Kama mmoja wa wanao tamani kua sehemu ya wasomi na wataaluma Tanzania, wasomi na wataaluma wenye tija kwaajili ya maendeleo ya Tanzania; tamaa hiyo inanisukuma kuongea kile ninacho kifikiri kinaweza kua sehemu ya mchango wa mawazo yangu. Kwakua inawezekana mawazo haya yasiwe sahihi basi nitaomba kukosolewa.
Yamesemwa mengi kiasi kwamba ninahisi nawezakua ninarudia japo ninapata faraja ya kuendelea kuandika kwa kuamini kuwa kurudia ni sehemu ya kukumbushana hasa katika kuelimishana kwa yale tuyaaminiyo kuweza kuwa ya maana na ya msingi kwetu.

Elimu katika Nyanja zote (kijamii, sayansi aina zote na teknolojia mbalimbali) inasambaa karibia pande na kona zote nchini Tanzania. Haya ni maswali tunayoweza kujiuliza-pengine ambayo yamenisukuma kuandika makala haya: -
1.     Elimu hii ni ya kiwango (quality) gani? 2. Elimu hii ni kwaajili ya nini au malengo yake ni nini kitaifa? 3. Ni kwa baada ya mda gani na kinatarajiwa kitu gani kama zao la elimu hii kwaajili ya kupambana na changamoto za maendeleo ndani na nje ya Tanzania (kwenye Global economy, Technological advancement and industrialization…etc)?

Ninafikiri ni maswali ambayo kwa namna moja ama nyingine wasomi na wataaluma wetu, watawala wetu, wanasiasa wetu na wanaharakati wetu Tanzania watakua ama walipaswa kujiuliza na kutoa majibu sahihi tangu elimu za aina zote zianze kutolewa kabla na baada ya kujitawala na sasa ikiwa ni miaka 50 ya kujitawala.

          Nitakua mnafiki, mwongo na mpuuzi nikisema kwamba elimu ya Tanzania na elimu waliyo nayo wasomi wetu nchini haisaidii ama haijasaidia! Swala linakuja imesaidia kwa kiwango gani na tunahitaji/tulihitaji kiwango kipi? Ukweli unabaki kuwa kiwango chake hakijajitosheleza tukilinganisha na kiwango ambacho nchi jirani ambazo pengine tumezisaidia sana na zilikua nyuma yetu karibia kwa kila kitu kama Burundi, Rwanda, Kenya….nk… Pia tukilinganisha na changamoto ambazo wasomi,wataaluma na wataalamu wetu wanakutana nazo kwenye soko la ajira (technological experts’) ndani,  East Africa, Africa na duniani kote. Upungufu bado ni mkubwa!

          Ni mabadiliko ya maendeleo ya kitechnolojia yaliyotokana na mabadiliko ya kimakusudi na maono (vision) ya ELIMU mahususi yaliyosababisha na kuendelea kusababisha mabadiliko chanya ya kiuchumi na kuwepo kwa nchi tajiri duniani na sisi watanzania kuendelea kuitwa maskini duniani! Japo vitabu vilivyokua vikitoa elimu hizi havitofautiani duniani tukiachilia lugha tu!

          Ninaamini, Watanzania tuna akiri sana na niwabunifu pia tuna uwezo mkubwa sana tukiwezeshwa, tukathaminiwa, tuka-aminiwa na kutumiwa! Ni kwa mabadiliko ya kimakusudi na maono (vision) ya elimu mahususi kwa watanzania itakayo kua na tija ya kuleta mabadiliko ya maendeleo ya kiteknolojia na hatimae mabadiliko chanya ya maendeleo ya kiuchumi yatakayo badilisha jina la Tanzania kua moja ya nchi tajiri duniani.
MAPENDEKEZO:-
Pamoja na kutambua kua kila mtanzania kwa nafasi yake mimi nikiwa mmojawapo tunawajibika kutumia elimu zetu kwa maslahi yetu sisi wenyewe na Taifa letu; ninapendekeza yafuatayo:-

Ø *Sisi tulio wasomi, wataaluma, wataalamu na tunaosoma -tuone umuhimu wa kujiamini, kuonyesha uwezo na ubunifu wetu bila woga, pia wajibu zetu kwa kujaribu kwani tunaweza. Badala ya kulalamika tu!
Ø *Serikali yetu iweke lengo (Target) la elimu inayohitajika kwaajiri ya watu wake zaidi ya kuwaandaa kuwa wanasiasa pekee. Binafsi ninge pendekeza lengo liwe kujitegemea kiteknolojia zaidi na viwanda kwa kutumia wataalamu wa ndani walioandaliwa na kuaminiwa kuliko ilivyo sasa.

Ø *Tanzania (Serikali) inapaswa kupeleka/kujenga vyuo vingi vya fani za ufundi (stadi za kazi) kama VETA; fani kama vile za ujenzi, uashi,   seremara, ushonaji, utunzaji wa vyakula (food processing)…nk katika mikoa yote kama ilivyojenga shule za sekondari za kata kwani kutaongeza wajasiliamali wengi na nafasi za kujiajiri nyingi na kwavijana wengi Tanzania!

Ø *Wasomi na wataaluma wa ndani wathaminiwe, wawezeshwe, waaminiwe na kutumiwa vema kwenye tafiti za kisayansi na teknolojia (tafiti hizo zifanyiwe kazi) na maeneo mengine ya kimaendeleo na uchumi! Mfano ni nchi zilizokua za USSR, CHINA ambazo zimefankiwa kwa haraka sana kwa kutumia watu wake na sasa masha yao huwezi yafananisha na nchi kama Tanzania yenye kilakitu (raslimali zote muhimu)!

Ø *Serikari kwa kushirikiana na viongozi wa shule za ngazi zote na vyuo vya ngazi zote nchini waone umhimu wa kuwekeza kwenye elimu kwa vitendo badala ya nadhalia tu.

Ø *Serikali iwawezeshe wasomi na wanataaluma wake wa ndani kuonesha uwezo wao wa kitaalamu na utafiti wa kisayansi (scientific researches)-kwenye Natural Sciences and technologies hasa!

Ninaamini kwa kufanya hayo niliyo yataja tunaweza kupunguza uwezekano wa wawekezaji wetu kuja na watu wao na hivyo watanzania kupata nafasi nyingi za ajira na pesa yetu kubaki kwetu! Pia thamani ya wasomi wetu itaongezeka.
 Ahsanteni Sana.
Author: FURAHA JACOB NDABILINDE; 
From Ngara-Kagera-Tanzania; 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Tatizo la bongo ni kuwa waliopo madarakani hawaondoki, hivyo kukosesha wasomi vijana kupata nafasi wakati muafaka wakiwa bado akili zao hazijachoka.Kuna viongozi toka enzi za TANu bado wapo kama sio wao basi watoto wao ,ni staili ya kurithishana vyeo.
    Mpaka wazee waking'amuka na hao wasomi vijana nao washazeeka au ndio nao washakuwa na familia kubwa na akili haiwezi kufanya kazi tena, anafikiria kuiba na ubinafsi.
    Kuna vingozi wana kashfa kibao lakini bado wanalindana na ndipo uozo unapoendelea hadi hii leo(maji,umeme,mafuta,barabara,nk).
    Naamini kuwa ipo siku tutaliona hili na tutapeana kazi kwa kiwango/ujuzi wa muomba kazi na sio kwa kujuana.

    ReplyDelete
  2. WaTZ wana elimu na wanapenda kusoma. lakini elimu pekee haitoshi, maana kiwango kikubwa kabisa cha elimu ni uprofesa. Tanzania ina maprofesa wengi sana. Sasa tujiulize hawa maprofesa wanafanya nini? Wengi wao wanachofanya ni kusomesha na kusimamia wanafunzi hawana jengine. Hii haitotupelekea kupata maendeleo. Nchi za ughaibuni zinategemea vipaji na juhudi vya watu wao. Kama una kipaji fulani mfano unataka kutengeneza kifaa fulani, hawa jamaa wanaangali pendekezo lako na wakiliona linaweza kuleta mafanikio wanakutafutia mtaji wa kulitekeleza. Aliyevumbua computer alipewa mtaji na serikali ya Marekani. Sasa sisi TZ hatuna watu wenye vipaji vya kutafuta vifaa vipya na pia hatua uwezo wa kuvigharamia. Maendeleo yatachukua muda mrefu kufika. Angalia kwenye maonyesho ya Nane Nane kumeonyeshwa ufugaji wa kuku wa kiwanda. Sasa wenzetu wamefanya huo utafiti muda mrefu sasa na wanautumia miaka mingi iliyopita, kwao sasa kila mtu anakula kuku kwa bei ndogo. Wakati sisi Uswazi ndio kwanza tunaibiana kuku!

    ReplyDelete
  3. Bwana Furaha Jacob. hoja yako uliyoitoa ni ya msingi kabisa. ni kweli kabisa watu kama nyie wenye muono chanya na kuona mbali ndio wanatakiwa katika Taifa letu ili tuweze kujikwamua katika matatizo haya yanayotukabili na ambayo hayana muelekeo kama yanapungua bali yanaongezeka tu kila kukicha. pia napenda kukupongeza kwa kutumia Lugha yetu ya Taifa Kiswahi kwani wengi wataweza kusoma na kuandika. pia jaribu kutafuta namna uweze kufnya mawazo yako pia yawe yanafika sehem husika na usiishie hapa kwa michuzi tu. kwani yoyote mwenye nia ya maendeleo atakubaliana na mawazo yako. keep it up kazi nzuri sana.

    ReplyDelete
  4. Nimependa makala/article yako bwana Jacob,na nina uhakika Tanzania ikipata vijana na wasomi kama wewe wenye akili yenye mwamko endelevu basi tutafika mbali i guess.Namuunga mkono mdau hapo juu kuwa ujitahidi fikra kama hizi kufika sehemu husika zaidi..ili ziweze kufanyiwa kazi!I hope huu ni mwamzo tutegemee mengi zaidi kutoka kwako.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...