuzi wa ukarabati wa jengo kwa Meneja wa Oiko Credit Tanzania Deus Manyenye (mwenye suti) mara baada ya hafla ya makabidhiano hundi yenye thamani ya milioni 500/- fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo kwa ajili ya ukarabati wa jengo la chama hicho lililokaa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo. Wakati wa hafla hiyo taasisi hiyo pia ilikabidhi hundi yenye thamani ya bilioni 1.6/- kwa Saccos ya Wazalendo ili kusaidia kuwawezesha watu wa hali ya chini. Katikati ni Katibu wa chama hicho, Frida Mbowe.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

KAMPUNI ya OIKO Credit inayojishughulisha na ukopeshaji fedha kwa taasisi mbalimbali duniani zikiwemo benki, imezikopesha jumla ya shilingi bilioni 2.1/- YWCA Moshi na Saccos ya Wazalendo ili zitumike kuiwezesha jamii ya watu wa kipato cha chini.

Fedha hizo zinazotumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la makao makuu ya YWCA Moshi na uwezeshaji jamii ili ijiendeleze kimaisha kupitia Wazalendo ni muendelezo wa mikopo kutoka kampuni hiyo iliyoitoa katika kipindi cha mwaka huu kwa taasisi 12 nchini unaofikia jumla ya bilioni 8.2/-

Akizungumza jana mjini hapa wakati wa hafla ya kukabidhi hundi Meneja wa Oiko Credit Tanzania Deus Manyeye alisema kuwa lengo la kampuni yake ni kuwekeza kwenye taasisi za fedha zilizolenga kuiendeleza jamii ya kipato cha chini duniani.

Akifafanua Manyeye alibainisha kwamba licha ya kupokea maombi mengi lakini wamehakikisha fedha wanazotoa zinaelekezwa kwenda kusaidia miradi ya uzalishaji inayolenga watu wa hali duni wanaopigania kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

“Tulichunguza na kubaini kwamba YWCA Moshi na Wazalendo Saccos wamekidhi vigezo vya kupewa mikopo kwani walikuwa na nia ya dhati ya kuikomboa jamii ya chini kutoka kwenye umaskini unaoikabili. Tayari fedha zimeshaanza kutumika kama mnavyoona ukarabati wa jengo hili unavyoendelea,” alisema Manyeye.

Aidha kwa kuwa idadi ya watu Tanzania ni kubwa kuliko ile ya Kenya na Uganda taasisi hiyo imepanga kuziwezesha kwa kuzikopesha zaidi asasi na wadau wa nchini ili waweze kuhudumia kundi kubwa la watu kuliko ilivyo sasa ambapo nchi hizo zimekuwa zikipata fungu kubwa la fedha.

Kwa upande wake Katibu wa YWCA, Frida Mbowe alisema kwamba kwa kuwa manispaa hiyo inajiandaa kuwa hadhi ya jiji mkopo huo wa milioni 500/- utawawezesha kukarabati jengo kuwa lenye muundo wa kisasa utakaotoa mvuto kwa wawekezaji kupangisha na kufungua ofisi mbalimbali.

Naye Mbonea Maghimbi ambaye ni mwenyekiti wa Wazalendo aliishukuru Oiko Credit kuwakopesha bilioni 1.6/- na kusema watazitumia kama ilivyokusudiwa kwa kuwawezesha watu wa kipato cha chini kuweza kuinua hali yao kimaisha.

“Mbali na hilo pia tumepanga kuzitumia fedha hizo kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuhifadhi ama kujiunga na Saccos ya Wazalendo na faida mbalimbali watakazonufaika nazo mara watakapotimiza vigezo,” alisema Maghimbi.

Tangu Oiko Credit yenye makao makuu yake nchini Uholanzi ilipoanzishwa nchini mwaka 2006 imejiongezea wateja kutoka sekta mbalimbali ikiwemo benki, SME’s, Saccos, Makanisa na kuwekeza kutoka milioni 260/- hadi kufikia bilioni 16 Juni mwaka huu kutoka wateja wawili hadi 21.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...