NA VERONICA KAZIMOTO – MAELEZO

Shirika la Bima la Taifa limefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 31.7 baada ya kuuza baadhi ya majengo yake na mali nyingine zisizoendana na biashara ikiwa ni hatua mojawapo ya kutimiza azma ya kuwa na mizania sahihi ya kifedha (balance sheet) inayoendana na mwongozo wa sheria mpya ya Bima nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mwenyekiti wa Bodi la Shirika la Bima la Taifa Balozi Charles Mutalemwa amesema baadhi ya fedha hizo zitatumika kulipa malimbikizo ya madai yote ya wateja ambapo jumla ya shilingi bilioni 28.6 zinatarajiwa kulipa madai hayo.

“Shirika linatarajia kuanza kulipa madai yaliyohakikiwa kuanzia mwishoni mwa mwezi huu kupitia katika matawi yetu ya nchi nzima,” Amesema Mutalemwa.

Mutalemwa amefafanua kuwa zoezi hili la ulipaji litafanyika kwa uwazi unaostahili kwa kutangaza orodha za wateja watakaolipwa katika tarehe mbalimbali ili kuepusha gharama na misongamano isiyo ya lazima.

Amesema malipo yatafanyika kwa njia ya hundi kwa ajili ya kulinda usalama wa wateja,ambapo hundi zitatumwa kwa wateja kupitia anwani zao zilizomo katika majalada yao ya Bima,au kupitia kwa mawakala wao.

Aidha mwenyekiti huyo amesema, mteja yeyote ambaye anwani yake itakuwa imebadilika anaombwa kuwasiliana na Tawi la Shirika lililo karibu naye ili kumbukumbu zake zirekebishwe mapema.

Wakati huo huo Balozi Mutalemwa amewashukuru wateja wote wa Bima na watanzania kwa ujumla kwa kuendelea kuwa na imani na Shirika hilo kwa kuendelea kukata Bima zao kwenye Shirika hilo licha ya matatizo yaliyolikumba kwa muda mrefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...