Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dkt. Guido Herz, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo kwa ajili ya kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Juhan Toivonen , wakati alipofika ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo kwa ajili ya kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake nchini. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

Na Boniface Makene - OMR

Mabalozi wa nchi za Finland na Ujerumani leo wamefanya ziara katika ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumuaga huku kwa pamoja wakielezea kubakia na kumbukumbu ya namna Watanzania wanavyoishi na walivyowathamini wakati wakifanya kazi za kidiplomasia hapa nchini.

Wa kwanza kufika ofisini kwa Makamu wa Rais alikuwa Balozi Juhan Toivonen kutoka Finland ambaye aliisifia Tanzania na kumzawadia Makamu wa Rais Kitabu cha “The Great Savanna” kitabu kilicho na vivutio kadhaa vya utalii nchini Tanzania ambacho kilichapishwa kwa Kifini na kisha kutafriwa kwa Kiingereza.Balozi huyo alimuahidi kutoa kopi nyingine za kitabu hicho zipatazo 9,000 kwa Makamu wa Rais ili zisambazwe kwa wadau wa utalii nchini.

Kwa upande wake Makamu wa Rais licha ya kumshukuru Balozi Toivonen,alifafanua kuwa uhusiano wa Finland na Tanzania ni wa siku nyingi na wenye tija nchini na kwamba historia inaonyesha kuwa katika fani ya Jiolojia, nchi ya Finland imesaidia sana katika kutanua rasilimali watu hapa nchini.

Katika hatua nyingine Balozi huyo alitaka kujua namna Tanzania inavyomudu kutanua demokrasia kulinganisha na mataifa mengine ya Afrika na Makamu wa Rais akamjibu kuwa, hali hii inatokana na mahusiano chanya kati ya serikali na wananchi na akatilia mkazo juu ya uongozi uliotukuka wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere hasa katika vigezo vya kujenga ushirikiano na hali ya kukubaliana kama Watanzania.

Katika mazungumzo na Balozi wa Ujerumani Dkt. Guido Herz, Balozi huyo aliyekaa nchini kwa miaka mitatu yeye alianza kusifia makubaliano ya kupatikana amani ya kudumu Visiwani Zanzibar huku akifafanua kuwa namna alivyoona tatizo lililokuwepo, alikuwa akiamini kuwa lingetatuliwa na Wananchi wenyewe.

Balozi huyo alifafanua pia kuwa anaamini demokrasia inakuwa nchini na pia akaeleza kuwa siasa za Tanzania bado zina mizizi ndani ya Chama cha Mapinduzi.

Makamu wa Rais alimuelezea Balozi huyo namna Tanzania ilivyojipanga katika sekta ya Utalii huku ikiwaza kuwa na utalii wenye tija lakini usiokuwa na idadi ya watalii wanaofurika na hivyo kuharibu mazingira. 

Suala lingine lililojadiliwa lilikuwa juu ya uchimbaji wa madini ya Uranium huku Makamu wa Rais akifafanua kuwa,kazi hiyo itafanywa kwa uwazi kabisa na tayari hatua za awali za kujitathmini kabla ya kuanza kazi hiyo zimeanza zikiwa chini ya wizara zinazohusika na Madini sambamba na Sayansi na Teknolojia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...