Waandamanaji London wakipinga dili hilo
Salam,

Desemba mwaka jana SFO (Serious Fraud Office) Uingereza iliiamuru  kampuni ya BAE Systems inayouza vifaa vya ulinzi ulimwenguni kulipa faini kama adhabu ya shughuli zake mbovu za kibiashara na serikali za Saudi Arabia na Tanzania. Mwezi Februari 2011 BAE ilikubali sharti ambalo ni kuilipa SFO paundi milioni 285 na serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni (shilingi 75.3 bilioni), kama pesa za kujisafisha uso; ikiwa ni kuueleza ulimwengu mzima kuwa kampuni hiyo tajiri yenye wafanyakazi laki moja duniani, ina maadili mema.
Toka tamko litokee imezuka migogoro kadhaa.

Bonde moja wamesimama wananchi Bongo wasioamini viongozi  kwamba wana malengo ya kutetea maslahi yao. Hapo hapo, BAE Systems imetoa kauli kwamba pesa  ziende kwenye mashirika ya fadhila( na NGO) Tanzania ambayo kawaida ni ya kigeni. Imedaiwa barua zimeandikwa na wananchi kuiomba BAE isiipe serikali pesa hizo.

Kilima kingine wamekaa wabunge na viongozi wa serikali wanaoamini huu ni ukoloni mambo leo. Kwamba nchi tajiri kuiamuru nchi changa namna ya kufanya mambo yake ni utumiaji mabavu kiuchumi.

Kihistoria baada ya Waafrika kutawaliwa miaka zaidi ya 60 tuliachwa maskini na wale waliojali maslahi ya raia waliondolewa na Wazungu, mathalan Patrice Lumumba wa Kongo alieuawa 1961 na nafasi yake kuchukuliwa na Joseph Mobutu. Toka Jenerali Mobutu alipochukua madaraka mwaka 1965  hadi leo Kongo-Zaire imeharibiwa kabisa.

Wapo waliomudu kama Mwalimu Nyerere aliyetetea Uafrika na kujenga amani Tanzania ambayo tunayo hadi leo.

Toka habari kuhusu Wabunge wanne kuja Uingereza kuzungumzia mtafaruku huu  chuki na hasira iliyoenea kutokana na ufisadi ni kama imewashwa; kidonda kimetoneshwa. Mhusika mmojawapo wa tukio la 1999,  Shailesh Vithlani ambaye inadaiwa alipewa hongo kutimiza dili, hajulikani aliko. Hata baada ya mahakama ya Uingereza chini ya Justice Bean kuamuru ashtakiwe bado bwana Vithlani yadaiwa anajificha Uswisi.

Balozi Uingereza, Mhe Peter Kallaghe (wa pili) alipowakaribisha Wabunge na ofisa wa mawasiliano kukutana na wanahabari. wanne kulia ni kiongozi wa msafara, Naibu Spika wa Bunge la Taifa, Mhe Job Ndungai.
Je, tutajuaje kwamba Wabunge wetu wanalo zuri moyoni, wanauliza wasomaji wengi mitandaoni? Je wahusika wengine katika dili hilo ambao bado wako serikalini wamefikia wapi? Je, tutaamini vipi kwamba mabilioni haya ya Waingereza yatatumiwa kusaidia elimu ya watoto wetu nchini, kama wanavyoahidi?

Hatuwezi kujua. Tunaloweza kulifanya ni kuamini. Kwa vipi?

Wakiongea katika Ubalozi wetu Uingereza mjini London, juma lililopita viongozi hao chini ya Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai walihimiza  kuwa wanafuatilia matokeo ya mahakama ya sheria Uingereza inayochunguza rushwa (SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo riba inaongezeka.

Kampuni ya BAE systems huuzia ulimwengu mzima silaha mbalimbali za ulinzi wa majini, ardhini na anga, pia vifaa vya kisasa  vya mawasiliano ya habari, umeme, usalama na teknolojia. Mwaka jana BAE systems ilipata faida ya paundi bilioni 22.4 (takribani shilingi trilioni 60).

Wabunge walikutana na “House of Lords” ambacho ni kitengo cha juu Bunge la Uingereza chenye usemi mzito nchi hii ya Malkia. Walikutana pia na Wabunge wenzao akiwemo Naibu Spika wa Bunge Lindsay Hoyle. Walitegemewa pia kukutana na maofisa wa kampuni ya BAE Systems Philip Bramwell na Lesley Collen.

Mbunge, John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Hesabu za Umma, aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika kujenga elimu,” alisema mwakilishi huyu wa Bariadi Mashariki.
Wabunge walionyesha nia ya kutaka kusafisha jina la Tanzania, kurekebisha jina la viongozi wetu na kuleta sura mpya ya mambo yanayoiharibu Afrika.

Walisisitiza na kuahidi kinaga ubaga kwamba pesa zitaendeleza elimu. Kauli yao ina maana macho yote yanawatazama na kuwategemea kama mashujaa wapya. Tusiwahukumu kabla hata ya kuanza.

Itakuwa vyema tukiikubali kauli yao kuwa wanadhamiria kutumia nafasi yao walioipatia kupitia kura za kidemokrasia kutenda la maana. Hakuna haja ya kumzomea mtu anayejaribu uzuri. Mwache kwanza amalize anachokidhamiria kabla ya kupiga kelele. La maana kwa sasa ni kuwatakia kheri maana kuna mawili. Nchi yetu kudharauliwa na wageni na  huduma mojawapo muhimu nchini, yaani elimu, kukidhiwa.
  
 Sasa hivi kweli tukibadilishana meza, tuseme Tanzania ndio tuwe na uwezo wa kufanya utapeli kwa kuwauzia rada Waingereza? Kisha  baadaye watushtukie kuwa tulifanya rafu?  Halafu sisi tuwaambie kuwa tutawalipa baadhi ya fedha kutumia NGOs zetu?  Je, tutakuwa salama? Je mnadhani Waingereza wataukubali usanii huo?

MGOGORO WA RADA ZA NDEGE BAINA SERIKALI NA BAE SYSTEM UNAWEZA KUWA CHANZO CHA UONGOZI BORA TANZANIA

Tafakari.

Asanteni,

Imeandikwa na Freddy Macha pamoja na URBAN PULSE 
wakishirikiana na Jestina George

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 28, 2011

    Fred, umeenda vizuri hapo mwanzo. But uliposema kwamba mambo yangegeuka na sisi ndo tungewatapeli waingereza umekosea. Ni mfano usio sahihi. Hii ni kwa kuwa waingereza hawakutuibia wala hawakua na nia ya kutuibia. Sana sana wengi wao walilalamika tulivyotaka kununua hiyo rada. Ni sisi watanzania, kupitia viongozi wetu serikalini, tuliojitapeli na kujiibia. Hivyo huo mfano wako hauna mantiki. Sasa mtu anaejiibia halafu anaambiwa ameejiibia na anaambiwa viongozi wake waliohusika kujiibia lakini hawawajibishi, na kama haitoshi wengi wao wako madarakani; mtu huyo huyo umletee kupitia viongozi haohao pesa alizojiibia. Hivi hiyo ni akili au matope!!! Kwa vile waingereza ndo walioshtukia, waliopeleleza na waliopigania mpaka chenji ikarudi wakati sisi tumelala usingizi wa pono basi waache wao ndo watugawie wanavyotaka wao. Tusitake kujifanya tumezinduka mwishoni!! Aftaol kama kujidhalilisha tumeshajidhalilisha sana kwa kujiibia na kutowajibika. Hii aibu tunayoogopa sahvi haifiki hata robo ya aibu tuliyojipa mwanzo. Ni mpaka hapo tutakapopata akili ya kuchagua viongozi wanaozingatia utawala bora.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 28, 2011

    Ndugu mwandishi tunakushukuru kwa mada yako. Katika kumalizia umesema tuwaamini serikali walipwe hizo pesa kwani hata ingekuwa ni kwa waingereza wasingekubali utapeli huo.

    Lakini sisi wananchi tungependa uelewe kwamba hata sisi tunauona utapeli huo lakini Je si afadhali utapeli ambao mwisho wa siku mnachodai kitaonekana kuliko utapeli wa viongozi wetu ambo mwisho wa siku hakuna kitakachoonekana. Ninachotaka uelewe ni kwamba hatuna imani na serikali yetu kwani hawana nia ya dhati ya kumaliza ufisadi unaoendelea nchini.

    Hebu jiulize swali kuna nini kinaendelea katika hiyo pesa? Kwa nini hao BAE waamue kukataa hizo pesa zikitumika kupitia serikali? Kinachoonekana ni kwamba hilo lilikuwa dili la serikali lilofanikishwa na Andrea Chenji. Kama ingekuwa serikali haihusiki Chenji si angeshachukuliwa hatua? Mbona yupo mitaani andunda? Jingine ni kwamba kwa nini waende kufuatilia mambo ya rushwa huko UK wakati aliyehusika yupo Tz. Kama wanaona hakuhusika basi wasifuatilie hiyo pesa kwani ilikuwa halali kununua rada kwa pesa hiyo.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 28, 2011

    Hawa jamaa wajiulize kwa nini watu wanatushuku kuwa hiyo hela haitaishia mifukoni mwa watu?

    Je wana plan gani na malengo gani tiyari ya kuhakikishia watu kuwa pesa itafikia walengwa? je kuna malengo yoyote ambayo yataweza kupimika kwa hatua moja moja na mafanikio kuweza kupimwa hatua kwa hatua bila kusuburi mwisho? mfano:

    1. Je hizo nyumba za walimu wanazozisema, wameshasema specifically ni shule ipi iliyoko wapi na itajengewa nyumba ngapi?
    2. Je wameshasema baada ya hizo pesa kuingia ni baada ya muda gani nyumba zitakuwa tayari? with specific milestones?
    3. Je wameshaweka utaratibu ni jinsi gani watagawa hizo cantracts za ujenzi? wameshaweka utaratibu wa kuchagua contractors kutokana na vigezo vya uwezo wao na records za contractors? au ni mambo yaleyale ya duka la stationary huko Texas kupewa contract ya kuleta umeme Tanzania?

    Ingekuwa jambo la maana na kututuliza wananchi kama wangekuwa na ka-plan ambacho kako transparent. Otherwise sababu zipo nyingi tu za kuwashuku...

    Najua it is popular kuwapaka wazungu kuwa wanatudharau nakadhalika je tushajiuliza dharau inatokea wapi? tushaweka mikakati ya kupambana na hizi dharau kwa vitendo? mfano viongozi waanze kuwajali wananchi na si kujilimbikizia mali tu ambazo ni za wananchi na si zao...

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 28, 2011

    Naona mnapotosha ukweli wa mambo kutaka kujisafisha na kujifanya tumedhulumiwa tumeibiwa wakati si kweli. Ukweli ni kwamba Tanzania haikulazimishwa kununua rada hiyo tuliandamana kupinga ununuzi wa rada hiyo lakini viongozi wetu ndio waliolazimisha inunuliwe kwasababu walishaweka maslahi yao. Kulikuwa na rada bora zaidi tena mpya na tena zenye bei nafuu zaidi wakaambiwa lakini wakan'gan'gania inununuliwe ile ya BAE kwasababu walishapanga bei wao wenyewe. Rada inauzwa milioni 12 wao wakasema tuuzieni milioni 30 ili hizo za juu mtuwekee kwenye akaunti zetu sasa hizi kelele za tumeibiwa na wazungu zinatoka wapi wakati watu walishagawana vijisenti na mpaka leo wako mtaani wanadunda. BAE watarudishaje Chenji kwa serikali wakati wahusika walishakula mgao mara ya kwanza...Tuwadai hawa kina vijisenti kwanza waturudushie chenji yetu halafu ndio tuwakamate wazungu..Wazungu wanaujua ukweli wakiwaambia mtabaki midomo wazi kwa hiyo bora BAE wasimamie hiyo sadaka na wala sio chenji..chenji watu walishachukua muda mrefu uliopita.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 28, 2011

    Me nimeipenda hiyo picha ya waandamanaji. Yaani mpaka wazungu wanaandamana kwa ajili yetu sisi tumekaa tu hatuna hata la kufanya!!! Kweli idumu amani ya nchi yetu...inaonyesha hatuna shida na hizo pesa. Ama watu wamechoka kwa kuwa imeshazoeleka kuwa kuibiwa ni jambo la kawaida kwa watz? Au nadhani tafakari ya kila moja ni kuwa tumeshazoea ahadi nyingi zisizotekelezeka ndio maana hakuna anae jishughulisha? Hivi hawa wabunge wapo huko kwa gharama za kwetu au za kwao?? Maana wasiwasi wangu ni kuwa isijetokea matumizi ya wabunge hawa yakakaribiana na kiasi cha fedha kinachodaiwa ati! Tusipoangalia pesa hizi zitarudi kwao tena kupitia hizo NGOs.....mmmh! this is Tz and sisi ndo waTz bana!!!!!

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 28, 2011

    Prof Haruna Lipumba alitwambia mapema kwamba Tunaibiwa lakini kutokana na serikali kuwa na Kiburi na kukataa kila kitu kinachosemwa na MTU MWEUSI wakaendelea na mchakato,wameambiwa wameibiwa ata awakushituka kusikia PESA Inatarudishwa ndio MACHO yanawatoka wanajua Watapata Chochote RUSHWA imewapofua Wanapata Akili ya Kufikiria Tuu wakisikia neno PESA hawana haja ya kusikia mwizi maana kwao PESA ndio muhimu Kwao ,iko Siku hii Nchi itapata WENYEWE

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 28, 2011

    That the dumbest article I have ever read, what are you trying to say? Let's take government words for it..and if it failed...then what? "I told you so". We all know people who are responsible for this mess in the first place are free up to this point, to name few Chenge, Mkapa, Shailesh Vithlani. Now you want to trust somebody else, because they said they will do the right thing. Even those who accused for corruption, claim they are innocent and before become leaders they been sworn to serve people of Tanzania and turn around they serve their personal interest. What make you think this time is going to be different...and mind that they know….. There are NO consequences for their action. They can squander that money, and walk on the street with smile on their faces. Come on man! do your homework and think rational before you come up in the stage with stupid article. Time for leadership trial is OVER, wake up Tanzanian....if not now then WHEN?

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 28, 2011

    Freddy Macha,

    Nadhani kukaa kwako Uingereza kunaanza kukupofua macho na hali halisi ya nyumbani......angalau hata waingereza wanasema watarudisha hizo fedha kwa kuzipa NGO,Je serikali yetu imechukua hatua gani kwa waliotufikisha hapo......Anagalia Waingereza wanaandamana.......lakini Chenge alichinjiwa Ng'ombe na kupokewa kama shujaa mkuu jimboni kwake...baada ya kujiuzulu kwa kulazimishwa kama mbunge......!

    Freddy unaijua serikali ya Tanzania wewe? Unajua ulaji ulio serikalini? Kukaa kwenye kikao kuna bahasha......kufungua tenda bahasha.......kukaa saa za ziada bahasha......Je unataka pesa hiyo ikirudi iliwe kwa jinsi hiyo?

    Unajua ni allowance kiasi gani zimetumika kumtuma Cheyo na ujumbe wake? Unajua posho za kujikimu ujumbe huo kuja Uingereza? Je Balozi wetu huko asingetosha kufikisha ujumbe huo? Hebu Freddy chukua likizo kidogo angalau uone jinsi gurudumu la utendaji wa serikali linavyozunguka.......!

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 28, 2011

    Kuna watu wanajaribu kulinganisha uwajibikaji wa uingereza na Tanzania.Tunajua kabisa kuwa BAE wanafanya blanda kwenya mikataba lakini BAE haiwakilishi uwajibikaji wa nchi ndio maana mnashangaa kuwa wananchi wao wanaandamana kwa ajili yetu.Ninaamini kwa kiwango cha demokrasia walichofikia hawawezi kuwa na watu wa kuongea blaa blaa kama huyo mtoa mada hapo juu. huyo macha amekaa uingereza miaka mingapi bado ana mawazo ya ujima.huu utanzani jambo linatokea halafu siku mbili tunasahau ndio gharama ya tunachokivuna kwa hao viongozi walalahoi wanaotaka kuishi kama hollywood wasiangalie background ya ufukara walikotoka.Hapa uingereza ni sheria mbele kwa mbele umekosea ni mbele ya sheria na nyinyi wabongo hao watu mnataka wawakosee mara ngapi? its a shame hata hao wabunge hawana aibu wanatunisha kifua kudai pesa ya wizi wanazidi kuporomoka kadri wanavyozidi kudai haki ya wizi.Tanzania imevunja rekodi ya usanii. NINGESHAURI TU WAACHI NGAZI SERIKALI IMEWASHINDA KWANI NCHI IMEFIKIA HATA HAKUNA MZUNGUMZAJI ANAYEWEZA KUKEMEA MAOVU.MIMI NAONA KAMA NDOTO ATI.Narudia waziri wa fedha aliwahi kudiriki kusema eti yuko tayari watanzania wale nyasi ila dege la rais linunuliwe sitasahau dhihaka hiyo mpaka basi.mungu mlaze mahali pema BABA YETU MPENDWA -BABA WA TAIFA.

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 29, 2011

    Mdau Freddy,
    Kwanza nikusahihishe katika mada yako - SFO sio mahakama ya sheria inayochunguza rushwa bali ni kitengo cha kuchunguza makosa ya jinai. Mahakama ndio iliyo amuru pesa pauni milioni 29 zirudishwe kwa watanzania.
    Sasa hivi sisi watanzania tunaongela hili swala kama vile tumezulumia ilihali ni baada ya uchunguzi mzuri wa SFO tumeweza kufikia hapa. Itakumbukwa pia waziri wa maendeleo ya kimataifa wa Uingereza Claire Short, alijiuzuru katika serikali ya Toni Blair maana alieleza wazi kwamba mbali na sisi watanzania kutohitaji rada hii, pia kulikua na harufu kubwa ya rushwa lakini ununuzi ukaendelea!
    Baada ya mambo yote haya, tunawezaje kuamini kuwa serikali hii hii inan'gan'gania kurudishiwa hizo pesa na kwamba watazitumia katika sekta ya elimu ilihali ni serikali hiyo hiyo walio tembeza wizi na ambao baadhi bado wandunda bungeni??

    Mdau, Geneva.

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 29, 2011

    Mnategemea nini kutoka kwa Macha kama sio ubabaishaji kwani anashindwa kujua kwamba ni mahakama ndiyo iliyoamua hivyo baada ya suala hilo kuripotiwa kwa SFO na wao kulifikisha mahakamani.Huna lolote la kutuambia unataka kuwapotosha watu kuhusu ukweli endelea na biashara yako kwa hili huna cha kutueleza kukaa kwako kote ulaya bado unashindwa hata kujua nini kinachoendelea,unaongea utumbo mtupu.

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 30, 2011

    Ina maana hamjui Kama Macha nae aweza kuwa na hisa Yake, ndio maana anajifanya bwege anafagilia wezi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...