Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Bi.Vivian Shalua akisisitiza jambo wakati wa tathimini ya shindano la urembo la utalii iliyofanyika wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza hilo.Kulia kwake ni Muandaaji wa shindano hilo Bw.Gideon Chipungahelo na Mratibu Rajab Zubwa.
Rais wa Miss Utalii ambaye pia ni muandaaji wa Shindano la urembo la utalii,Bw.Chipungahelo akitoa maelezo kuhusu shindano lake kwenye kikao hicho cha tathimini.Kushoto kwake ni Bi.Shalua.
Afisa Kutoka Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Idara ya Utamaduni Bw.Michael Kagondela akitoa michango ya uboreshaji wa shindano la Miss Utalii kwenye kikao cha tathimini kilichofanyika wiki hii Ukumbi wa BASATA.
Baadhi ya waliokuwa washiriki wa shindano la Miss Utalii lililopita wakifuatilia kikao cha tathimini.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendesha kikao maalum cha kutathimini shindano la urembo la utalii (miss utalii) linalofanyika kila mwaka ambapo wito umetolewa kwa waandaaji wa shindano hilo kufuata kanuni na taratibu zilizopo.

Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika wiki hii kwenye Ukumbi wa BASATA,Mkurugenzi wa Idara ya ukuzaji Sanaa wa baraza hilo,Bi Vivian Shalua alisema kwamba,shindano la miss utalii limebeba utambulisho wa taifa hivyo waandaaji hawana budi kujipanga na kufanyia kazi mapungufu yote yanayokuwa yanajitokeza

“Kumekuwa na mapungufu mengi katika mfumo mzima wa uendeshaji wa shindano hili,kamati haionekani, mambo mengi yamekuwa yakifanyika kinyume cha makubaliano na maandishi yaliyopo.Hata mratibu wa shindano kutoka BASATA amekuwa hahusishwi katika masuala kadhaa” alisema Bi.Shalua wakati akitaja baadhi ya mapungufu yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka.

Aliongeza kwamba,katika kutangaza vivutio vya utalii shindano hilo limekuwa likijikita katika maeneo ambayo tayari yanafahamika na ya eneo moja tu badala ya kwenda katika vivutio mbalimbali vilivyo katika kanda tofauti hapa nchini na kutumia mavazi na ngoma kutoka makabila mbalimbali.

Awali wakitoa michango yao, pamoja na kupongeza wazo na uwepo wa shindano lenyewe, wajumbe kutoka kada mbalimbali ndani ya jamii walishauri kuangaliwa upya kwa mfumo wa uendeshaji wa shindano hilo ambapo walitaka majukumu ya kamati ya uendeshaji shindano hilo yawekwe wazi.

Aidha,walitaka maandalizi ya mapema ya shindano ikiwa ni pamoja na kutimiza kanuni na taratibu mbalimbali za kulifanya lifane na kuvutia watu wengi zaidi tofauti na lilivyo sasa ambapo limedunishwa kutokana na mfumo wake wa uendeshaji.

“Shindano la Miss Utalii ni kubwa sana kuliko yote,ndilo limebeba nembo ya kitaifa ni lazima kwanza litangazwe na lifahamike pia washiriki wasiandaliwe kwa ajili ya kuwakilisha shindano tu bali pia kuliwakilisha taifa” alisema Michael Kagondela ambaye ni Afisa Kutoka Wizara ya Habari,Vijana,utamaduni na Michezo idara ya Utamaduni.

Aliongeza kwamba,kumekuwa na dhana mgando miongoni mwa waandaaji wa mashindano ya urembo nchini ya kuwaandaa washiriki katika kuyawakilisha mashindano yao badala ya taifa zima hali ambayo imekuwa ikisababisha wafanye vibaya kutokana na kukosa uungwaji mkono miongoni mwa watanzania walio wengi.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mchakato wa kuyapitia na kuyapa taswira mpya mashindano ya urembo nchini ili yawe na mfumo wa uwazi katika uendeshaji na zaidi kufuata sheria,kanuni na taratibu zilizopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 02, 2011

    Ndugu Michuzi nina ushauri mdogo tu.
    Wakati mukiandika nakala au ikiwa mtu kataka kutumia nakala yake hapa angalieni lugha kidogo kama itakuwa na matatizo au haileti maana ya kile kitu basi bora kuirekebisha.
    Mfano kichwa cha habari cha hii habari iliyopo juu"BASATA YAIFUNDA MISS UTALII".
    Maana ya hicho kichwa cha habari ni kuwa BASATA WAMEIPIGA MISS UTALII. Mimi ninachoomba tu kujitahidi kukitumia kiswahili vizuri ili kisiharibike kwasababu vyombo vya habari ni chombo kimoja ambacho kinasaidia ukuzaji wa lugha katika jamii kwa kila njia.
    Mdau

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...