Na Mwandishi Maalum – Pemba

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amewahakikishia wananchi Kisiwani Pemba kuwa serikali itashughulikia kero zote za muungano na hatimaye suala hilo libaki kuwa historia.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kikazi hapa Pemba na viongozi wa chama, serikali na wananchi wa Micheweni na Kangagani mkoa wa Kaskazini Pemba Dk. Bilal amesema nia ya serikali ni kuona muungano unaimarika na kudumishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.

“Mimi kwa nafasi yangu ya Makamu wa Rais, na Waziri wetu hapa anayeshughulikia masuala ya muungano tutafanya kazi ya kuhakikisha kero za muungano zinakuwa historia. Tutafanya kazi kuhakikisha muungano unadumishwa na vyombo vya muungano vinanufaisha watu wa pande zote za muungano,” alisema Makamu wa Rais.

Aliwaambia wananchi hao kuwa suala la kudumisha muungano ni muhimu ukizingatia kwamba Watanzania waliotoka visiwani wanaendesha maisha yao katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na isitoshe katika ulimwengu wa sasa mataifa yanafanya juhudi ya kuungana.

“Muungano tutaudumisha,” alisisitiza na kuongeza “ukienda Arusha, Singida, Manyara, Mtwara, Lindi…ukienda kokote Tanzania Bara utawaona Watanzania waliotoka visiwani wanaendesha maisha yao. Huko Ulaya, nchi zipatazo 40 zimeunda Umoja wa Ulaya.”

Aidha aliwataka wananchi kisiwani humo kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais aliwataka wananchi Kisiwani Pemba kuongeza ari ya kuchangia katika miradi ya maendeleo.

Katika ziara hiyo Dk. Bilal aliweka mawe ya msingi ujenzi wa kituo cha afya Bagamoyo kilichoko Mtambwe katika wilaya ya Wete na ujenzi wa skuli ya msingi Wingwi Mapofu iliyoko Micheweni na kutoa jumla ya shilingi milioni 4 ambapo kati ya hizo shilingi milioni 3 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo cha afya na shilingi milioni moja kwa ajili ya skuli ya msingi Wingwi Mapofu.

Aidha alipata fursa ya kutembelea maskani ya CCM ya Mhe. Shamsi Vuai Nahodha, Shaame Shanta na kukagua ujenzi wa tawi la CCM la Majenzi ambako pia alichangia jumla ya shilingi milioni moja, shilingi 500,000 kwa ajili ya kusaidia maskani na 500,000 zilizobaki kusaidia ujenzi wa tawi la Majenzi.

Makamu wa Rais leo ataendelea na ziara yake hapa Pemba ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea kinu cha umeme kilichoko Wesha Tibirinzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 18, 2011

    Ni vema kuondoa kero za muungano. Ila Wazanzibara kuishi Zanzibar na Wazanzibari kuishi Bara sio kigezo cha muungano. Nadhani kuna watu wengi tu wa mataifa ya kigeni tusiokuwa na muungano nao wanaishi na kufanya shughuli zao Tanzania, kama ilivyo kwa watanzania kuishi na kufanya shughuli zao SA, Ulaya, na marekani!

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 18, 2011

    Wewe mtoa maoni wa kwanza una hoja nzuri tu..Ukiwa mwanasiasa lazima utawambia watu kama alivyofanya DR.BILAL..angekuwa anaongea kama mhadhiri wa mlimani pale angetumia lugha nyingine..Mimi kusema kweli muungano naupenda kama 'muungano'lakini hizo kero za muungano huwa ni zipi haswa??.Mara nyingi utasikia Serikali(viongozi) wanasema..kero za muungano...kero za muungano..Kuna kitabu zimeandikwa naweza kuzipata na kuzisoma au ni siri?

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...