CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA).


Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana katika Mkutano wa Dharura uliofanyika siku ya Jumamosi na Jumapili tarehe 06 Agosti 2011 katika Hoteli ya Imagi Mjini Dodoma. Pamoja na mambo mengine Ilifikia maamuzi yafuatayo :

1. Kamati Kuu ilipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo iliyoyatoa katika Mkutano wake wa tarehe 17 Julai 2011 iliyowataka madiwani wa CHADEMA Arusha kujiuzulu nafasi walizozipata pamoja na kuomba radhi kwa makosa waliyoyafanya kutokana na mwafaka uliofikiwa baina yao na madiwani wenzao wa TLP na CCM kwa kuwa chama hakikuridhia wala kuutambua mwafaka huo.


2. Kamati Kuu imezingatia kuwa, kati ya madiwani 10 waliopewa maelekezo na Kamati Kuu, madiwani watano (5) ndio wametekeleza maelekezo kikamilifu wakati madiwani wengine watano (5) wamekataa kuyatekeleza maelekezo hayo.


3. Baada ya kutafakari kwa kina taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kuu, na kuwapa nafasi ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu Madiwani ambao walikuwa hawajatekeleza maelekezo,Kamati Kuu imezingatia kuwa madiwani wamekataa kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu.


Aidha, Kamati Kuu imezingatia kuwa kitendo cha madiwani kukataa kutekeleza maagizo halali ya Kamati Kuu ni utovu mkubwa wa nidhamu na ni kuvunja maadili na kanuni za chama, na kinaenda kinyume na msingi mama wa CHADEMA wa uwajibikaji.


Hivyo basi, kwa kutumia mamlaka ya Kikatiba Kamati Kuu imewafukuza uanachama madiwani watano wafuatao kwa kosa la kukataa kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu:


i) Ndugu Estomih Mallah


ii) Ndugu John Bayo


iii) Ndugu Charles Mpanda


iv) Ndugu Rehema Mohamed


v) Ndugu Reuben Ngowi

Watajwa hapo juu wamejulishwa maamuzi ya Kamati Kuu ndani ya Mkutano tarehe 07 Agosti 2011 saa 7:57 usiku, Aidha, kila mmoja wao atakabidhiwa barua yenye kueleza maamuzi ya Kamati Kuu.


4. Aidha, Kamati Kuu imepokea taarifa ya mazungumzo baina ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe Freeman Mbowe, na Waziri Mkuu, Mhe Mizengo Pinda, juu ya nia na azima ya kumaliza tatizo la mgogoro wa umeya Arusha, waliyoyafanya asubuhi ya siku ya Jumamosi, Tarehe 06 Agosti 2011 nyumbani kwa Waziri Mkuu Mjini Dodoma.

Kamati imezingatia kuwa:


a. Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Waziri Mkuu wamekubaliana kuunda Kamati ya Kitaifa ya kushughulikia mgogoro wa umeya wa Arusha itakayojumuisha wajumbe kutoka sehemu mbili zinazohusika katika mgogoro huu ambazo ni CCM na CHADEMA

b. Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano itaundwa haraka iwezekanavyo, na kwa vyovyote mgogoro wa u meya Manispa ya Arusha ulikubalika uishe ndani ya mwezi mmoja tangu tarehe ya mazungumzo ya Mwenyekiti wa Taifa na Waziri Mkuu


c. Uenyekiti wa Kamati ya Kitaifa utakuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Ndugu John Tendwa, na kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa ataratibu uundwaji wa Kamati hiyo ya Kitaifa.

5. Kamati Kuu imetambua juhudi za Waheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe Freeman Mbowe, kwa hatua yao chanya ya kumaliza mgogoro wa Arusha.

6. Pamoja na hatua njema kuelekea kumaliza mgogoro wa umeya Arusha, Kamati Kuu ya CHADEMA itaendelea kusitisha kumtambua rasmi Meya wa Arusha hadi pale mazungumzo yaliyoanishwa hapo juu yatakapokamilika na mwafaka bayana kupatikana.


Imetolewa na:
Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe (Mb)
MWENYEKITI WA TAIFA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Fukuza woooooooote wanaoleta za kuleta. Sisi sera yetu ni ubabe, vitisho, tribalism, fujo na kunyenyekea walio mamlakani.
    Safi sana CHADEMA. Nadhani next Bwana Lema naye anatakiwa afukuzwe maana ndiyo kiini cha matatizo
    Mdau

    ReplyDelete
  2. Huu ni mwanzo katika kuelekea utawala wa sheria na uhuru wa kujieleza. lazima tukumbuke,nchi ni watu na wanaingoza nchi ni watu kwa kufuata utaratibu wa kisheria na kikatiba. Hivyo taratibu hizo zinapotumiwa vibaya na wahusika matokeo yake wanaumia wananchi kwani wao ni nyasi wakati mafahali wanapigana kwa kutofuata mfumo na utawala wa kisheria. Aidha jamii yeyote inapokosa maadili na na uaminifu basi matokeo yake ni mabaya sana. viongozi wanapoteza muda kujadili majungu, malumbano na chuki binafsi wanasahau kuwakilisha wananchi.

    ReplyDelete
  3. watanzania mnataka nini?

    CCM wanasita kufuza wanachama mnapiga kelele, CHADEMA wanatimua watu mnapiga kelele. du! hamjui mnalolitaka.

    ReplyDelete
  4. Huu ni unafiki wa hali ya juu kabisa. Demokrasia halisi huanza ngazi ya chini kabisa, yaani kwa watu/wananchi kisha ikapanda juu. Chadema walichokifanya ni udikteta tu wa kutaka amri ya wakubwa itekelezwe na wananchi (grassroots). Be that as it may, Chadema haitapata umeya Arusha ng'oo as long as kyadema wana madiwani wachache kuliko CCM na TLP hata huyo bw "funga milango tupigane" akitambika uchi wa mnyama.......

    ReplyDelete
  5. Wakati wa kampeni wazawa na wenyeji wa A-town tulikuwa tukimwita Lema 'tapeli' sasa hivi tunamwita 'mheshimiwa migogoro'.

    ReplyDelete
  6. aahh mm ni mwanachama wa chadema, anyway sijui madiwani walichokaidi ila mm naona too much sasa kufuatilia. huu nadhani ni muda wa kufanya kazi na nsi kampeni, tunapoteza muda mwingi kwa story tu ambazo hazina maslahi> wangeonywa nadhani inatisha.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...