Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi- Zanzibar


Serikali imewaonya vikali Maafisa na Askari Polisi wanaoendeleza vitendo vya kudai na kupokea rushwa hapa nchini na kuwataka wajiondoe wenyewe kwenye nafasi zao katika Jeshi hilo la sivyo watatolewa kwa nguvu kwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa onyo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Zanzibar Mh. Haji Omar Kheri, wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi Mdogo kwa Askari Polisi yaliyomalizika leo kwenye Chuo cha Polisi Zanzibar.

Akifunga mafunzo ya uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi ngazi ya Koplo, Sajenti na Sajin-meja, Mh. Kheri amesema pia kuwa hali ya kutowajibika kwa baadhi ya Askari na watendaji wengi wa serikali ni mambo yanayokwenda kinyume na utawala bora.

Amesema kutotenda ama kuchelewesha haki, kudai na kupokea rushwa na kutowajibika ama kutoa siri za wasiri wa Polisi wanaowataja wahalifu, ni mambo yanayoweza kupunguza imani ya Jeshi hilo mbele ya wananchi.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano zitahakikisha zinatafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili askari kama vile uchakavu wa vituo vya Polisi, ukosefu wa nyumba za kuishi pamoja na ukosefu wa vyombo vya usafiri na mawasiliano ili kuwawezesha kufanya kazi zao kikamilifu.

Akizungumzia mabadiliko ya hali ya uhalifu duniani, Mh. Kheri amesema kuwa mbinu mpya zimekuwa zikibuniwa na wahalifu katika kutekeleza matukio ya kihalifu na hivyo pasipo mafunzo zaidi kwa askari Polisi, haitawezekana kuwakabili kikamilifu.

Hata hivyo Mh. Kheri amepongeza utaratibu unaotumiwa na Jeshi la Polisi hapa nchini wa kutoa mafunzo kabla ya kuwapandisha vyeo wanaostahili na kusema kuwa utaratibu huo unawawezesha askari kukumbushwa wajibu wao wakiwa katika vyeo na madaraka yao mapya.

Hata hivyo Waziri Kheri amesema kuwa ni muhimu kwa kila askari kusaidia katika kuwaelimisha wananchi kufuata misingi ya utawala bora na pia Polisi waepuke kuibua malalamiko kwa kutowatendea haki walalamikaji wanapofika katika vituo vya Polisi jambo ambalo amesema ni kinyume na matarajio ya utawala bora.

Naye Kamishna wa Piolisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amesema kuwa kuanzishwa kwa mpango wa Utii wa Sheria pasipo Shuruti, kumeingizwa katika miradi ya Polisi Jamii na kupunguza matumizi ya nguvu katika ukamataji wa watuhumiwa.

Wakitoa tathimini ya mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar ACP Maulidi Mabakila na Mkufunzi Mkuu wa Chuo hicho SSP Andrew Mwang’onda wamesema kuwa washiriki wote wamefundishwa mambo mbalimbali yatakayoweza kuongeza tija kwa Jeshi la Polisi mbele ya wananchi.

Mkuu wa chuo hicho ACP Mabakila, amesema kuwa wahitimu hao wakiwa chuoni hapo wamepata mafunzo mbalimbali ya ndani na nje ya darasa kama vile kutembelea katika shehia mbalimbali kwa lengo la kujifunza utekelezaji wa Polisi jamii na Ulinzi shirikishi kwa vitendo wakiwa katika mabaraza ya kamati za Ulinzi na Usalama za Shehia husika.

Kwa upande wake Mkufunzi Mkuu wa Chuo hicho SSP Anderw Mwang’onda, amesema kuwa katika kufanikisha mafunzo hayo Chuo hicho kimewaalika wataalamu mbalimbali kutoka nje na ndani ya Zanzibar ili kutoa elimu itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao pindi warudipo vituo mwao.

Awali Waziri Kheri alikagua gwaride na kutunuku vyeti na zawadi ya virungu vya heshma kabla ya kuwavisha vyeo wahitimu waliofanya vizuri zaidi wakati wa mafunzo yao kabla ya gwaride kupita mbele yake kwa mwendo wa pole na wa haraka kwa kutoa heshima na baadaye kuona onyesho la judo na singe.

Jumla ya Askari 826 wakiwemo wa mafunzo ya koplo, sajenti na Sajin-meja wamehitimu mafunzo yao ya awamu ya pili chuo hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 28, 2011

    domo nyumba ya maneno!!! mfumo mzima wa polisi hapa zanzibar na tanzania kwa ujumla umeoza kabisa. Hapa zanzibar polisi, jeshi na hata uhamiaji wote wanatumia jezi yao (uniform) kunyanyasa wananchi. Viongozi wanajua na haswafanyi lolote. Ni kusema sema tu kila siku. Zanzibar mlala hoi hana haki, ni pesa tu inayozungumza. Siandiki mengi hapa ikaja kuwa michuzi akaweka kapuni au akaingia matatizoni.

    Ule msemo wa siti ambao mzee rukhsa aliutumia wa "zanzibar njema atakae aje" unafaa kubadilishwa kwa sasa uwe "zanzibar ya ajabu, njoo ujionee mwenyewe"

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 28, 2011

    Polisi wala Rushwa kukiona..hapa ndipo tunakubali kuwa vichaa wa mziki
    Ngoma Africa Band aka FFU bin watoto mbwa,kuwa ujumbe wao unakubalika ,uliomo ktk Cd yao "Rushwa ni hadui wa haki" ambao kwa sasa upo at www.ngoma-africa.com

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 28, 2011

    Ha ha!!!!!!!! danganya watoto wa shule lakini siyo watanzania wa leo. Aibu kweli. Kama ni kweli na wewe ni mtanzania uanetaka kuchapa kazi FUKUZA POLISI WOTE.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 29, 2011

    POLISI KUJIVUA GAMBA NI NGUMU, BILA KUNG'OLEWA NI BURE. IGP ANZA KUSAFISHA VITUO VYA TEGETA NA WAZO KUNA UOZO WA AJABU! TRAFIKI WA ENEO HILI NI VERY CORRUPT UNAWEZA KUONA MAGARI MABOVU YA ABIRIA TOKA WAZO HADI TEGETA YANA PLATE NAMBA ZA MANJANO NA TRAFIKI WAPO BARABARANI. PIA WANATOZA NAULI ZA JUU; MFANO
    1.TEGETA HADI WAZI NI SHS. 300.00(KM4)
    2. WAZO HADI MADALE NI 500.00( KM6)
    KWA HIYO; TEGETA-WAZO MADALE NI SHS 800.00(KM 10)
    KITUO CHA POLISI WAZO KINATIZAMANA NA KITUO CHA DALADALA LAKINI HAKUNA HATUA ZA KUTUSAIDIA WAKAZI WA MAENEO YA MADALE PAMOJA NA KWAMBA HATA MTENDAJI MKUU WA SUMATRA( ISRAEL SAKILASA) ANAISHI MADALE LAKINI NAE HANA LOLOTE JUU YA TATIZO HILI! AIBU KWA SERIKALI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...