Na Mohammed Mhina,Zanzibar.

Mtandao wa Polisi wanawake mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, leo umetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto na wazazi waliolazwa katika Hositali Kuu ya Mnazimmoja mjini humo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa, Mtandao huo umetoa vitu mbalimbali yakiwemo madaftari, kalamu, sabuni, juisi, pipi, biskuti pamoja na vitu vidogovidogo vya michezo kwa watoto.

Akizungumza wakati wa utoaji wa misaada hiyo, Mwenyekiti wa Mtandao huo ambaye pia ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Magharibi Zanzibar SP (Bi) Salma Khamis, amesema kuwa pamoja na kutoa misaada hiyo, kazi kubwa ya mtandao huo ni kusaidia kusukuma mbele kesi dhidi ya unyanyasaji wa wanawake na watoto.

Amesema kuwa mtandao huo pia umekuwa ukijihusisha na kutoa elimu kwa wananchi kujua haki zao na jinsi ya kupiga vita ukatili wanaofanywiwa wanawake na watoto hapa nchini.

Naye mmoja wa wauguzi kwenye Hospitali hiyo Bi. Fatma Saidi Bavuai, amesema kuwa kuna haja ya Majeshi na Vikosi vingine vya Ulinzi na Usalama hapa nchini kuiga mfano wa Mtandao wa Polisi Wanawake katika kutoa misaada kwa watu wasio na uwezo.

Amesema kuwa baadhi ya wagonjwa wanaofikishwa katika Hospitali mbalimbali hapa nchini, wengi wao hawana ndugu na mara nyingi wamekuwa wakiishi kwa kutegemea zaidi misaada kutoka kwa wahisani jambo ambalo linawawia vigumu kumudu maisha na ghalama za matibabu.

Hivyo amesema kama zitajitokeza taasisi na wadau wengine kutoa misaada kama hiyo itasaidia kupunguza machungu na ugumu wa maisha wakiwa hospitalini.

Wakati huo huo, imebainika kuwa zaidi ya watoto 80 waliochini ya umri wa mika mitano na sita, hufikishwa katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibara kutokana na majanga ya kuungua moto wakiwa chini ya uangalizi wa wazazi na walezi majumbuni mwao.

Akizungumza na Mtandao huo wakati wa kutoa misaada hospitali hapo, Muuguzi wa zamu kwenye wadi watoto waliopatwa mna ajali mbalimbali, Bi. Asha Khamis Abdallah, amesema ajali za watoto kuungua moto zimeongezeka sana visiwani humo ambapo kila siku watoto kati ya watatu na wanne hufikishwa katika Hospitali hiyo wakiwa wameungua vibaya kwa moto wakiwa wajumbani mwao.

Bi. Asha amesema kuwa tatizo la kuungua kwa watoto zimeongezeka sana na kwamba kama wazazi na walezi hawatakuwa makini na tahadhari na watoto wao wanaweza kufariki dunia ama kupata vilema vya kudumu kutokana na majanga ya moto.

Amesema kuwa mara nyingi watoto wanaoungua ni wale wenye umri wa kuanza miezi sita ama kufikia wakati wa kutambaa hadi miaka mitano na sita ambao mara nyingi wanakuwa chini ya uangalizi wa wazazi ama walezi wenye dhamana.

Amesema ingawa matukio hayo ni kama ajali, lakini ajali hizo ziangeweza kuepukika kama wazazi na walezi wenye dhamana wangekuwa makini katika kudhibiti nyendo za watoto hao ambao baadhi yao hufariki dunia na wengine kubaki na vilema vya kudumu.

Nao baadhi ya wazazi na walezi walikutwa wakiwauguza watoto hao wameelezea sababu mbalimbali zilizopelekea watoto hao kuungua moto.

Bi. Nuru Ali Simaye, amesema kuwa mtoto wake aliuungua baada ya kutumbukia kwenye sufuria ya supu iliyokuwa ikipikwa kwa biashara nje ya nyumba yao.

Bi Sharifa Iddi, amesema kuwa mtoto wake aliungua na chai baada ya kuchukua kikombe hicho akitaka kunywa hata kabla ya kutiwa sukari na ndipo kilipomponyoka na kumuunguza kifuani.

Na Bi. Fatma Ali salum, ambaye pia ni Mwalimu wa Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe “A” mjini Zanzibar amesema kuwa mtoto wake alijikwaa baada ya kujikwaa na kutumbukia kwenye maji ya chakula yaliopunguzwa na mpishi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...