
MWANARIADHA chipukizi anayezidi kuja juu kwa kasi, Mary Naali kutoka klabu ya Skytel ya Arusha jana aliibuka kidedea kwa upande wa wanawake katika mbio za Muungano Half Marathon zilizorindima jijini Dar es Salaam na kushirikisha wanariadha kadhaa nyota.
Mary alikamata nafasi ya kwanza katika mbio hizo zilizoanzia viwanja vya Karimjee na kupita barabara kadhaa za Jiji la Dar es Salaam, alitumia saa 1:13.33 na kufuatiwa na Polines Chacha wa Mara saa 1:14.17 na kufuatiwa na Jackline Sakilu JWTZ 1:15.37 huku Banuelia Brighton wa Moshi akikamata nafasi ya nne akitumia saa 1:16.39 huku nafasi ya tano ikienda kwa Anastazia Msandai wa klabu ya Hakika ya Arusha 1:16.40.
Kwa upande wa wanaume, Faustine Mussa wa JWTZ Arusha aliibuka kidedea akitumia saa 1:03.29 na kufuatiwa na Ezekiel Jafari wa JKT Arusha 1:03.30 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Rogath John wa Polisi 1:03.57 na kufuatiwa na Alphonce Felix kutoka Winning Spirit sekondari 1:04.08 huku nafasi ya tano ikienda kwa Samson Ramadhani wa JWTZ Arusha saa 1:04.18.
Mbio hizo ziliandaliwa na klabu ya Nyro Athletic chini ya Mkurugenzi wake, Sarah Ramadhani, ambaye alitoa hamasa kwa wahisani kuwekeza zaidi katika michezo mbalimbali, ikiwemo riadha, badala ya sika pekee pamoja na kuwashawishi vijana kuipenda michezo mingine pia.
Sarah, aliwataka vijana wa Kitanzania, wapende na kujituma katika michezo, kwa lengo la kujiimarisha zaidi na kujijengea majina, badala ya kutanguliza maslahi zaidi hali ambayo itasaidia kuwainua na hata kuzikaribia nchi nyingine kama nchi jirani ya Kenya.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, lengo la kuandaa mashindano hayo ni kufufua mchezo wa raidha nchini, pamoja na kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambako pia yatakuwa yakifanyika kila mwaka.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...