Na Mwandishi Wetu,Mbeya.
Wahandisi wa Maji nchini wametakiwa kuweka kwa makini na kutoa taarifa sahihi zinazohusiana na mikataba na matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Taarifa na Takwimu za Maendeleo ya Sekta ya Maji kuhakikisha kuwa matumizi ya mfumo unakuwa endelevu ili kukidhi malengo yanayotarajiwa katika kuboresha huduma za maji nchini.
Akiongea kwenye mafunzo yanayoendelea nchini juu ya matumizi ya Mfumo huu mkoani Mbeya, Mkurugenzi Msaidizi wa Maji Vijijini Mhandisi Gibson Kisaka, alisema mpango wa Wizara ya Maji kwa sasa ni kuwachukulia hatua Wahandisi watakaokosesha Halmashauri zao kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kwa uzembe wa kutoa takwimu zisizosahihi za matumizi ya fedha za miradi ya maji.
“Mfumo wa Kieletroniki sasa upo hivyo uzembe wa utoaji takwimu sahihi kwa wakati kwa kweli utaathiri Halmashauri husika kupata fedha za miradi ya maji na inabidi sasa wanaohusika kuchukuliwa hatua stahiki kwani wanasababisha wananchi wasio na hatia kutopata huduma za maji’’ alisema Kisaka.
Alizisisitizia Wahandisi wa Maji wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha kuwa mikataba inayosainiwa na matumizi yoyote ya fedha za Sekta ya Maji lazima ziwekwe kwenye Mfumo ili uandaaji wa taarifa ufanyike kwa wakati na kuwezesha upelekaji fedha kwenye Halmashauri ufanyike kwa wakati ili kuzingatia makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo katika utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mratibu wa Mafunzo ya Mfumo huo unaoendelea nchini Joash Nyitambe amesema Wizara ya Maji kwa sasa inaendelea na utoaji wa mafunzo ya vitendo ambapo washiriki wanaweka takwimu zao kwenye mfumo ifikapo mwezi Agusti taarifa za miradi na matumizi yote ya fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ziweze kuanza kupatikana kwenye mtandao wa kompyuta ili kujenga mfumo wa uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma pamoja na matumizi ya fedha za umma zinazohusiana na Sekta ya Maji.
Mafunzo hayo yamekamilishwa kituo cha Morogoro na sasa yanaendelea katika kituo cha Mbeya yakihusisha Wahandisi wa Maji kwenye Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya kutoka mikoa ya Iringa, Rukwa. Ruvuma, na Mbeya.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...