![]() |
| Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wananchi wenye uwezo wameshauri kujenga mazoea ya kuwasaidia wenzao wanaoishi maisha duni ili nao waweze kupata nafasi ya kufurahia huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma ya elimu na afya.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua maonyesho ya mavazi yaliyoandaliwa na Lions Club kwa kushirikiana na wabunifu wa mavazi kwa ajili yakuchangisha fedha za kuzuia upofu na kusaidia kurudisha uwezo wa kuona katika ukumbi wa Kempinski jijini Dar es Salaama.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliendelea kusema kuwa juhudi za makusudi zinatakiwa ili utamaduni wa watu kujitolea uweze kujengwa katika maeneo mbalimbali ya jamii kama mashule na katika taasisi ili wanafunzi waweze kujihusisha na huduma za kijamii.
“Ikiwa kila Mtanzania mwenye uwezo atajitolea kusaidia walau mtu mmoja anayetoka katika familia duni hakutakuwa na mtoto ambaye atakosa elimu au mtu atakayekosa tiba kwa kukosa fedha za matibabu,”alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA alizishauri Taasisi zinazofanya kazi za huduma ya kujitolea ziwezi kujitangaza ili watu wenye moyo wa kujitolea waweze kujiunga nao na kuisaidia jamii inayowazunguka
Kwa upande wake Rais wa Lions Club Dar es Salaam Frank Goyaye alisema kuwa nia ya kuandaa onesho hilo ni kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kwa ajili ya kuzuia upofu na kusaidia kurudisha uwezo wa kuona kwa wananchi wenye matatizo ya macho na kuihimiza jamii ione umuhimu wa kutunza macho.
Naye kiongozi wa Club hiyo Saruti Shahi alisema kuwa kwa mwaka huu wanaprogramu ya kujenga jengo la wagonjwa wa macho katika mkoa wa Kigoma, jengo ambalo litakuwa nje ya Hospitali ya mkoa na katika jengo hilo kutakuwa na vifaa vilivyokamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 15 zilipatikana huku wadau mbalimbali wa maendeleo wakiahidi kuisaidia Club hiyo kwa hali na mali ili iweze kutimiza malengo yake.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...