Mojawapo ya matangazo ya ziara ya Birmingham
nchini kwenye TV za Uingereza 

Ziara ya Birmingham City kuzuru Tanzania mwezi Julai kwa michezo kadhaa ya kirafiki iko katika hatihati, na endapo kama wenyeji wao Simba SC watashindwa kuthibitisha ratiba na malipo stahili kwa ziara hiyo ifikapo saa sita kamili mchana wa leo huenda ikaahirishwa, Globu ya Jamii inaweza kuthibitisha.



Habari za uhakika zilizotufikia kutoka London zinasema Birmingham City imemuandikia Mwenyekiti wa Simba SC, Mh. Alhaj Ismail Aden Rageh kwamba wamepatwa na wasiwasi baada ya Wekundu wa Msimbazi hao kuchelewa kutoa uhakika wa ratiba ya ziara kwa muda ulioafikiwa awali na pande hizo mbili.


Kwa mujibu wa barua hiyo toka kwa  Julia Shelton, Mkuu  wa Utawala wa Mpira wa Klabu hicho cha Premier League ya Uingereza, ambayo Globu ya Jamii inayo nakala yake, Birmingham imetishia kufuta kabisa ziara hiyo endapo kama mkataba wa ziara hiyo haujasainiwa na kufikishwa kwao ifikapo saa sita kamili za mchana leo  - yaani masaa matatu kuanzia sasa.

Katika barua hiyo Julia Shelton ametahadharisha pia kwamba tayari Birmingham wameishaingia gharama kibao za maandalizi ikiwa ni pamoja na kukodi ndege maalum kwa ajili ya ziara hiyo, chanjo kwa wachezaji iliyopangwa kufanyika Mei 23  pamoja na gharama zingine muhimu ambazo, amesisitiza huenda ‘zikaongelewa’ huko mbeleni.

Julia Shelton pia ameongelea athari za yatayojiri kwenye vyombo vya habari vya kimataifa zitapozungumzia kadhia hii kwa ubaya endapo kama mkataba huo haujasainiwa na ziara kutofanyika baada ya maandalizi makubwa.


Glolu ya Jamii imewasiliana na Mh. Rage asubuhi hii naye amethibitisha kwamba ziara hiyo ina hati hati kwani Simba hawatoweza kusaini mkataba huo kabla ya mechi yao na Wydad Casablanca iliyopangwa kuchezwa Cairo Mei 28, 2011 kwa kuhofia kwamba endapo watashinda hawatoweza kucheza na Birmingham kwani watakuwa na kibarua kingine cha Ligi ya Mabingwa Afrika.


Mechi  hiyo ya kutafuta timu itakayocheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Wydad Casablanca ya Morocco itachezwa Mei 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Petrosport jijini Cairo, Misri. 

Simba, ambayo ilishatolewa kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 6-3 na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imerudishwa tena kufuatia ushindi wa rufaa yake dhidi ya Mazembe baada ya mabingwa hao mara mbili wa Afrika kumtumia mchezaji Janvier Besala Bokungu bila kukamilisha taratibu za usajili. 

Baada ya kushinda rufaa hiyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likapanga mechi ya Simba na Casablanca ambayo nayo ilishatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho na Mazembe ichezwe mkondo mmoja uwanja huru, katika mechi  ambayo  ikiisha bila kufungana ndani ya dakika 90, mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penati.

“Kwa kweli nimesikitishwa sana kwa haya kujitokeza kwani tayari makampuni kibao yalishakubali kuwa wadhamini na wengine kama vile bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) walikuwa tayari kwenye Birmingham kutangaza vivutio vya utalii kwa mashabiki ambao wangeambatana na timu hiyo”, Mh. Rage ameiambia Globu ya Jamii.


Akaendelea:  “Wenzetu huwa wanataka kupata uhakika kwa ziara kama hiyo siku 60 kabla nasi kwa kusema kweli kusaini mkataba leo kabla ya saa sita inakuwa ngumu kwani kama tukipita katika mchezo na Wydad kule Cairo hiyo Mei 28 hatutoweza kuwakaribisha Birmingham City.


“Kinachonisikitisha zaidi sio sana mchezo wenyewe bali fursa kubwa ya kutangaza utalii wetu ambapo mashabiki 1000 walikuwa waje na timu, na tena waliomba wafikie hoteli za Kariakoo na sio katikati ya jiji ili wawe karibu zaidi na wenyeji.


"Awali mashabiki kama 5000 hivi walikuwa wanajiandaa kuja lakini tukasita kuwakubalia kwani idadi hiyo ni kubwa mno kwa sisi kuweza kuwa-accomodate katika jiji la Dar ingawa ingekuwa jambo safi sana kiutalii...

“Kesho nitakutana na waandishi wa habari na kutoa msimamo endapo kama ziara ya Birmingham itafanyika au la kwani hapa nilipo bado hatujatoa uamuzi kamili kwamba tusaini mkatana huo ama vipi maana muda bado...”






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Kutokana na gharama kuchangiwa na YANGA NA SIMBA hiyo ziara haitafanikiwa kwa sababu YANGA waliisha anza kukataa.
    Kuleta timu za ULAYA jamani ni kazi ngumu sana kwani wanahitaji kila kitu kiwe kabla ya miezi mitatu maana hawa wenzetu wanamipango au progamu za mwaka mzima kwa hiyo ili kuwa na uhakika ni lazima wapewe taarifa mapema.
    UIngereza ni dunia ya kwanza jamani na Tanzania ni dunia ya tatu kwa hiyo ziara hizi sasa hivi hazina faida kwanza Birmingham inakaribia kushuka daraja,kwa hiyo sio timu itakayo wafurahisha wananchi.
    Kiingilio kitakuwa bei sana kutokana na gharama za timu ya Birmingham na uwezo wa wabongo ni mdogo sana
    MUHIMU kuziharika timu kama MAN U ,ARSENAL AU CHELSEA SIO timu kama BIRMINGHAM ambayo ndugu zake ADEN RAGE wapo Birmingham wanaishi karibu na hiyo timu.
    MPIRA JAMANI NI BIASHARA KUBWA SANA AU MICHEZO KWA HIYO SISI TANZANIA TUCHANGAMKE TUSIWE TUNAANGALIA MPIRA WA ULAYA NA KUSEMA KWA NINI yanga au simba WASICHEZE KAMA MAN U AU BARSELONA,Jamani wenzetu wanaanza michezo wakiwa watoto na wanauwezo wa kugharamia mtoto kwenda kwenye mafunzo,kumnunulia mtoto vifaa vya michezo na serikali kama ya Uingereza inawalipa watoto pesa kila wiki kama SH 120,000 ZA KITANZANIA kwa hiyo ni rais kwa mtoto kuwa na vifaa vya michezo

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 20, 2011

    TATIZO USWAHILI MWINGI,WENZENU HAWATAKI LONGO LONGO....MNALETA MAMBO YA TANDIKA MKEKA LETE MAJI YA KUNAWA TULE...WENZENU WAMESHATOKA HUKOOO FUNGUKA ALAAA.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 20, 2011

    Hawa Birmingham City ni kampuni ya biashara. Kila wanachofanya ni lazima waingize faida au wasile hasara. Uwanja wao unaingiza watu 30,000 na kila mtu kiingilio cha chini ni £30. Kuna watu wameshalipa kwa msimu mzima. Sasa unapomwalika usitegemee akakwambia atakuja bure. Atataka umgharamie safari yote na malipo mengine zaidi. Timu nzima atakayo kuja nayo ni wachezaji 30 na viongozi 15. Usafiri wanataka business class, hotel ni 5 star. Pengine watataka walipwe £1 milioni. Usafiri ni £100,000, hoteli kwa siku 5 ni £25,000. Usafiri wa ndani £5000. Hizo kwa hesabu za haraka ni pound 1,130,000/=. Weka kiingilio cha chini Tsh30,000/=. Wakiingia watu 30,000 utapata Tsh900,000,000/=. Wathamini alau watoe Tsh2,000,000,000/= kwa hesabu za haraka haraka. Je Simba wataweza kupata hizo pesa? Mimi siko tayari kutoa Tsh30,000 kwenda kumuangalia Zigic au Danny.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 20, 2011

    Mimi kama mchumi siungi mkono timu kama hizo kuletwa Tz zinafilisi uchumi wa Tanzania. Hebu angalieni tuliialika Brazil tukawalipa mapesa kibao na bado wakatufunga. Kuna lolote tuliloimarisha kwenye timu yetu kwa kuwaleta hao? Juzi tumefungwa na Nchumbiji, tukafungwa tena nyumbani na Bafanabafana. Sas mnawaleta hao waingereza. Ni kuharibu tu pesa za nchi. Ndi maana pesa yetu inashuka thamani kila kukicha kwani importation inakuwa kubwa kuliko exportation na hatuchukui hatua za kukabiliana na hilo badala yake tunaendelea kuimport tuuuuuuuuu. Rage huna uchungu na nchi.

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 20, 2011

    Jamani mie naunga mkono huo mtembeleo wa timu toka Brazil, ulaya, Marekani, au pande zote duniani. Hizi timu zinaleta maendeleo kwetu haraka, mafundisho na kufungua milango kwa wachezaji wa bongo. Na mpaka sasa Nizar ni mchezaji wa Tanzania wa kulipwa na kuaminika kwa sababu Whitecaps walioona kipaji chake toka bongo. Bali naona viongozi wetu hawaelewi jinsi yakuongea na hizi timu. Hizi timu, hata Brazili zinaelewa Tanzania ni masikini, kwa hiyo inabidi wawaombe waje kucheza bule, kujitolea. Hizo timu kama tulivyoona gharama yake ni kubwa sana, lakini wenyewe wanaweza kujitolea kwani wanaelewa Africa ni bala masikini. Lakini viongozi wetu wanajipeleka kichwa kichwa tu,hawajui hata kuongea na hawa jamaa, matokeo yake ndiyo hayo.

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 20, 2011

    RAGE ACHA UHUNI ULIKIMBILIA HUKO UKIFIKIRIA UTAPATA KWA BEI YA CHEE... HAMTOSAINI SABABU HAMUWEZI KULIPA HELA WANAZOZITAKA, NA HAPO NDIO MJIFUNZE KUACHA KUKIMBILIA TIMU ZA EUROPE... ALIKENI AL HALY NDIO SAIZI YENU!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...