Gharama ya kura yangu

Ndugu Watanzania. Mwaka huu wa-Tanzania tumepata tena nafasi ya kufanya maamuzi magumu nchini mwetu, maamuzi ya kuchagua viongozi watakaokuwa na majukumu ya kutuendeleza kama Taifa.

Ninaamini swala la uchaguzi ni zito na muhimu sana na kila mmoja wetu ana wajibu mkubwa wa kuwa makini kwa sababu uzembe katika kupiga kura huzaa uongozi wa kibabaishaji na ni ndoto za alinacha kutegemea viongozi wabovu, wapenda rushwa na wasio na sifa kuleta mabadiliko yoyote.

Natambua kila mmoja wetu ana vigezo vyake vya nani atakayempa kura zake, nimeona niwaeleze vigezo vyangu ili tuweze kubadilishana mawazo.

Urais:
Anayekubali midahalo; Ninaamini Rais anayenifaa ni yule amabaye anaelewa matatizo ya kitaifa na mwenye upeo wa kuelewa nini kifanyike katika kukabiliana na matatizo hayo. Ili niweze kumtathmini na kumpima na wagombea wengine lazima awe tayari kuingia kwenye midahalo ili nikiwa kama mpiga kura nipate nafasi ya kumhoji. Siko tayari kumpigia kura mgombea anayefanya kampeni kama tape recorder, yaani anakuja jukwaani kusema anayotaka yeye tu na kuondoka.

Elimu ya Bure; hakuna taifa linaloweza kuwa na mategemeo ya maendeleo bila ya kuwaelimisha wananchi wake. Tanzania ya leo inakabiliwa na tatizo la masikini kuendelea kuwa masikini na matajiri wanazifi kuwa matajiri, njia muhimu ya kuwakomboa walio wengi ni kuwapa elimu yenye manufaa wananchi wote. Siko tayari kukubali hoja ya kwamba haiwezekani, nataka kiongozi ambaye anathubutu kubana matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali kama magari ya fahari ili elimu ipatikane.

Uwajibikaji kifedha; Nataka Rais ambaye hawachekei wahalifu wenye tabia ya kudokoadokoa fedha za umma. Fedha za umma zitumike kwa kile kilichokusudiwa tu na kwa kufuata taratibu zilizopo . Nimechoka kusikia ripoti za kitaalamu zinazothibitisha wizi na Rais hawaagizi wasaidizi wake kuwapeleka wahusika kwenye vyombo vya sheria. Matatizo yetu mengi yangeweza kupungua endapo matumizi ya fedha za umma yangeboreshwa.

Serikali iliyo wazi; nimechoshwa na tabia ya kuendesha kazi za Kiserikali kisiri kama kibaka anayekwenda kuiba usiku wa manane. Nakataka Rais atakayetuletea Sheria inayogusa maswala ya Open Records ambayo inamruhusu kila Mtanzania kupata taarifa zinazohusu maamuzi ya Serikali. Kama Serikali imetoa zabuni kwa kampuni yoyote basi tuwe na nafasi ya kujua undani kama vile makampuni mangapi yaliomba tenda, vigezo gani vilitumika, etc. Kwa mikataba ambayo inaweza kuwa ya siri kama ya kiusalama nayo iwe monitored na kamati ya uchumi ya Bunge ili angalau tuwe na wabunge watakaotuwasilisha kudhitibi utoaji wa zabuni.

Uchumi na Biashara; Kabla ya uhuru tulikuwa ni wazalishaji wa malighafi kwa ajili ya mataifa makubwa, leo hii baada ya karibu miaka 50 bado tunafanya hayohayo. Nataka rais mwenye jibu ya kubadilisha Tanzania kutoka nchi inayozalisha malighafi na kuwa taifa linalozalisha bidhaa za viwango vya juu zilizokamilika.

Serikali na Bunge; Kuna haja ya kuwa na mapinduzi ya katiba. Katiba ina matatizo kadhaa, moja wapo ni hili ya wabunge kuwa mwaziri. Kwa mtizamo wangu hii ni conflict of interest kwa sababu haiwezekani wabunge wajidhibitu wenyewe, tunahitaji clear separation ya hizi nguzo mbili za dola. Mfumo wa sasa hauthamini fedha za walipa kodi, mfano sasa hivi mawaziri wako majimboni kwenye kampeni lakini Serikali inawalipa mamilioni ya mishahara. Wakirudi maofisini Serikalini hawaonekani majimboni mpaka wakati wa uchaguzi ujao wakati wanalipwa fedha kama wabunge. Hawa wanatafuna fedha za bure kwa kuwa haiwezekani wafanye kazi mbili zinazohitaji muda mwingi. Mfumo huu unatumaliza.

Kuimarisha mahakama; leo hii mahakama zetu zinakabiliwa na matatizo ya kdaji kutokana na ukata. Nataka Rais ambaye atahakikisha mahakama zetu zinapata bajeti ya kutosha ili wananchi wapate haki zao katika kipindi muafaka.

Katika nafasi ya Ubunge halikadhalika kura yangu itakwenda kwa Mbunge anayeunga mkono matakwa haya.

Je, wewe una masharti gani kwa anayetaka kura yako?

By US Blogger
Usblogger11@gmail.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 37 mpaka sasa

  1. I hope wat wote wangekua wanaona na kuchagua kiongozi kama wewe. We have a long way to go my brutha.

    Mimi kwa kuadd nataka katiba ibadilike pale raisi anapo waeua wakuu wa mikoa na wilaya. hiyo imepitwa na wakati sana kwa vile hao watu hawatafanya kazi kwa kutumikia umma bali kumridhisha rais. Wanajua lolote atakalosema watamsikiliza au kazi hamna.

    Pia raisi atakaye jali watoto ambao ni taifa la kesho. Irudishwe ile system ya kuwapa watoto uji na matunda saa nne. Watoto hawawezi kusoma kama hawajala siku mbili. Raisi atakayekomesha child trafficking. Hii mambo ya kuzoa house girl kutoka morogoro na kuwatesa Dar ikemewe kabisa. Itafutwe njia bora ya kuwaajiri hao wafanyakazi wa ndani.

    ReplyDelete
  2. Kura yangu inaenda kwa kiongozi anayethamini nyumani kwake

    ReplyDelete
  3. Barack Obama alishinda uchaguzi wa marekani kwa njia ya midahalo alikuwa akijibu maswali kwa uhakika ccm kugoma kufanya mdahalo ni kuficha udhaifu wao hivyo wanatumia mwanya wa kuwa chama tawala kushinda uchaguzi

    ReplyDelete
  4. Transparency muhimu. Tunataka kujua mishahara ya watu wote wa serikali na anuani zao tuzione.

    Katiba ibadilike mbunge aishi kwenye jimbo lake. Wabunge wote wanaishi Dar siku hizi sijui huko walikochaguliwa watatumikia saa ngapi. Muda wao wote baada ya kura wanautumia kati ya Dar na Dodoma. That is not right...Utajuaje matatizo ya jimbo unalolitumikia kama unaishi Dar na kutwa unajishughulisha na miradi yako tu.

    Kwanza katiba ingesema kwa mika mitano unayotumikia usijihusihe na biashara yeyote...na mwenye moyo wa utuishi hilo sio tatizo kabisa....

    ReplyDelete
  5. great mtoa mada hiyo nzuri yaelekea ni msomi wa elimu ya juu,MUNGU IBARIKI TZ

    ReplyDelete
  6. Rais atakayebadilisha mfumo mzima wa kitawala wa nchi nzima. Haiwezekani kuona kuwa mkoa mmoja unaendesha nchi kwa kutoa GDP karibu 3/4 ya nchi nzima. Mgawanyiko huo unaifanya Tanzania kuwa mbili--ile ya "Dar" na ya mikoani.
    Rais ataebadilisha mfumo wa malipo na mishahara kwa wafanyakazi wake walipwe kulingana na kazi wanazofanya na sio semina na warsha zinazofanya nje ya vituo vyao vya kazi.
    Rais alietayari kupoteza umaarufu kwa kutoa maamuzi mazito kwa maslahi ya nchi wala sio yake binafsi.
    Rais alietayari kufukuza watumishi wote wavivu na kuweka wachapakazi bila kujali itikadi yao wala urafiki.

    kwa bahati mbaya huyu Rais ataendelea kubakia kama ndoto kwani asilimia kubwa ya watanzania ni wavivu wanaotaka pesa kwa njia ya mkato Sasa hizo kura atapewa na nani?

    ReplyDelete
  7. huyu naye kaibukia wapi? nilidhani na mwenzie nabii yohana mashaka walitokomea?

    ReplyDelete
  8. Aliyeleta mada hii anastahili kupata haki yake ya sifa ya ushupavu. Wengi wetu tunayajua hayo lakini tu kinachotumaliza ni "palpet" na hali hiyo inatufanya tuwe watumwa kifikra na kuona waliopo madarakani au chama kilichopo madarakani ndo hitimisho la ukamilifu wa kila kitu katika taifa.

    Bila kuwepo ushindani wa uongozi katika kuongoza nchi kwa vyama mbalimbali matatizo mengi hujitokeza na hivyo kuna kujenga tabia ya kulinda na hata kuwapigia debe la kurudi madarakani walio na tuhuma za ubadilifu wa mali ya uma au kutuma ovyo madaraka yao. Na kabisa kupichi cha lala salama awamu ya mwisho mtu anajikita zaidi katika kulinda maslahi binafsi badala ya mambo majukumu yenye manufaa kwa taifa.

    Lakini upinzani ukiwa mkali na hivyo walio madarakani watazidisha uadilifu kwa kuogopa kupoteza uongizi wa nchi kwa chama kingine.

    Tanzania ni wakati wetu kuamka sasa na kupanua wigo wa demokrasia bila kuangalia kiongozi bora anatoka wapi au chama gani ila mwenye kuonyesha uadilifu na uchungu wa nchi yetu na watu wake ndio nampa kura yangu.

    Mwaka huu sichagua sare bali nachagua sera. Mwaka huu naondokana na dhana ya kuchagua kati ya jembe na nyumba itikadi za miaka kadhaa iliyopita ila upeo wa hali ya juu katika kuendeleza taifa letu na wala si hadaa.

    Nakubaliana na mtoa mada hii yuko sahihi kabisa na nategemea wengi watamwunga mkono wenye uchungu na nchi yetu.
    Mungu ibariki Tanzania na watu wake.

    ReplyDelete
  9. TATIZO KUBWA LA AJIRA NI UCHU WA VIONGOZI KUKUMBATIA MADARAKA KADHAA PEKE YAO WAKATI WENGINE WANA NJAA YA AJIRA. WAZIRI NI MBUNGE NA PIA YUPO KWENYE JOPO LA BODI FULANI NA KADHALIKA, SASA NAFASI HIZO ZINGEGAWANYA KUSHIKA WATU WENGINE AJIRA INGEPANUA WIGO ZAIDI. MBUNGE AKISHATEULIWA KUWA WAZIRI BASI JIMBO LIBAKI WAZI NA MWINGINE AGOMBEE ILI AWAKILISHE KIKAMILIFU.

    PIA SERIKALI NI KUBWA MNO (big govenment) KWA MANTIKI KUWA NCHI MASKINI KAMA TANZANIA INA WIZARA NYINGI KULIKO MATAIFA MAKUBWA KAMA MAREKANI. MAANA YAKE BAADHI YA WIZARA NI ZIMEUNDWA KWA AJILI YA KUKIRIMIANA VINGINEVYO TUNGEANGALIA UMUHIMU KWANZA NA HALI YA KUBANA MATUMIZI YA SERIKALI SIDHANI KAMA TUNAHITAJI WIZARA ZAIDI YA 15. KUNA WIZARA ZENYE MANAIBU WAWILI NA MANAIBU MAKATIBU ZAIDI YA MMOJA.

    KAMA WIZARA ZITAPUNGUZWA, MAGARI YA ANASA SERIKALINI YAKIPUNGUZWA, SAFARI ZA WAKUBWA NJE NA NDANI YA NCHI ZIKIPUNGUZWA, NA KISHA ULIWAJI KOJI UFUATILIWE NA HATA KUBUNI ZAIDI MAENEO AMBAYO BADO YANAKWEPA KODI NINA HAKIKA ELIMU BURE KWA SHULE ZA AWALI HADI VIDATO NA PIA GHARAMA ZA HUDUMA ZA ZITAPUNGUA.

    KWA MFANO NDEGE YA RAIS INAPORUKA KWA SAA MOJA INATUMIA SH MILIONI 6, KAMA ATAPUNGUZA SAFARI ZA NDEGE KWA ASILIMIA 50 MAANA YAKE INAWEZA LIPA ROBO YA GHARAMA ZA ELIMU SHULE ZA AWALI NA SEKONDARI. JE KUPUNGUZA WIZARA, KUPUNGUZA SEMINA, KUPUNGUZA SAFARI NYINGINE ZISIZO ZA MUHIMU NA HIVYO KUOKOA OVER PAYMENTS BADO GHARAZA ZA AFYA NA ELIMU HAZIJAFUTWA?

    ReplyDelete
  10. Rais mpenda haki na mtunza heshima.
    Sheria iwe msumeno na haki itendeke na watu walindwe kiasi cha kutosha na haki zao zilindwe. Heshima ni kule kuheshimu watu, maslahi yao na kujiheshimu na kuheshimu kazi na cheo kwani cheo ni dhamana na sio kigezo cha kugandamiza na kupuuza wengine. Ni hayo tu kwa leo. Bado nchi iko nyuma sana.

    ReplyDelete
  11. Uchaguzi mwema. Tuanze lini kuambiana ukweli?

    ReplyDelete
  12. Nakubaliana na mdau asilimia 100%. Nahisi mgombea urais wa CCM anakimbia mdahalo kwa sababu zifuatazo
    (1) Anaogopa aibu na hajiamini. Haamini kwamba ana uwezo wa kuingia kwenye mdahalo na wasomi kama Dr. Slaa na Professor Lipumba bila kujiabisha kwa kuwa hana upeo unaotakiwa katika kutatua matatizo nchi iliyonayo
    (2) Kuna mambo mengi sana ambayo amayafanya visivyo au alitakiwa kuyafanya lakini hakuyafanya. kuna maswali kibao yanayohusu ufisadi, matumizi mabaya ya serikali e.t.c amabayo ana hakika akiwapa nafasi watu kumuuliza ataabika kwa kuwa hatakuwa na majibu yanayoridhisha au hana majibu kabisa
    (3)Anajivunia kulifanyia taifa mambo mengi ambayo akiwapa nafasi watu kumhoji vizuri ukweli utaonekana. kwa mfano. Mimi binafsi naamini mambo mengi ambayo anadai ameyafanya yangeweza kufanyika bila hata raisi kuwepo kwa sababu sio mambo amabayo yanahitaji mkakati usio wa kawaida (any special iniative). serikali yeyote yenye wafanyakazi wanaoenda kazini saa mbili na kutoka saa tisa na nusu ingeweza kufanya mambo hayo

    Mdau

    ReplyDelete
  13. HAYO MENGINE LABDA UKO SAHIHI, LAKINI KWA HILI LA ELIMU SIKUBALIANI NA WEWE, NCHI PEKEE ILIYOKUWA INATOA ELIMU YA BURE NI UJERUMANI AMBAO SASA PIA IMEFUTWA. KWA NCHI MASIKINI KAMA SISI ELIMU YA BURE ITAKUWA DUNI KAMA SIO MBOVU

    ReplyDelete
  14. Nafurahi watanzania tunaamka japo kwa kujisusua, ila naamini iko siku tutaacha uvivu,mazoea na unafiki.

    ReplyDelete
  15. Kama hakuna mwenye hizo sifa ulizotaja tusipige kura?
    Sijasikia hata mmoja kaongelea hizo sifa unazotaka.
    Urais si mdahalo,bali ni kufanya kazi tu.
    Kama ingekuwa kuongea sana ndio uongozi bora basi tuchague viongozi wa dini,walimu na waandishi wa habari.
    Mtu unalilia mdahalo hivi mpaka leo hatujajifunza tu blah blah za wanasiasa. kama huamini angalia midahalo ya wabunge inayoendeshwa na vituo vyetu vya Television.Mgombea anasimama anasema mkinichagua kati ya milioni 12 za mshahara wangu,nitachukua milioni 2 tu.nyingine nitawagawia wanannchi.Halafu watu wanashangilia kweli kweli.
    Hatuwezi kuishi kwa ndoto za ABUNUASI.Tusipende kushangilia kila neno tamu la mwanasiasa tutaumia jamani.Tusichezee miaka mitano.

    ReplyDelete
  16. tumeichezea nchi yetu Tanzania kwa mda mrefu kwa kweli tuchaguwe rais anayetufaa nasiwengine niwagombea wa vyama vya upinzani nadhani Dr W. SLAA anafaa

    ReplyDelete
  17. Tatizo letu ni ushabiki,wengi wetu tumekuwa washabiki tu kuamini kwa kila kinachotamkwa na mwanasiasa anayempenda.
    Na hili ndilo linatukwamisha.Hata alienzisha mada hii ni mshabiki vile vile.Katika uandishi wake kaonesha yuko upande gani?Ana akili sana kwani amecheza na hadhira.Ili upongezwe kwa mada yako ni lazima uoneshe upande fulani la sivyo utatukanwa na hilo ni tatizo.Kwani hivi sasa tupo tayari kuchagua mtu kwa mapenzi tu hata akionge pumba tutapia makofi,hata akifanya ujinga katika jamii tutatetea kwa nguvu zote.
    Ntakayempigia kura nimjua tarehe 30 baada ya kufanya uchambuzi wa kina kwa kufuata vigezo vyangu na si kwa kufuata kupigiwa makofi na watu kwani wapiga makofi wengine ni washabiki tu.

    ReplyDelete
  18. Wewe wacha hizo propaganda zako za kuishabikia Chadema. Huko uliko ni matajiri kuliko sisi je ulisoma buree? Na sasa wanaongeza ada za vyuo vikuu na hiyo nayo ni bure?

    Hakuna cha bure duniani na hata ada wanayolipa secondary ni ndogo sana, shule za msingi hawalipi kitu na michango ilifutwa, lakini mzazi popte pale duniani ananunua uniforms, na sehemu nyingine madaftari na kalamu.

    Niambie kuhusu shule za private zitafutwa au kufungiwa? Na wamiliki wa hizo shule wataziendeshaje bila kutoza ada? Hizi ziko dunia nzima, kwa hiyo hapo hakuna cha elimu bure!

    Midahalo ni wastage wa time kwanza unataka umuulize mgombea urais wetu anakuhusu nini wakati wewe kisheria si MTZ uliukana uraia wa Tanzania ili ufaidi vya wazungu, sorry huwezi kupiga kura nchini mwetu subiri uchaguzi wa kwenu huko kwanza hutapata hata nafasi ya kutoa maoni wewe ni migrant na wenyeji wanachukia migrants UNATAMBA HUKU HUKU KWENYE BLOGU ZA WAMATUMBI WENZIO.

    Mwisho zile ndoto zako za kuja uwe waziri futa kabisa, kwa sababu mgombea wako hatapata urais! Endelea kubeba box salama!

    ReplyDelete
  19. yah, hii kweli kabisa. tunahitaji watu wa namna hii. tanzania ikikua kifikra kwanza, kutoka katika utumwa huu wa kimawazo na kuingia katika level nyingine, tofaoti na hii ya sasa, hapo tutafika mbali.
    kiongozi kama mtoa hoja aliyemtaja ndie hasa anayetakiwa kwa tanzania hii. urafiki wa kijinga eti kulinda maslahi ya watu wa karibu na kurinda hadhi ya mtu, si vizuri hata kidogo. tunahitaji kiongozi anayeweza kutoa maamuzi mazito. mf. jk alithubutu kuruhusu best ake lowasa atoke madarakani pamoja na kuvunja baraza zima la mawaziri na kulipangua na kuunda jipya.
    watu waitegemea kuuna kitu kipya kutoka timu hiyo mpya lakini wapi. mambo yalikuwa yale yale. sijui lakini kwa sasa itakuwaje, labda tutaona baada ya ridhaa ya watanzania kutoa nafasi kwa nani.
    mambo megi yanahitaji kutatuliwa na kupewa ufumbuzi wa kudumu, tukumbuke..."MAISHA SIO MAJARIBIO, NI UTEKEREEZAJI TUU" sijui kama nimepatia tafsiri hii, yaani..."LIFE IS NOT A RIHEASAL, ITS A PERFORMANCE"
    TUWE MAKINI NDUGU ZANGU, jukumu ni letu ss wenyewe, si viongozi. wao ni kama waelekezi na wawezeshaji tuu. ss watekerezaji.

    ReplyDelete
  20. AKILI NYINGI HUONDOA MAARIFA

    UMEJITAHIDI KUANDIKA KWA KIREFU LAKINI UMESAHAU KUTOA SIFA ZA YULE UNAEMTAKA AU KUMPIGIA DEBE.

    MAELEZO YOTE YAMEMLENGA A SITTING PRESIDENT AMBAPO KWA KIASI KIKUBWA NDIYE ULIEMNADI NA KUZIDI KUWA POPULAR.

    UNGEKUWA NA MAARIFA ZAIDI USINGEGUSA SIFA YEYOTE YA SITTING PRESIDENT NA BADALA YAKE UKAELEZA SIFA ZA YULE UNAEMTAKA TUMWELEWA.

    HADI LEO HII SIJASIKIA MTU AKIMNADI MGOMBEA MWINGINE YEYOTE KWA KIREFU ZAIDI YA JK.

    WENGI WA OPPOSITION HUMNADI JK KABLA YA KUMALIZA NDIYO WANASHTUKA NA KUANDIKA KAMSTARI KAMOJA KADOGO, SASA HAPO HATA HATUJAELEZWA KWANINI TUMCHAGUE HUYO ALIEANDIKWA KWA UFUPI.

    SASA HIVI JK MOTO, NA NDIYE MAARUFU ZAIDI KULIKO WAGOMBEA WENGINE

    ReplyDelete
  21. Kwa mawazo yako ni sawa kabisa. Ila nafikiri labda wewe na mimi tuntakiwa kuchangia katika kubadirisha mawazo pamoja na tabia mbaya za utendaji kazi. Mimi ninaona kura yangu itakwenda kwa raisi ambaye anaweza KUONYESHA UTENDAJI KAZI WAKE KAMA WA MAREHEMU SOKOINE! HAKUNA KUSEMA MENGI na kama ni mkutano ni dakika 15-30 na akiwa anasema yaliyoandikwa kusudi baadae aweze kuyafuatilia. Kwa maana hiyo nafikiri uamzi kutoa kura yangu unaeleweka.

    SASA BASI WEWE NA MIMI TUFANYE YAFUATAYO:
    1. KUTAFUTA njia ya kuwezesha umma hasa wananchi ambao hawana access ya mitandao ili waweze kuelewa kinachoendelea hapa nchini.
    OMBI LANGU NI je tufanye je wewe na mimi ili GAZETI LA MAWANAHALISI ALIPATE KILA MTANZANIA HASA KWA WALE AMBAO WAKO VIJIJIN!!!!

    MUNGU WABARIKI WOTE WANAOSEMA UKWELI.

    ReplyDelete
  22. Kwa kweli vigezo vyako vinagusa kona zote muhimu kabisa kama tungepata Viongozi ambao wanaweza kuleta hayo mapinduzi na nchi ikaendeshwa katika misingi ya haki na kweli Tanzania ingekuwa mbali sana, maana ni aibu kubwa kwa dunia hadi leo umaskini, na bado tupo kwenye kupanga mikakati tu, yaani umaskini unazungumziwa kwenye makaratasi tu na waheshima ambao wameshajishibia miaka na miaka. Jamani watanzania tunahitaji kubadilika na kutafuta mbinu mbadala ya kufanya mageuzi makubwa kwa nchi yetu.

    ReplyDelete
  23. Natamani Mada hii ingikuwa inaweza kuonekana na wapiga kura wote millioni 19, lakini bahati mbaya asilimia kubwa zaidi ya wapiga kura wako huko vijijini ambako hawajawahi hata kumuona rais wa nchi. Kiasi kwamba kuna kijiji kimefikiwa na mmoja wa wagombea urais na wamemuona ni kiongozi mzuri sana kwa sababu amefika kwa mara ya kwanza tangu uhuru kiasi kwamba wamefurahi mno na wameahidi kumpa kura zao hata hawana haja hata ya kusikia hizo mnazoziita sera. Mimi nafikiri njia ya kupata viongozi kwa kupigiwa kura siyo njia nzuri maana hata asiyeelewa kiswahili sawasawa anaruhusiwa kupiga kura matokeo yake anaangalia mgombea ambaye picha yake inatabasamu zuri anampigia huyo huyo. Kiasi kwamba tunapata viongozi wasio na upeo hata chembe.

    ReplyDelete
  24. KWA TANZANIA YA SASA MTU HUWEZI KUCHAGULIWA KUWA KIONGOZI MFANO HEAD PREFECT KATIKA SECONDARY AU RAISI KATIKA CHUO CHOCHOTE CHA ELIMU YA JUU BILA YA KUFANYA MIDAHALO HAPO HAKUNA UBISHI 100% KAMA UMESOMA SEC AU CHUO CHOCHOTE KILE IWEJE LEO NAFASI VYETI KAMA UBUNGE NA URAISI CCM WANAOGOPA?JE HAWAKUSOMA ELIMU YA KITANZANIA?TENA NI WATU MAARUFU,HAKIKA HII NI HISTORIA KATIKA UCHAGUZI MKUU NAAMINI 2015 MAMBO YATABADILIKA,MUNGU IBARIKI BLOG YA JAMII.

    ReplyDelete
  25. anony anayepinga suala la elimu bure tatizo nini?tanzania kila mwaka tunatoa wasomi kama 6000 hadi 8000 kwa mwaka je tutashindwa kusomesha watu kama hao,nini tofauti na ccm wameahidi maisha bora kwa kila mtanzania tupo milioni karibu 45 mbona hushangai ahadi kama hiyo ambayo iliahidiwa mwaka 2005 hadi sasa inatekelezwa?tusiwe washabiki wa bila kujaji mambo

    ReplyDelete
  26. watanzania huu ni wakati wa kuamka maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na malaika toka mbinguni ndio maana wanadamu tumepewa akili na uwezo wa kupamabanua mambo,mfano barabara ya dar mwanza toka mwaka 2005 kuna kipande kidogo tu cha manyoni - singida hakina lami leo hii ni miaka 5 imeshindikana kabisa kutengeza hivi hapo nani alaumiwe?lini patajengwa?

    ReplyDelete
  27. tunashukuru m/kiti unauma na kupulizia hii nzuri MUNGU ibariki blog ya jamii

    ReplyDelete
  28. tatizo watanzania ni mabingwa wa kulalamika vijiweni,maofisini na kwenye misiba kila mtu nchi hii bwana haina maendeleo wanasahau kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na wao kwani ndio wapiga kura,kupiga kura sio suala la maigizo inatakiwa watu wawe wana elimu ya uraia

    ReplyDelete
  29. mimi napendekeza jk atafute msomi mzuri anafahamu sera za ccm amuwakilishe kwenye mdahalo bila hivyo hii ya mwaka huu itaacha historia katika uchaguzi wa uraisi ,ben hakuwa maarufu ila alishiki kikamilifu midahalo yote

    ReplyDelete
  30. Midahalo baina ya wagombea inakuwa mizuri pale tu ambapo wagombea wote ni wapya badala ya watu wanavyodai sasa kufanya midahalo baina ya wagombea mmojawapo akiwa madarakani. JK atakuwa hajawatendea haki wagombea wenzie endapo atakubali kuingia nao katika mdahalo kwani atakuwa anaitetea serikali imefanya hiki na kile il hali wenzie watakuwa wanatoa ahadi tu, zingine zikiwa ngumu kutekelezeka.

    Aidha kwa kipindi Dr Slaa alichoanza kusikika toka livyokuwa Padre kanisani hadi Mbunge wa kuchaguliwa, ameonekana tayari kuwa ni mdini, mbinafsi na aliyetawaliwa na jazba. Dr Slaa amepitia njia zote alizowahi kupitia Mchungaji Kibwetere wa Uganda aliyewateketeza waumini wake ili kukwepa kudaiwa ahadi
    zisizotekelezeka alizowaahidi waumini wake. Je tumjaribu? si tunakuwa tunakwangua ujiti wa kiberiti pembezoni mwa pipa la mripuko?

    ReplyDelete
  31. Suala la kudai Mdahalo sasa sikubaliani nalo kwani tunakaribisha na kukubali kudanganywa, Madai kuwa JK anakimbia mdahalo ni kweli kabisa kwani anaokoa muda na kukwepa jambo lisilo na maana sana.

    Dr Slaa alikuwa chachu bungeni iliyopelekea kuibana serikali hadi kuwafikisha mafisadi mahakamani. Lakini je, hicho ni kigezo tosha cha yeye kumpa dhamana ya kuiongoza nchi?

    Dr Slaa ni msomi, lakini hajulikanwi na wengi, tabia za yeye kama Padre mstaafu kuzivumilia imani za wengine? Jazba? na mahusiano na watu wa jinsia tofauti na yake. Tayari hata kampeni hazijesha keshabeba mwanamke bila kuchunguza kuwa ameachika kihalali au la.

    ReplyDelete
  32. serikali ya tanzania haina dini ndio maana kule bungeni hakuna bajeti za kuendesha makanisa au misikiti ila dini ni haki ya mtu hivyo mtoa maoni hapo juu acha kumuhukumu dr slaa kuwa aliwahi kuwa padri ule ni wito na siyo lazima ndio maana alipoona wito wake umefikia kikomo akaacha je hilo ni kosa?

    ReplyDelete
  33. nasikitishwa sana na wote wanaopinga mdahalo kwani mdahalo si sawa tu na interviews hata kuomba kazi yoyote ya serikali ua public sector mbona unaitwa na kuulizwa maswali ya kazi unayoiomba inaniuma sana na kusikia uchungu kwa jinsi watanzania tunavyoiweka reheni nchi yetu,mimi binafsi kwangu siyo lazima kumchagua dr slaa tumchague hata pro lipumba basi yeye haogopi midahalo any time muulize maswali anataka kufanya nini kwa watanzania ana majibu ya uhakika

    ReplyDelete
  34. wewe mtoa maoni unayesema kuwa midahalo haina maana utakuwa na elimu ya darasa la 7 tu hujasoma sec wala chuo

    ReplyDelete
  35. Asante mtoa mada. Pia umefika wakati vyeo vya mkuu wa mkoa viwe ni vya kugombewa kama ubunge. hilo ni jambo ambalo inabidi tuige wenzetu Marekani, mkuu wa mkoa anatakiwa awe anagalau ni mtu anaetokea na ni mkazi wa eneo hilo hivo anaelewa fika mazingira na matatizo ya hapo mahala, alafu yeye akishachaguliwa na wananchi ndo achague wakuu wa wilaya ya mkoa wake. Vinginevyo hiki cheo kitabakia kuwa ni cha kishkaji ambacho raisi anagawa kwa washirka wake ambao mostly wameshindwa kwenye kazi zao sasa wanapewa favor! Ni muhimu sana hili likawepo ktk katiba.
    thanx.

    ReplyDelete
  36. Wengine hatuoni mgombea anayefaa wakati option zimekwisha. Kuna wagombea wawili tu. Kilichobaki ni kupiga Ana-Ana-Doo!

    Hii ndo njia tunayotumia shuleni wakati mtihani umefika shingoni.

    ReplyDelete
  37. Mtoto wa CoastOctober 09, 2010

    Gharama ya Kura yangu ni kuona Mpiga kura:-

    1. Ambaye kwa kutumia vigezo vyake, demokrasia aliyonayo na haki yake ya kikatiba anatokea siku ya kupiga kura na kupiga kura bila kumshinikiza mwingine au kuona uamuzi wa mwingine kuwa ni wa kivivu au kisaliti au usiofaa.

    2. Ambaye baada ya matokeo kutangazwa akubali kushirikiana na wengine (walioshinda au kushindwa) kuchapa kazi kwa uadilifu, kwa nguvu zake zote kwa akili zake zote katika nafasi yoyote aliyopo awe mkulima, mfanyakazi, mfanyabiashara, mwanafunzi pasi kusubili kuona MIUJIZA TOKA KWA MTU MMOJA AITWAYE DIWANI AU MBUGE AU RAIS.

    Hasilani siamini katu kuwa maendeleo yetu yataletwa na kiongozi mmoja au hata viongozi watatu tutakaowachagua tarehe 31 bali sisi wote!
    Tutafakari sote juu ya hili.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...