Mechi ya mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon katika ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Algeria (Desert Warriors) itachezwa Septemba 3 mwaka huu jijini Mwanza.
 
Awali tulipanga mechi hiyo ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Lakini uamuzi wa kuihamishia Mwanza umefanyika baada ya jana kupata barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikitufahamisha kuwa Uwanja wa Taifa hautatumika tena kwa sasa. Kwa mujibu wa Wizara, uwanja huo utakuwa katika matengenezo baada ya kuharibika wakati wa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita.
 
YANGA, SIMBA NAZO KUATHIRIKA
Uamuzi huo wa uwanja kufungwa kwa ajili ya matengenezo pia umeziathiri klabu za Yanga na Simba ambazo zilikuwa zimekubaliwa timu zao zitumie kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu.
 
Tayari leo (Agosti 18 mwaka huu) tumeziandikia rasmi klabu za Simba na Yanga kuzifahamisha kuhusu uamuzi huo wa Wizara, hivyo kuzitaka zitafute viwanja vingine kwa ajili ya mechi zao za ligi.
 
Hatua hiyo ya uwanja kufungwa, itailazimisha TFF ifanye mabadiliko kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuzingatia viwanja ambavyo klabu za Yanga na Simba zitakuwa zimeamua kuvitumia.
 
Mabadiliko hayo pia yataziathiri timu za African Lyon, Azam, JKT Ruvu, Moro United na Villa Squad ambazo licha ya kutumia Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam, zilipanga mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Taifa.
 
Kwa sasa msimamo wa wamiliki wa Uwanja wa Azam ni Yanga na Simba kutoutumia kwa vile uwezo wake wa kuchukua watazamaji ni mdogo.  
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Hii ni serikali ya ajabu sana, wanatoa taarifa wakati zimebaki siku mbili ligi kuanza!! Wanategemea timu zitapangaje bajeti na kutafuta pesa za kupeleka timu mikoani kwa ghafla hivyo? Inabidi timu zigomee ligi na wizara iwajibike.

    ReplyDelete
  2. kwani uwanja wa uhuru si upo?

    ReplyDelete
  3. yaani hiri ri nchi rinaendeshwa kijeshi tu, mtu anaamka na kujiamulia tu vitu wakati watu wamepoteza muda wao na pesa kujipangia mikakati yao.

    ReplyDelete
  4. ifike mhali timu zijenge viwanja vyao sio kila siku kutegemea uwanja wa taifa tu hayo ndiyo matatizo yake je hizo timu za simba na yanga zingekuwa mikoani zingekuja kucheza kwenye uwanja wa taifa? tubadilikeni jamani timu kongwe hata uwanja wa mazoezi hamna? mimi naona sawa tu tena wapigwe kabisaa marufuku kuchezea ligi hapo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...