Na Anna Titus-Maelezo
UONGOZI wa Kamati ya Taifa ya Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu umetambulisha alama maalum za Usalama barabarani kwa watu wenye Ulemavu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu Bw.Jutoram Kabatelle amesema wameona haja yakuwa na alama maalum zitakazowalinda watu wenye ulemavu hasa wanapotaka kuvuka barabara.
Bw.Kabatelle amesema barabara zilizopo hazina alama maalum za kumruhusu mtu mwenye ulemavu kuvuka kwa usalama kupelekea ugumu na mashaka katika kuvuka barabara.
“Zipo alama za kawaida katika kuvuka barabara ambazo haziwasaidii watu wenye ulemavu hasa kutokana na uharaka unaohitajika katika utembeaji wakati wakuvuka.” Alisema Bw. Kabatelle.
Ameelezea kuwa kutakuwepo na alama tano maalum kwa walemavu wa macho, walemavu wa viungo,walemavu wa ngozi,watu wenye ulemavu wa kusikia pamoja na walemavu wa akili.
Aidha Bw.kabatelle amesema kuwa kuwepo kwa alama hizo katika maeneo maalum kama mashuleni,vyuoni ,hospitalini,sehemu za burudani pamoja na huduma za kijamii zitawatambulisha madereva muda wote kuwa na tahadhari ili kuwalinda watu hao kuvuka kwa usalama.
Wakati huo huo amewaombaka wenye magari ya biashara kuagiza magari yenye miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ilikuzingatia mahitaji maalum ya wenye ulemavu.


maofisini, mashuleni, mahotelini, hakuna alama au vifaa hivyo. mfano vyoo vya wenye vilema, njia zao za kupita, maofisini na penginepo hakuna!! au mnadhani wenye ulemavu ni wale vipofu tu? rekebisheni hata majengo yaendane na hali halisi bila kubagua
ReplyDelete