Viongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakijadiliana jambo, kabla ya kuanza mkutano wa kwanza wa wadau wa shirika hilo, leo katika ukumbi wa Simba, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (IACC) mjini Arusha. Kutoka kushoto ni Mkurugnezi wa Uendeshaji Crescentius Magori, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamnini wa Shirika hilo, Mh. Abuabakari Rajabu. Nyuma yao ni Mkuu wa Uhusiano na Huduma kwa wateja, Bi. Eunice Chiume

Wananchi wengi wameusifia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa hatua yake ya kusaidia juhudi za serikali kuondoa kero ya umeme ambayo unaosumbua nchi hivi sasa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na Globu ya Jamii, wananchi hao wamesema hatua ya NSSF ni ya kuigwa na mashirika mengine ya umma yenye uwezo na uzalendo wa kuendeleza nchi, na kwamba hilo ni moja ya majukumu yao.

Wameifagilia sana NSSF kwa mpango huo na ule wa ujenzi wa daraja la Kigamboni unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

"Hivi ndivyo shirika la umma linatakiwa liwe", amesema Bw. Mussa Mtulya, fundi viatu mtaa wa Samora jijni Dar. "Miradi ya maendeleo sio majumba ya ghorofa pekee na migari ya kifahari", alidakia mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Saratoga.

Mdau mwingine mkazi wa Ilala Mchikichini, Frank Noel, ameipa tano NSSF kwa mpango wake wa kuendeleza eneo la hapo kwao, ambapo nyumba karibu zote zitavunjwa na mafleti kujengwa badala yake.

"Unaambiwa ujenzi ukikamilika wakaazi walioko sasa watapewa kipaumbele kwa kukopeshwa fleti ya vyumba vitatu kwa mkopo nafuu wa kama shilingi milioni 20 hivi", aliongezea Noel.

Mpango wa kuzalisha umeme ulitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dk. Ramadhan Dau, jijini Arusha, ambapo amesema mchakato umeanza wa kuzalisha megwati 300 za umeme na kuziingiza katika grid ya taifa ifikapo Desemba mwaka huu, ili kusaidia kuondoa matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa sasa.


Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa, alisema tayari mfuko wake umeshateua mtaalamu mshauri kwa ajili ya kutekelezwa kwa mradi huo, ambao pia hakutaja gharama zake.

Hatua hiyo imekuja wakati nchi ikikabiliwa na matatizo ya umeme na kulilazimisha Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza mgawo mara kwa mara.

Dk. Dau alikuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa NSSF unaofanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi.
Aidha, Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza.

“Madhumuni ni kusambaza gesi inayozalishwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alisema Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na mradi huo.

Kuhusu wanachama wa mfuko huo, Dk. Dau alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wameongezeka kutoka 380,000 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka 2009/10 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 33. Alisema ifikapo Juni mwaka huu wanachama wanategemewa kufikia 518,410.

Kwa upande wa makusanyo, alisema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126.96 hadi Sh. bilioni 315.31 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 148. “Mategemeo yetu ni kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu,” alisema.

Akizungumzia uwekezaji, Dk. Dau alisema shirika limeendelea kuwekeza raslimali katika miradi ya muda mfupi na mrefu. Kutoka mwaka 2005/6 hadi 2009/10 uwekezaji wa Mfuko uliongezeka kutoka Sh. 424.89 bilioni hadi Sh. trilioni 1.03. Alisema uwekezaji huu umesaidia kuongeza ajira na kuboresha thamani ya shirika.

Kuhusu ulipaji wa mafao, alsema Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha pensheni kwa asilimia 52 ambapo kutokana na mabadiliko hayo kiwango cha chini cha pensheni kwa wastaafu kimeongezeka kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 80,000 kwa mwezi.

Katika hatua nyingine, Dk. Dau alisema tathmini inayoishia Juni 2009, imeonyesha kuwa NSSF inaweza kujiendesha, hata kama shirika litaacha kukusanya michango na bila kupata mapato yo yote kutoka katika vitega uchumi vyake, bado linaweza kuendelea kutoa mafao yote saba na kukidhi gharama za uendeshaji kwa muda wa miaka saba.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kazi na Ajira, Mh. Gaudensia Kabaka, aliipongeza NSSF kwa kujizatiti kuanza ujenzi wa daraja la Kigamboni na mipango ya kuzalisha megawati 300 za umeme na kuziweka katika gridi ya taifa pamoja na kusafirisha gesi asilia.

“Hii ni mipango mizuri na ni endelevu kwa ustawi na maendeleo ya taifa. Ujenzi wa daraja la Kigamboni ambao kwa muda mrefu wananchi walitarajia kuwa litajengwa sasa watapata faraja kusikia kuwa utaanza wakati wowote,” alisema.

“Kuhusu ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme ni jambo la muhimu zaidi na ni muafaka kwa uchumi wa taifa kwani upungufu wa umeme/kukatika mara kwa mara kwa umeme kunaathiri sana mitambo ya uzalishaji wa bidhaa viwandani, tija na ufanisi katika maofisi kupungua na hivyo kuleta athari kwa taifa,” alisema.

“Lakini athari kubwa zaidi ni ile ya kukimbiza vitega uchumi kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza wa ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha ajira kwa wananchi kukosekana,” alisema, na kuongeza:
“Jitihada hizi zinazofanyika na NSSF zitapunguza sana kama si kuondoa kabisa kero hizi.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Abubakar Rajabu, aliiomba serikali kutoa uamuzi wa kuukubalia mfuko huo kujenga majengo ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuokoa fedha za serikali kwa kupanga ofisi.

Kwa taarifa zaidi za NSSF
BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Ankal, nina suala moja naomba uniulizie huko NSSF. Jee wawekezaji halisi, wale wananchi wanokatwa kila mwezi katika mishahara yao na NSSF kwa ajili ya akiba ya uzeeni, wananufaika nini na biashara hii na bishara nyengine zinzofanywa na NSSF? Kwani rasilimali kubwa ya NSSF inapatikana ni makusanyo haya ya akiba ya uzeeni, na wananchi wengi wakistaafu wanalipwa kiasi kile kile alichoweka tu bila faida yeyote. Sasa faida inayopatikana kutokana na uwekezaji wake wa muda wa miaka 25 au 30, yeye mwenyewe hastahiki kigaiwa hata kidogo?
    Ahsante

    ReplyDelete
  2. Mil 20 kwa watu wa mchikichini watawezaje kuulipa?

    ReplyDelete
  3. Binafsi nafarijika sana na utendaji kazi wa Dr.Dau kwa kulisimamia vyema shirika (NSSF) katika kubuni, kupanga na kuendeleza miradi mbalimbali yenye kuleta tija katika taifa letu. Ni mtu mwenye kufanya maamuzi magumu wakati mwingi angalia hili la kuzalisha umeme,nilishawah kusoma maohajiano yake (kama sikosi uncle au blog ingine ilifanya mahojiano hayo), nakumbuka katika moja ya statement yake alisema kuwa "ukitaka kufanikiwa jaribu kuthubutu/kufanya uamuzi mgumu katika jambo ambalo unadhan lina maslahi kwa taifa".Na hiki Dr. Dau ndicho alichosema na silaha ya ushindi kwa NSSF, ambayo mara nyingi imekuwa ikipingwa pale inapotaka kuanzisha mradi fulani. Ama kwa hakika mashirika mengine ya umma yaige kutanguliza maslah ya taifa mbele kama lifanyavyo shirika la NSSF kwa kazi zake nzuri zinazooneka.

    Go Dr.Dau, go NSSF

    Mdau Belgium

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...